Wawaklishi wa wazee wa Mkoa wa Ruvuma wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ibuge Ikulu Ndogo mjini Songea Juni 24, 2021.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameanza kukutana na makundi mbalimbali, kundi la kwanza kupata fursa hiyo ni wazee wa Mji wa Songea ambao wamewawakilisha wazee wa Mkoa wa Ruvuma.
RC Ibuge amezungumza na kusikiliza kero mbalimbali za wazee katika kikao kilichofanyika Ikulu Ndogo mjini Songea kikihusisha wazee wa makundi yote wakiwemo wazee wa Baraza la Makumbusho ya Majimaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Ruvuma.
Kabla ya kufanya majumuisho, Mkuu wa Mkoa alitoa fursa kwa wazee kutoa maoni yao na kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa jumla.
Mzee Ismail Nyingo ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wazee wa Makumbusho ya Majimaji, Mchungaji Adimu Mwezegule wa makanisa ya Pentekoste na Tito Mbilinyi, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma walizungumzia changamoto ya Kituo Kikuu cha mabasi cha Songea kilichopo Kata ya Tanga.
Walisema licha ya kwamba Kituo hicho ni cha kisasa,changamoto kubwa ni abiria wanapofika kutoka nje ya Songea wanapata kero ya mawasiliano ya simu na daladala majira ya usiku hivyo kuingia gharama kubwa ya kukodi taksi hadi mjini Songea.
“Tunaomba kwa usiku mabasi yanapofika stendi ya Tanga kuruhusu kubeba abiria hadi mjini kwa sababu wananchi wanaangaika sana’’, alisema Mchungaji Mwezegule.
Mzee John Nyoni Mwenyekiti wa Baraza Huru la Wazee Manispaa ya Songea alimwomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo Bima ya afya kwa wazee, pensheni na kuomba Sera ya wazee itungiwe Sheria kwa sababu ipo muda mrefu.
Mayasa Mfaume ni Katibu wa Waganga wa Jadi aliomba kutatuliwa changamoto zinazowakabili waganga wa jadi alidai kwamba hivi sasa hakuna mfumo kamili wa kuwatambua waganga wa jadi na kuwapatia vibali.
Sponsioza Katambala amemuomba Mkuu wa Mkoa kukutana na mabaraza ya wazee mara kwa mara ili wazee hao waweze kuibua mambo mengi yanayohusu wazee na wananchi kwa ujumla.
Mzee Gerold Haule amemuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia pembejeo kwa wakulima ambapo amesema Mkoa umekuwa unazalisha kwa wingi mazao ya chakula kwa kutumia mbolea hivyo upatikanaji ukiwa rahisi uzalishaji unaweza kuongezeka zaidi.
Mzee Adolf Kumbukuru amezungumzia changamoto ya uharibifu wa mazingira katika Mto Ruvuma ambao upo kwenye tishio kubwa kukauka kutokana na shughuli za kibinadamu. Ameomba Mto huo kuhifadhiwa ili kuulinda.
Akizungumza baada ya kusikiliza changamoto za wazee, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema wazee ni hazina kubwa ndiyo maana ameamua kuwa kundi la kwanza kuzungumza nao baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa mkoa.
RC Ibuge ameahidi atazifanyia kazi changamoto hizo,ikiwemo stendi ya mabasi ya Tanga ambayo amesema atafuatilia kwa sababu serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni sita kuwekeza na kwamba ataangalia namna bora ya kukabiliana na changamoto za stendi hiyo bila kuathiri stendi.
Amesema changamoto zote atazifuatilia na kuzitolea majibu katika kikao kingine ambacho atapanga tena kukutana na wazee ambapo ametoa rai kwa wazee kuendelea kushirikiana na serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumzia mfumo wa stakabadhi ghalani katika mazao ya ufuta na soya, Mkuu wa Mkoa amesema mahitaji ya soko kupitia mfumo huo ni makubwa hasa nje ya nchi na kwamba changamoto za mfumo huo ni ndogo kwa kuwa mkulima anapata faida kubwa zaidi.
“Kinachofanya maendeleo yasitokee popote ni watu wachache wenye maslahi binafsi ambao wanapotosha,mfumo wa stakabadhi ghalani tangu umeanza kutumika mkoani Ruvuma mwaka 2018, umekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima’’, alisisitiza RC Ibuge.
Mkuu wa Mkoa pia amesisitiza suala la amani kuwa ni moja ya vipaumbele vyake, ambapo amesema anataka kuona katika Mkoa wa Ruvuma, kila mtanzania anakuwa salama na kushiriki ipasavyo bila woga katika uzalishaji mali.
No comments:
Post a Comment