VIJANA SINGIDA WATAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA KUENDELEZA MIRADI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 5 June 2021

VIJANA SINGIDA WATAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA KUENDELEZA MIRADI

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahan, akizungumza na vijana wa Kikundi cha Wachapakazi Vijana Group kinacho jishughulisha na ushonaji wa nguo wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika  Halmshauri ya Wilaya Mkalama na Singida ili kujionea shughuli za kiuchumi zinazofanywa na vijana walionufaika na mkopo wa mapato ya ndani ya halmashauri. 


Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahan, akizungumza na vijana wa Kikundi cha Wachapakazi Vijana Group kinacho jishughulisha na ushonaji wa nguo wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika  Halmshauri ya Wilaya Mkalama.


Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahan (katikati), akiwa shambani na  Vijana wa Kikundi cha Masogwenda kilichopo Ilongero wilayani Singida wakati wa ziara hiyo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amewataka vijana mkoani  Singida kuwa wabunifu katika kuendeleza miradi ya kiuchumi.

Ndahani ameyasema hayo juzi alipokuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika  Halmshauri ya Wilaya Mkalama na Singida ili kujionea shughuli za kiuchumi zinazofanywa na vijana walionufaika na mkopo wa mapato ya ndani ya halmashauri. 

" Vijana wengi wanaanzisha miradi ya kiuchumi lakini hawapati mafanikio kulingana na matarajio hivyo kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati," alisema Ndahani.

Ndahani aliwaeleza vijana hao kuwa ubunifu katika biashara ni jambo la msingi katika kukuza biashara au shughuli yoyote ya kiuchumi,hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu pamoja na kujifunza kwa waliofanikiwa.

Alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki kwa mashirika na asasi binafsi ili kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana ikiwemo kuwapatia mafunzo ya stadi za maisha na ujuzi,elimu ya ujasiriamali pamoja na masuala ya afya ya uzazi, hivyo  vijana wanapaswa kuona fursa hii adimu na kuacha kulalamika na kuilaumu Serikali.

Alisema Mkoa wa Singida umejipanga kutekeleza sheria ya utoaji wa mikopo kupitia mapato ya ndani ili kuwapa vijana.

Aidha Ndahani aliwaomba viongozi wa vijana na mtaa kuwatengea maeneo vijana kwa ajili ya kuendeleza miradi yao ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara na viwanda kwa kufanya hivyo viongozi watakuwa wametimiza wajibu wao na kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa la kuvitaka vijiji,mitaa na halmshauri kutenga maeneo  kwa ajili ya shughuli za vijana.

Kwa upande wao vijana wa Mkalama na Wilaya ya Singida wamemshukuru Ndahani kwa kuwa karibu na vijana na kuiomba Serikali kuhimiza utoaji wa mikopo na mafunzo ili mikopo inayokopwa iendane na mahitaji ya vijana.

Afisa Maendeleo Vijana Wilaya ya Singida, Monica Nderike alimuhakikishia Ndahani kuwa ushauri uliotolewa kama halmshauri wataufanyia kazi ikiwemo kuwapatia mkopo wa vifaa badala ya fedha taslimu na kuongeza kasi ya utoaji wa mafunzo ya stadi za maisha na ujuzi.

No comments:

Post a Comment