WAZIRI NDAKI AAGIZA UCHUNGUZI MNADA WA PUGU JIJINI DAR ES SALAAM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 6 June 2021

WAZIRI NDAKI AAGIZA UCHUNGUZI MNADA WA PUGU JIJINI DAR ES SALAAM

Meneja wa Mnada wa Pugu, Samweli Kerambo (kushoto) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) taarifa za makusanyo ya maduhuli alipofanya ziara mwishoni mwa wiki katika mnada huo uliopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na baadhi ya wajumbe kutoka eneo lilipo Mnada wa Pugu, wajumbe hao walikutana na Waziri huyo mnadani hapo kwa lengo la kumuomba kuwapatia sehemu ya eneo katika Mnada huo.


    Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akikagua kumbukumbu za makusanyo ya maduhuli alipofanya ziara katika Mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam.

    Na Mbaraka Kambona

    WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameagiza kufanyika kwa ukaguzi katika mnada wa pugu hususan kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali baada ya kubaini mapungufu kadhaa katika eneo hilo. 

    Waziri Ndaki alitoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mnada huo uliopo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo pamoja na mambo mengine alibaini kuwa kumbukumbu za ukusanyaji wa mapato katika mnada huo hazina uwiano. 

    Baada ya kufanya ukaguzi katika kumbukumbu za makusanyo na vibali vya mifugo ambavyo vimetolewa kuanzia mwezi wanne mpaka wa tano alibaini kuwa taarifa hizo hazijakaa vizuri na mahesabu hayalingani. 

    “Kumbukumbu zenu hazijakaa vizuri, pesa zilizokusanywa na vibali vilivyotolewa hakuna uwiano, haziendi pamoja jambo ambalo linatia mashaka,” alisema Ndaki 

    Kufuatia mapungufu hayo aliyoyabaini, Waziri Ndaki aliagiza Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara aende akafanye ukaguzi wa kina katika mnada huo ili aweze kuyatambua mapungufu na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote watakaoonekana kusababisha mapungufu hayo. 

    Aidha, aliuelekeza uongozi wa mnada huo kuhakikisha malipo yote yanayofanywa na wateja wao yanafanyika kupitia benki kama ambavyo serikali imeelekeza na sio vinginevyo. 

    “Mnada huu ni mkubwa na serikali inapata mapato kupitia hapa, sitaki taratibu za ukusanyaji wa mapato zilizowekwa mzipindepinde, kile kinachokusanywa chote kiende serikalini, kama kuna mambo mnayafanya ya kukwepesha mapato tutajua mapema tu,” alisisitiza Ndaki. 

    Ndaki alitumia fursa hiyo pia, kuwataka watendaji wa mnada huo kuwa waaminifu kwani mnada huo ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali huku akiwakumbusha kuwa mnada huo ni lango la mifugo yote inayotoka sehemu mbalimbali za nchi na kuingia jijini Dar es Salaam hivyo wanawajibu wa kuhakikisha maduhuli ya Serikali yanakusanywa ipasavyo.


    No comments:

    Post a Comment