Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameziagiza Taasisi za TFNC, MUHAS, SUA, TBS kuharakisha uandaaji wa muongozo lishe ili uanze kutumika kuanzia mwezi Julai, 2021.
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Boresha Lishe katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Julai 6, 2021.
“Jambo hili limeingia kwenye programu ya kwanza ya boresha lishe ninaomba Watanzania wote tushukuru, tuunge mkono na hatuna haja ya kuchelewa tena na Muongozo huu utoke kabla ya mpango wa pili haujaanza,” Aliongeza Waziri Mhagama.
Amesema kuwa muongozo huo utaliondoa Taifa kwenye tatizo la udumavu kwa kiasi kikubwa sana kama kila mtu atajuenga tabia ya kunywa uji wa lishe bora.
“Tujenge tabia ya kunywa kikombe cha lishe kila asubuhi, wafanyakazi wanywe, wanafunzi wanywe, uji huu utabadilisha mtazamo na kuboresha afya za watoto, wakubwa na wazee wote kwani wanaitaji kuwa na lishe bora, mimi mwenyewe nitaongoza kampeni ya kunywa uji wa lishe asubuhi,”alisisitiza Waziri Mhagama.
Aidha amesema mradi huo umeweza kuongeza wanawake wanaokula vyakula mchanganyiko ambavyo ni vya asili kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 49.
Pia idadi ya watoto kutoka miezi 6-23 wanaopata vyakula mchanganyiko imeongezeka kutoka asilimia 3 mpaka 35 na kusisitiza kuwa mradi huu umekuwa na faida kubwa sana.
Katika ziara hiyo Waziri Mhagama alikabidhi pampu 75 za umwagiliaji kwa ajili ya visima vifupi vilivojengwa na mradi huo pamoja na mashine za kushonea 40 kwa ajili ya vikundi vya VICOBA pamoja na kutembelea kijiji cha Buigiri ambapo alijionea shughuli za ushonaji, bustani za mboga mboga, maonyesho ya mapishi na vibuyu chirizi.
Kwa upande wake Meneja miradi wa WFP Bi Alessia Decaterina amesema wamefanikisha mradi wa boresha lishe katika wilaya nne za Bahi, Chamwino, Ikungi na Singida Vijijini na mradi huo umekuwa na faida kubwa sana kwa wakazi wa maeneo hayo na kusisitiza kuwe na uendelevu katika kusimamia miradi iyo ili izidi kufaidisha watu wengi zaidi.
Mradi wa Boresha Lishe unaoendeshewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani na kufadhiliwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya ukilenga kuimarisha upatikanaji na matumizi ya chakula chenye lishe kwa wanawake na watoto kupitia ya mabadiliko ya tabia, kuzalisha vyakula mchanganyiko na kusambaza chakula bora katika Wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Wilaya za Ikungi na Singida Vijijini Mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment