Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu masuala mbalimbali ya tozo za miamala ya simu leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu masuala mbalimbali ya tozo za miamala ya simu leo Jijini Dar es Salaam kulia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile.
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema Serikali imesikia kilio na maoni ya wananchikuhusu tozo mpya ya miamala ya simu na kuwaomba wawe watulivu wakati jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari akiambatana na Waziri wa Teknolojia ha Habari na Mawasiliano Dkt. Faustine Ndugulile.
“Kwa maaneo ambayo wananchi wametoa ushauri na kuelezea namna ambavyo jambo hili linawagusa lakini pia tumepokea maeneo ambayo yanatakiwa kutoa elimu zaidi ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa ni pamoja na viwango vinavyokatwa kwa nayetuma na anayetoa lakini pia kuhusu mantiki ya jambo lenyewe” alisema Mhe. Mwigulu
Alisema kuwa jambo la tozo za miamala linatekelezwa kupitia sheria iliyopitishwa na Bunge lakini kuna kanuni za utekelezaji zinazo mhusu yeye kama Waziri wa Fedha na Mipango na maeneo mengine yanahusu Wizara ya Teknollojia ya Habari na Mawasiliano ambazo zitajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Dkt. Nchemba alisema kuwa siku ya Jumanne tarehe 20 Julai, 2021 kutakuwa na kikao kilichoitishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kujadili suala hilo na pia kutakuwa na kikao kingine cha Mawaziri wa Wizara zote kuchambua kwa kina suala hilo.
“Lakini Tayari Mheshimiwa Rais naye alishaguswa na jambo hili amesikia maoni ya watanzania wote na yeye ametolea maelekezo kwamba tuyafanyie kazi maoni hayo, Nitoe Rai kwa wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili tutaendelea kuelezea na kutoa ufafanuzi kwenye kila maeneo yanayohitaji ufafanuzi na tutachukua hatua kwenye maeneo ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua ili ujenzi wa taifa letu uweze kuendelea kama ambavyo wananchi wamekuwa na shauku kubwa kuona ujenzi wa Taifa letu unaendelea kwa ajili ya maendeleo ya nchi” Aliongeza Dkt. Nchemba
Dkt. Nchemba aliwaonya wale ambao wana nia mbaya ambao mara zote wapenda kupotosha ama kubadili dhana ya maana halisi ya jambo ambavyo lilikuwa limekusudiwa na kuwataka wasifanye hivyo, kwani mambo haya yana maslahi mapana kwa nchi.
“Haya ni mambo ambayo ni ya kisheria, sheria za nchi zinatakiwa kuheshimiwa, ni mambo ambayo ni ya kikanuni na mambo yanayohitaji uelimishaji tutaendelea kufafanua lakini yale yanayotakiwa kufanyiwa kazi niwaahidi watanzania tutaendelea kuyafanyiakazi kama ambavyo viongozi wetu wakuu wamesema” Alisisitiza Mhe. Nchemba
Alisema tayari aliwapa maelekezo wataalam wa mifumo kuangalia vipengele vya Sheria ya mifumo ya malipo Serikalini pamoja na Sheria ya Mawasiliano ya Mtandao (EPOCA) inayoelezea kuhusu masuala ya miamala kwa njia ya mtandao na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kufikia muafaka wa jambo hilo.
Alitoa Rai kwa watanzania waendelee kumuunga mkono Mhe Rais katika Dira yake ya kuhakikisha anasukuma mbele shughuli za maendeleo ya nchi na ili tuwakomboa na kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Dkt. Faustine Ndugulile alibainisha kuwa Wizara yake pia ambayo inaguswa moja kwa moja na tozo hizo imeendelea kupokea maoni na kuchakata taarifa mbalimbali tangu tozo hiyo ianzishwe na kumwahidi Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atampa ushirikiano kuhakikisha kwamba maelekezo yaliyotolewa na viongozi yanatekelezwa.
Alirejea kutoa wito kwa watanzania kuwa watulivu wakati jambo hilo linafanyiwa kazi na kusema kuwa Serikali ni sikivu na itafikia muafaka mzuri.
No comments:
Post a Comment