Na Mwandishi Maalum
SHUGHULI za Royal Tour zilizokuwa zikifanywa kwa mara ya kwanza nchini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya Utalii, Biashara na Uwekezaji nchini zimeanza kuzaa matunda kwa wawekezaji kuanza kujitokeza kwa uwekezaji wa hoteli za kisasa ndani ya hifadhi za Taifa. Hayo yamebainishwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro mara baada ya mkutano wake maalum na Wawekezaji uliofanyika Dar es Salaam mapema leo. Ambapo amekutana na wawekezaji hao kutoka Bara la Ulaya katika nchi ya Bulgaria watakaojenga hotel za Nyota tano 'brand' za Kempinski kwenye hifadhi Nne za Taifa nchini. Waziri Dk. Damas Ndumbaro amesema mpango mkakati wa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kuandaa kipindi cha Royal Tour umeweza kuzaa matunda hayo na wao kwa Wizara wameupokea kwa kwa sasa ni utekelezaji. ''Juhudi kubwa za kimkakati za Royal Tour zilizoendeshwa na Rais wetu zimeweza kuzaa matunda ambapo leo tumepokea wawekezaji mahiri kutoka Bara la Ulaya ambao watawekeza kwenye hoteli kwa kujenga hoteli tatu za nyota tano za 'brand' ya Kempinski kwa uwekezaji wa Dola za Kimarekani Milioni 72. [USD 72 Milioni]. ''Mkutano wetu huu hii leo umekwenda vizuri sana na Wawekezaji hawa kwa hiyo unaweza kuipata hoteli ya Kempinski baada ya ujenzi huo kukamilika. .. Kempinski Serengeti, Kempinski Manyara, Kempinski Tarangile na Kempinski Ngorongoro." Alisem Dk. Ndumbaro. Waziri Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, ujenzi huo ni mkubwa sana na unakadiriwa kuanza rasmi mwezi Januari 2022 ambapo amemshukuru kwa mara nyingine Mhe Rais kwa kuwezesha kuwapigia 'pass' na wao kupitia wizara ya Maliasili ni utekelezaji ikiwemo kupokea Wawekezaji katika sekta hiyo ya Utalii. ''Tunaenda kasi tayari hii Royal tour kwangu mimi kama Waziri na Wizara ya Utalii na Maliasili kwa ujumla wake tunaichukulia kama 'pass' ya mwisho katika mpira, unapopewa pasi ya mwisho kazi yako wewe ni kufunga tu. Kwa hiyo sisi tumeshafunga 'Goal' lingine hilo kuhakikisha kwamba Royal Tour inakuwa na mafanikio zaidi'' alimalizia Waziri Dkt. Damas Ndumbaro. Agosti 28, mwaka huu Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alianza rasmi kurekodi vipindi vya Royal Tour maeneo mbalimbali ya vuvutio vya utalii na uwekezaji ikiwemo Tanzania Bara na visiwa vya Zanzibar. Ambapo katika ziara hiyo ya kuandaa vipindi hivyo kutembelea na kuonesha kwa wageni vivutio mbalimbali vya Utalii, Uwekezaji, Sanaa na Utamaduni vilivyopo nchini na kwa sasa matunda yake yameanza kuonekana. |
No comments:
Post a Comment