RAIS DK. HUSSEINMWINYI AISHAURI WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 18 July 2021

RAIS DK. HUSSEINMWINYI AISHAURI WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE...!

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  ameishauri  Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale  kuandaa Kalenda maalum ya kufanyika kwa Mashindano ya Kimataifa ya  Marathon  (Zanziar International Marathon ) , ili kuwawezesha wadau wa sekta hiyo kuzitangaza mbio hizo katika Maonyesho ya kimataifa ya Biashara na Utalii, yanayofanyika kila mwaka.

Dk. Mwinyi ametoa ushauri huo katika Uwanja wa Amani jijini Zanzibar katika Mashindano ya Kimataifa ya  Marathon 2021 (ZIM 2021)  zilizoanzia Forodhani Jijini Zanzibar, na kuwashirikisha wanariadha kutoka ndani na nje ya Zanzibar pamoja na wananchi kwa ujumla. Amesema uandaaji wa Kalenda hiyo  utaendana na madhumuni ya msingi ya kurudishwa mbio hizo, sambamba na kuitumia njia hiyo kama moja ya vivutio vya kukuza sekta ya utalii,  kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.  

Alisema Serikali itatoa ushirikiano katika kuendeleza michezo mbali mbali pamoja na kuhakikisha mbio za   Kimataifa za  Marathon  zinafanyika kila mwaka hapa Zanzibar, ikiwa ni  hatua ya kutoa wanariadha wenye vipaji na uwezo  wa kushindana Kimataifa. Dk. Mwinyi aliwapongeza waandaji wa mbio pamoja  na Uongozi wa  Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kurejesha mbio hizo pamoja na juhudi wanazoendelea kuchukua, ili kuleta ushindani katika riadha, wakati huu ambapo hamasa imepungua.

“Nimefarijika sana tumeweza kuzirudisha tena mbio hizi zilizositishwa kuandaliwa na hatimae kutoweka kabisa kwa zaidi ya miaka kumi sasa”, alisema.

Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Awamu ya nane inahamasisha ubunifu na kuandaa mazingira mazuri zaidi ya kisera na kisheria, ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Alisema katika kuimarisha sekta ya Utalii, Serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha miundombinu mbali mbali ya michezo kwa kiwango cha Kimataifa ili michezo hiyo  iwe sehemu ya kukuza utalii. Dk. Mwinyi alisema Serikali ina azma ya kufufua mashindano ya Triathlon yanayojumuisha michezo ya kuogelea, mbio za baiskeli pamoja na kukimbia, ili kuendeleza vuguvugu la wanamichezo na kuongeza idadi ya watalii wanaozuru nchini.

Aidha, akawahimiza Viongozi wa Wizara hiyo kuendelea kusimamia vyema vyama vya michezo yote ili viweze kutekeleza ipasavyo Katiba na Kanuni za vyama vyao. Rais Dk. Mwinyi ambee alikuwa miongoni mwa washiriki wa mbio hizo za kilomita tano (km5) alItumia fursa hiyo kuwahimiza wafanyabiashara na Wawekezaji kujitokeza kudhamini timu na Vilabu vya michezo , kwa kigezo kuwa hatua hiyo itaamsha ari na hamasa ya wanamichezo na mashabiki, na hivyo kuondokana na utamaduni uliozoweleka wa kushabikia  timu za mataifa mengine.

Alisema suala la Udhamini lina mchango mkubwa katika kutangaza na kukuza biashara na majina ya Kampuni ziliopo hapa nchini.

Akigusia sera ya michezo ya Zanzibar ya mwaka 2018, Dk Mwinyi alisema sera hiyo inaelekeza ushirikishwaji wa taasisi mbali mbali za serikali na Binafsi katika kuendeleza michezo , hivyo akatowa wito kwa jamii kushiriki michezo kutokana na umuhimu kuwa inajenga afya, kuleta furaha, umoja na mshikamano pamoja na kuendeleza amani na utulivu uliopo. Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa moja ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Nane  ni kukuza Uchumi wa Buluu, hivyo akabainisha Utalii wa Michezo kuwa moja katika vipaumbele vyake.

“Ni ukweli usiopingika kuwa mbio za Kimataifa  zina faida kubwa kwa Taifa letu, ikiwemo kuitambulisha nchi yetu, kujenga urafiki, kupata wawekezaji, kujipima kwa wakimbiaji wa kitaifa na kimataifa, kukuza utalii, kutengeneza ajira pamoja na kupunguza maradhi yasioambukiza”, alisema.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwashukuru washiriki wote wa mbio hizo kutoka ndani na nje ya Zanzibar, Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mashirikiano mazuri na vyama vyengine , sambamba na kuwapongeza wadhamini wote kwa kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo.

Mapema, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid , alisema kufanyika kwa mashindano ya Kimataifa ya Marathon  (Zanzibar International Marathon 2021) ni moja kati ya mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM  2020-2025 pamoja utekelezaji wa ahadi za Rais wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Alisema Wizara hiyo ina azma ya kuhakikisha Ligi Kuu ya Soka ya Zanzibar inaimarika ili iweze kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alivishukuru vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kusimamia ulinzi na kuhakikisha mashindnao hayo yanafanyika kwa amani na usalama,huku akibainisha kuwa hiyo ni Marathon ya kwanza kufanywa na Wazawa.

Aidha, Rais wa Chama cha Riadha Zanzibar, alitumia fursa hiyo kumuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa mlezi wa chama cha Riadha Zanzibar. Sambamba na hayo Mjumbe Kamati ya Habari katika Maandalizi ya mashindano hayo  Ali Saleh ‘Alberto’ pamoja na kuiomba Serikali kuyaingiza katika Kalenda, alitoa shukurani kwa wafadhali wote  waliojitokeza kusaidia maandalizi yake. 

Mashindano ya Kimataifa ya  Marathon (ZIM 2021) yaliokuwa katika masafa ya Kilomita 21, km10, km 05  na mbio za nyongeza za mita 400 pamoja na  mbio za watoto na watu wenye ulemavu, yaliwashirikisha wanariadha wapatao 2000 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Ufaransa na Switzerland na wenyeji Zanzibar. Katika mashindano hayo ya kilomita 21 mshindi wa kiume alikuwa ni Panel Mkumbo na yule wa Kike alikuwa ni Pamela Chepkoech wote kutoka Kenya.

Makampuni na watu mbali mbali walijitokeza kudhamini mashindano hayo, ikiwemo  PBZ, NMB, Dar Fresh, Raza Lee, VODACOM, Red TV, Justfit, Afya, Azam TV, Early childhood, Isaraya, Catalunya, ZMMI,World Sport, Park Hyatt, ZSSF, JOMA, nakadhalika.

No comments:

Post a Comment