BILIONI 87 KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA WASSO HADI SALE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 25 September 2021

BILIONI 87 KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA WASSO HADI SALE

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Arusha, Eng. Reginald Massawe, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Loliondo hadi Mto wa Mbu (km 217), Awamu ya Kwanza ya Wasso hadi Sale (km 49), kwa kiwango cha lami.



Muonekano wa sehemu ya barabara ya Wasso hadi Sale (km 49), inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Arusha. 

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu hadi Loliondo (km 217) awamu ya kwanza inayohusisha eneo la Wasso hadi Sale (km 49), kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi za kitanzania Bilioni 87.

Akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Naibu Waziri Kasekenya amamtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo kukamilisha ujenzi huo kwa mujibu wa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba ifikapo mwezi Aprili mwaka 2022.


“Barabara hii ni muhimu sana kwa Serikali kwani kukamilika kwake kutarahisisha biashara ya usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara, lakini pia kukuza utalii kwani kupitia barabara hii watalii wanaweza kuona mlima wa Oldonyo Lengai lakini pia kufika kwa urahisi katika mbuga ya wanyama ya Serengeti,” amesema Mhandisi Kasekenya.


Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kukuza uchumi na hatimae kutokomeza tatizo la umaskini kwa wananchi hususani wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo ambao kwa sasa wamekuwa wakipata adha ya usafiri hasa nyakati za mvua. 


Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU), Mhandisi Mbaraka Shafi, amemuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Wasso hadi Sale umefikia asilimia 88 na kuwa tayari madaraja 19 yameshajengwa, madaraja madogo 105 kati ya 107 yamekamilika na tayari kilometa 18.4 zimewekwa tabaka la mwisho la lami na kazi ya kukamilisha sehemu iliyobaki inaendelea.


Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amemuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa  Barabara ya Mto wa Mbu hadi Loliondo ina jumla ya urefu wa kilometa 217 na kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa kwa awamu hivyo awamu inayofuata itakuwa ni kuanzia Sale hadi Ngaresero River yenye urefu wa kilometa 57.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi


No comments:

Post a Comment