BENKI YA NMB YATOA MSAADA WA SH. MILIONI 68 KWA MKOA WA MARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 18 July 2021

BENKI YA NMB YATOA MSAADA WA SH. MILIONI 68 KWA MKOA WA MARA

Mkuu wa Mara Ally Hapi (wa pili kulia) akipokea vitanda 8 vya kujifungulia akina mama kutoka kwa Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi Buhare kwa ajili ya Hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kushoto ni Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk. Joachim Eyembe na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dk. Alfany Haule (kulia).



Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori (kushoto) akimkabidhi viti na meza 157 kwa Meya wa Manispaa ya Musoma Kapteni William Gumbo, kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi Buhare-Musoma, ambapo NMB imetoa mabati 750, madawati 157 kwa ajili ya shule za mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu uwajibikaji wake kwa jamii.


Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori katika picha ya pamoja na baadhi ya Walimu wa shule zilizonufaika na msaada wa madati na vifaa vya kuezekea mara baada ya hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya msingi Buhare - Musoma


BENKI ya NMB imetoa msaada wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 68 kwa ajili ya kusaidia Sekta za Elimu na Afya mkoani Mara. Msaada huo utazinufaisha shule 11 za Msingi na Sekondari (Rorya na Musoma) pamoja na Hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa iliyopo wilaya ya Musoma.

Msaada huo ni madawati, vifaa vya kuezekea madarasa pamoja na vitanda maalum vikiwa na godoro na mashuka yake.


Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kukabidhi vifaa hivyo wilayani humo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori alisema kuwa benki yake itaendelea kuunga mkono serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika Sekta ya Elimu na Afya, kwani NMB inatambua umuhimu wa Sekta hizo katika ustawi wa jamii.


Kimori alibainisha kuwa, benki hiyo tayari imekwishatumia zaidi ya Sh, bilioni 1.88 kuanzia mwezi Januari mwaka huu  hadi sasa kuzisaidia Sekta hizo - ambapo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, msaada huo umezinufaisha shule na vituo vya kutolea huduma za afya 129 huku mkoa wa Mara ukiwa umepokea jumla ya madawati 587, mabati 2,580 na vitanda 8 katika kipindi hicho.


Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi aliishukuru NMB kwa msaada huo na kuwapongeza kwa juhudi za kusaidia jamii inayowazunguka kwa kutenga 1% ya faida yao baada ya kodi kutatua changamoto katika Sekta ya Elimu, Afya na Majanga.


Hapi alieleza kuwa, msaada huo waliopokea kutoka NMB utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba uliokuwepo katika Sekta hizo mbili mkoani humo. Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutumia bidhaa mbali mbali za benki hiyo ili waweze kunufaika nazo hasa katika kuweka akiba kwa ajili ya baadae.


Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk. Joachim Eyembe pia aliishukuru NMB kwa msaada wa vitanda huku akisisitiza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha huduma zitolewazo hospitalini hapo, ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za kibingwa tofauti na zile za mama na mtoto za siku zote.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Prof. Philemon Sarungi wakifurahia baada ya kukabidhiwa viti na meza 50, kutoka Benki ya NMB kwenye hafla iliyofanyika shuleni hapo katika kijiji cha Minigo, wilayani Rorya mkoani Mara.


No comments:

Post a Comment