RC MKIRIKITI AAGIZA FORODHA KILANGAWANA SUMBAWANGA KUANZA KAZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 29 July 2021

RC MKIRIKITI AAGIZA FORODHA KILANGAWANA SUMBAWANGA KUANZA KAZI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti (kushoto) akiwa pamoja na viongozi wa wilaya ya Sumbawanga wakibeba nondo maalum kwa ajili ya ujenzi wa nguzo za jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga iliyopo Laela. Akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ndogo ya ujenzi wa mradi huo tangu mkataba uliposainiwa mwezi Juni mwaka huu ambao utagharimu shilingi Bilioni Moja.

MKUU wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti Julai 28 ametatua mgogoro uliodumu kwa miaka 27 baina ya wananchi na pori la akiba Uwanda ambapo wananchi wamekuwa wakizuiwa kupita kwenye pori la akiba la hifadhi wanapokwenda kuvua samaki Ziwa Rukwa.

Mkirikiti ametoa agizo hilo alipokuwa akiongea na mamia ya vijana na wananchi wa kijiji cha Kilangawana na Ilambo kata ya Kilangawana ambapo ameiagiza halmashauri ya Sumbawanga na hifadhi ya pori la akiba la Uwanda (TAWA) kuanzisha kituo cha forodha kwa ajili ya kukata vibali na ushuru kwenye kijiji hicho hatua itakayoondoa usumbufu wa watu. 


"Kuanzia sasa awepo Afisa Uvuvi hapa Kilangawana atoe huduma ya forodha kwa wavuvi bila kikwazo, nataka TAWA msisumbue wananchi wenye vibali," alisema Mkirikiti.

Kijiana Frank Solokoto wa kijiji cha Ilambo alisema kero ya ukosefu wa forodha inawafanya wasafiri umbali mrefu kilometa 40 hadi kijiji cha Legeza kufuata huduma ya forodha na pia imesababisha askari wa pori la akiba Uwanda kuwakamata na kunyang'anya pikipiki na kudaiwa rushwa.


"Mhe. Mkuu wa mkoa mwaka Jana nilikuwa natoka kuvua samaki nikapita njia inayokatiza kwenye hifadhi ya Uwanda nikakamatwa wakaninyang'anya pikipiki, baada ya kuwapa kiasi wakaniachia ila wakabaki na pikipiki, kwa kuwa kazi yangu ni kuvua samaki nikatafuta pikipiki ingine ambayo nayo walinikamata nayo, pikipiki hizo zimeuzwa na mahakama, sina kazi hapa sina pesa hata mia ya matumizi naomba msaada wako mkuu!!." Alisema Frank.


Mkuu wa mkoa huyo baada ya kusikia kilio hicho alimuita Frank na kumpatia shilingi elfu kumi ya matumizi papo hapo huku wananchi wakishangilia kwenye mkutano wa hadhara.

Frank alimshukuru Mkuu wa mkoa na kukiri makosa ya kupita hifadhini kinyume cha Sheria na kuomba ili kuondoa tatizo la wananchi kukamatwa hifadhini serikali ifungue forodha ya Kilangawana.

"Mkuu wa mkoa ahsante sana, forodha ya Kilangawana ikifunguliwa tutaokoa mapato na kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kukamatwa na wahifadhi wa Uwanda, naomba forodha ifunguliwe ya Kilangawana." Alisema Frank.

Maombi hayo yalipata Baraka ya Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta ambaye alimueleza mkuu wa mkoa mkutanoni hapo kuwa hata halmashauri iliwahi kupokea malalamiko hayo na kuyawasilisha kwa maandishi katika ofisi ya maliasili lakini hawajajibu.

Mkuu huyo wa Mkoa yupo kwenye ziara ya kazi kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwemo kutoa elimu ya kujikinga na UVIKO-19 kwenye Halmashauri za mkoa wa Rukwa.


No comments:

Post a Comment