TANZANIA YASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA TAASISI ZA UMOJA WA AFRIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 12 February 2025

TANZANIA YASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA TAASISI ZA UMOJA WA AFRIKA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akishiriki Kikao cha 46 cha Baraza ya Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 12 na 13 Februari, 2025.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa taasisi za Umoja wa Afrika kuongeza kiwango cha utekelezaji wa shughuli walizojipangia kwa mwaka ili kufikia malengo ya pamoja na kuleta ustawi kwa wananchi barani Afrika.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) katika Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kinachofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia tarehe 12 hadi 13 Februari, 2025 alipokuwa akichangia taarifa ya Kikao cha 49 cha Kamati ya Mabalozi/Wawakilishi wa Kudumu (PRC) katika Umoja wa Afrika.

Balozi Kombo ameipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya na kutoa msisitizo zaidi katika maeneo kadhaa ikiwemo; Matumizi mazuri ya rasilimali ya fedha zinazotokana na michango ya nchi wanachama, utoaji wa ajira kwa kuzingatia uwiano wa uwakilishi na ukomo wa nafasi za ajira kwa nchi wanachama pamoja na usimamizi madhubuti wa Mfuko wa Fedha za Operesheni za Amani barani Afrika.

Aidha, Tanzania ikiwa nchi mwenyeji wa Taasisi za umoja wa Afrika imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Miongoni mwa Taasisi hizo ni Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu, Bodi ya Ushauri wa Masuala ya Rushwa na Umoja wa Posta.

Kikao cha Baraza la Mawaziri kilianza kwa hafla ya ufunguzi ambapo Mwenyekiti wa Baraza hilo anayemaliza muda wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania, Mhe. Mohamed Salem Ould Merzoug katika hotuba yake ya ufunguzi amesisitiza ushirikiano kwa lengo la kujenga mtangamano imara na wenye maslahi kwa pande zote, usuluhishi wa migogoro kwa maslahi ya wananchi na umuhimu wa mageuzi ya kimfumo ndani ya Umoja huo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anayemaliza muda wake Mhe. Mahamat Moussa Faki amelishukuru Baraza la Mawaziri kwa ushirikiano aliokuwa akiupata katika utekelezaji wa majukumu yake na kwamba ni muhimu kuthamini mshikamano na kuimarisha undugu kati ya nchi wanachama.

Vilevile, ameeleza kuwa bara la Afrika linaendelea kuaminiwa hivyo changamoto zinapojitokeza isiwe sababu ya kupoteza matumaini katika kuyafikia malengo ya kuifikia Afrika yenye ustawi.

Kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Gedion Timotheos aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo jijini Addis Ababa pamoja na kusisitiza umuhimu wa mshikamano, ushirikiano katika kupatikana kwa suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazojitokeza.

No comments:

Post a Comment