HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2021/2 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 12 June 2021

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2021/2



Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akionesha mkoba wenye Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka 2021/22 yenye thamani ya shilingi trilioni 36.33, jijini Dodoma.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA




HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO 

NA MATUMIZI KWA MWAKA 2021/22














   10 Juni 2021 Dodoma

 







“Kwa upande wa wafanyabiashara, nawahimiza kulipa kodi stahiki kwa Serikali. Si haki wala si uungwana kwa wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi. Kufanya hivyo kutaifanya Serikali yetu ishindwe kutoa huduma muhimu kwa wananchi. Hospitali zetu zitakosa dawa  na kusababisha vifo, Watumishi watakosa mishahara na haki zao Stahiki na wanafunzi watakosa elimu bure ambayo ni zawadi tuliyowapa.”




Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


14 Mei 2021









  1. UTANGULIZI


  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2021/22. Hotuba hii inawasilisha bajeti ya kwanza ya Kipindi cha Kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika Bunge lako Tukufu yanawasilishwa kwa mujibu wa Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 23 (3) cha Sheria ya Bajeti, Sura 439 pamoja na Kifungu cha 124 (4) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020.

  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina Bajeti ya Serikali. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2021 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2021 nayo ni sehemu ya bajeti hii.


  1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu amani, umoja na mshikamano na kutupatia kiongozi mwadilifu, thabiti na imara chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

  1. Mheshimiwa Spika, huu ni Mkutano wa kwanza wa Bunge la Bajeti baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 2020, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipata ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza nchi yetu. Ushindi mkubwa na wa kishindo uliopatikana kwa CCM umedhihirisha siyo tu imani kubwa ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi, bali pia ni matarajio na kiu kubwa waliyonayo ya maendeleo kwa Taifa letu.


  1. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 17 Machi, 2021 Taifa letu lilipata msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Naomba kutoa pole kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge lako Tukufu, Wanafamilia hususan Mama Janeth Magufuli na Watanzania wote kwa msiba huo mzito. Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa uongozi wake shupavu wenye uthubutu na uzalendo wa hali ya juu ulioleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu. Mwenyezi Mungu aipumzishe Roho yake mahali pema peponi. Amina! Aidha, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Watanzania kwa kuondokewa na Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mhandisi Balozi John William Herbert Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu hao mahali pema peponi. Amina!




  1. Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi yetu. Mheshimiwa Spika naomba Niweke Ufunguo, Katika Hotuba yangu popote nitakapo tumia neno “MAMA YETU” Nitakuwa namaanisha  Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Katika muda mfupi wa uongozi wake, MAMA YETU ameonesha dhahiri kuwa ni kiongozi makini, shupavu, mchapa kazi, mwadilifu, msikivu na aliye na dira thabiti ya kuendelea kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa. Aidha, ninampongeza  “MAMA YETU” kwa kupata kura zote za ndio za wajumbe 1,862 wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Wana CCM na watanzania kwa ujumla wana imani kubwa sana kwake katika kukiongoza Chama kwa kuzingatia misingi ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi hasa ukizingatia uzoefu wake wa miaka 20 ya uongozi ndani ya chama. Hongera sana Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Ninawaomba watanzania wote kila mmoja kwa imani yake tuendelee kumuombea Mheshimiwa Rais ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ili Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema, hekima na busara katika kutekeleza majukumu yake na KAZI IENDELEE.


  1. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye Dira na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ya “Kudumisha mazuri ya Awamu zilizopita, Kuyaendeleza mema yaliyopo na Kuleta mengine mapya. Hivyo, makadirio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 yameandaliwa kwa kuzingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo: Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025; Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki 2050; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo; na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeyaridhia. Aidha, Bajeti imezingatia kikamilifu maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akilihutubia Bunge hili tarehe 22 Aprili 2021.


  1. Mheshimiwa Spika, naomba kurejea baadhi ya maeneo yaliyobainishwa katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo yamezingatiwa katika bajeti hii kama ifuatavyo: Kudumisha Tunu za Taifa yaani Amani, Umoja na Mshikamano ambavyo ni msingi mkuu wa maendeleo wa Taifa letu; kuendelea  kutekeleza kikamilifu Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini kwa kufanya marekebisho ya Sera, Sheria na kanuni mbalimbali ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza fursa za ajira; kufanya maboresho ya mfumo wa utozaji na ukusanyaji wa kodi ili kurahisisha ulipaji wa kodi na kuongeza wigo wa walipa kodi; na kuendelea kuimarisha uendeshaji wa mashirika ya umma ili yaweze kujiendesha kwa faida na kutoa gawio na mchango stahiki kwa Serikali.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwasilisha bungeni Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2021/22.

  1. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ni kuongeza tija ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuboresha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji kwa kushirikisha taasisi za fedha, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo pamoja na benki nyingine; kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, uongezaji wa thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko; kukuza sekta ya viwanda hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na vyenye kuajiri watu wengi; kuendelea kuziba mianya ya utoroshaji wa madini na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji na uchakataji wa madini nchini ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa; kuimarisha miundombinu ya usafiri, usafirishaji na nishati ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja, reli, usafiri wa majini na angani, upanuzi wa bandari pamoja na uzalishaji na usafirishaji wa umeme; kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji; na kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa.







  1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2020/21


Mwenendo wa Mapato

  1. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2020/21, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 34.88 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Hadi Aprili, 2021 shilingi trilioni 24.53 zimekusanywa sawa na asilimia 86.1 ya lengo la kipindi hicho. Mchanganuo ni kama ifuatavyo:

  1. Mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalifikia shilingi trilioni 14.54, sawa na asilimia  86.9;

  2. Mapato yasiyo ya Kodi yalifikia shilingi trilioni 1.80, sawa na asilimia 78.5 ya lengo; 

  3. Mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 607.4 sawa na asilimia 88.5 ya lengo;

  4. Misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa ilikuwa shilingi trilioni 1.89 sawa na asilimia 70.4 ya lengo;

  5. Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipa dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 3.99, sawa na asilimia 95.7 ya lengo; na

  6. Mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ilifikia shilingi trilioni 1.68 sawa na asilimia 88.1 ya lengo.


  1. Mheshimiwa Spika, mlipuko wa UVIKO-19 umesababisha kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani hususan kwa sekta za utalii, usafiri wa anga na uingizaji wa bidhaa kutoka nje. Aidha, baadhi ya mashirika na taasisi zimeathiriwa na UVIKO-19 na hivyo kupungua kwa michango na gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Mathalani, mapato ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania yameathiriwa kufuatia kuporomoka kwa shughuli za utalii kulikosababishwa na kusambaa kwa UVIKO-19 katika nchi zinazoleta watalii wengi nchini.


  1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha lengo la mapato ya ndani linafikiwa, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kama ilivyoainishwa ndani ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Kufanya Biashara Nchini (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji sahihi wa sheria, kanuni na taratibu za kodi; kuboresha mifumo ya TEHAMA ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS). Vilevile, Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa taasisi za Serikali pamoja na kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani.


  1. Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa hadi Aprili 2021 ni shilingi trilion 1.89 ikilinganishwa na shilingi trilion 1.82 mwaka 2019/20. Pamoja na athari za mlipuko wa UVIKO -19, misaada na mikopo nafuu iliongezeka kwa asilimia 3.84 ikilinganishwa na kiasi kilichopokelewa katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo ili kuwezesha upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu katika kuchangia bajeti ya Serikali.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya Taasisi za Fedha za Kimataifa ili kuhakikisha kiasi kilichopangwa kukopwa kinapatikana. Vilevile, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wawekezaji kwenye soko la ndani la fedha ili kuhakikisha kiasi kilichopangwa kukopwa kinapatikana kwa wakati.


Mwenendo wa Matumizi

  1. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi kwa mwaka 2020/21 yalikuwa shilingi trilioni 34.88 ambapo shilingi trilioni 22.10 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.78 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, jumla ya shilingi trilioni 24.74 zimetolewa sawa na asilimia 86.8 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.42 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 6.09 kwa ajili ya mishahara, shilingi trilioni 4.49 Matumizi Mengineyo na shilingi trilioni 6.84 kugharamia deni la Serikali.


  1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2021, jumla ya shilingi trilioni 7.32 sawa na asilimia 74.1 ya lengo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 6.24 ni fedha za ndani sawa na asilimia 79.7 ya lengo na shilingi trilioni 1.08 ni fedha za nje sawa na asilimia 52.8 ya lengo. 


  1. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, Serikali iliendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa kwenye bajeti kama ifuatavyo:  

  1. Ulipaji wa deni la Serikali kwa wakati shilingi trilioni 6.84;

  2. Ulipaji wa mishahara ya watumishi kwa wakati shilingi trilioni 6.09;

  3. Miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere; na mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) shilingi trilioni 1.02;

  4. Ujenzi na ukarabati wa Reli ikiwemo ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa shilingi trilioni 1.49;

  5. Ujenzi wa barabara, madaraja, na viwanja vya ndege shilingi trilioni 1.15;

  6. Ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa ya Watumishi, Wazabuni na Watoa Huduma, Wakandarasi na Washauri Elekezi shilingi bilioni 965.1;

  7. Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, elimumsingi bila ada, uimarishaji wa vyuo vya VETA, kukuza ujuzi kwa vijana na ujenzi wa miundombinu ya elimu shilingi bilioni 406.6; 

  8. Ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya shilingi bilioni 265.8; na

  9. Miradi ya maji mijini na vijijini shilingi bilioni 207.5.


Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Serikali

  1. Mheshimiwa Spika, Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Serikali ilifanyika Novemba, 2020 kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Tathmini hiyo ilionesha kuwa viashiria vya deni la Serikali viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika Tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa: uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 17.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; na uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 113.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240. 


  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa viashiria vinavyopima uwezo wa nchi kulipa deni, matokeo yalibainisha kuwa, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 13.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa mapato yatokanayo na mauzo ya nje ni asilimia 14.0 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 21. Kwa kuzingatia viashiria hivyo, Tanzania ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia miradi ya maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa wakati.


Mwenendo wa Sekta ya Fedha

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021, viwango vya riba za mikopo ya benki kwa ujumla vilipungua na kufikia asilimia 16.58 kutoka wastani wa asilimia 16.91 Aprili 2020. Riba za mikopo za kipindi cha mwaka mmoja zilipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.05 kutoka asilimia 16.37 Aprili 2020. Aidha, riba za amana ziliongezeka na kufikia asilimia 6.95 kutoka asilimia 6.69 Aprili 2020. Riba za amana za mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia asilimia 8.77 ikilinganishwa na asilimia 8.01 Aprili 2020. Hali hii inafanya tofauti kati ya riba za mkopo na amana kwa mwaka mmoja (interest rate spread) kupungua na kufikia asilimia 7.28 kutoka asilimia 8.36 Aprili 2020. Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya benki ili kuongeza kasi ya kushuka kwa viwango vya riba za mikopo.


  1. Mheshimiwa Spika, sekta ya benki imeendelea kuimarika ambapo uwiano wa mali inayoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu (Liquid Assets to Demand Liabilities) ulikuwa ni asilimia 29.63 Machi 2021, ikiwa ni zaidi ya uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Uwiano wa mikopo chechefu umepungua na kufikia asilimia 9.36 Machi 2021 ikilinganishwa na asilimia 10.50 Machi 2020. Aidha, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulifikia asilimia 4.8 Aprili 2021. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi unaenda sanjari na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwenye uchumi na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Athari za UVIKO - 19 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza juhudi za kukabiliana na athari za ugonjwa wa virusi vya korona (UVIKO-19), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliunda Kamati Maalum ya Wataalamu kuchambua athari za ugonjwa huo na kushauri namna bora zaidi ya kukabiliana nao. Kamati ilikamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa tarehe 17 Mei 2021 ambapo, pamoja na mambo mengine, Kamati ilibaini kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imeathirika kiuchumi na kijamii kutokana na UVIKO-19 hasa katika sekta muhimu zikiwemo afya, utalii, biashara, usafirishaji, sanaa na burudani, ambazo zimesababisha kushuka kwa mapato yatokanayo na mauzo ya huduma nje, akiba ya fedha za kigeni na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi. Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha shughuli za uchumi zilizoathirika zinarejea katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa kabla ya mlipuko wa UVIKO-19. 

  2. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 3 Mei 2021, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizungumza na Bi. Kristalina Georgieva - Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa nia ya kuimarisha mahusiano katika masuala ya kiuchumi na kijamii likiwemo suala la mikakati ya kukabiliana na athari za UVIKO-19. Kufuatia mazungumzo hayo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanza majadiliano na IMF ya mkopo wa dharura (Rapid Credit Facility - RCF) wa dola za Marekani milioni 571. Mkopo huu ni wa masharti nafuu kwa ajili ya kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na UVIKO-19.


  1. SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2021/22


Shabaha za Uchumi Jumla

  1. Mheshimiwa Spika, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2021/22, yameandaliwa kwa kuzingatia misingi (assumptions) pamoja na shabaha mahsusi za uchumi jumla.  Malengo na shabaha za uchumi jumla ni kama ifuatavyo:

  1. Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.6 mwaka 2021 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.2 ifikapo mwaka 2023; 

  2. Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3.0 – 5.0 kwa mwaka 2021/22; 

  3. Mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22; 

  4. Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21; 

  5. Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 

  6. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4.0); na

  7. Kuhakikisha kuwa viashiria vya ustawi wa jamii vinaimarika.



Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Serikali itaendelea kuweka vipaumbele zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Masuala muhimu ya kuzingatia ni pamoja na kuimarisha na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuendelea kutekeleza hatua zifuatazo: 

  1. Kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kuweka mazingira rafiki kwa mlipakodi kwa lengo la kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili kupanua wigo wa kodi; 

  2. Kuendelea kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwianisha na kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada kero;

  3. Kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA;

  4. Kuendelea kuboresha Mfumo wa Serikali wa Kieletroniki wa ukusanyaji wa mapato (GePG) na kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinatumia mfumo huo;

  5. Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha kuwa gawio na michango stahiki inawasilishwa kwa wakati;

  6. Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; 

  7. Kuhamisha jukumu la uwekaji vinasaba kwenye mafuta ya petroli kutoka kwa mkandarasi binafsi kwenda Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuhakiki ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini na kudhibiti ukwepaji kodi kutokana na uchakachuaji unaofanywa kwenye mafuta yanayopita hapa nchini; na

  8. Kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa mikakati na miradi ya kuongeza mapato.


  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wa wawekezaji kwenye soko la ndani la fedha na kuorodhesha Hatifungani za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza masuala yaliyoainishwa katika Mwongozo wa Ushirikiano wa  Maendeleo (Development Cooperation Framework - DCF) ili kuwezesha upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu na kukopa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo (Export Credit Agencies -ECA), ambayo masharti yake yana unafuu.


Sera za Matumizi

  1. Mheshimiwa Spika, Sera za Matumizi katika mwaka 2020/21 zitajumuisha yafuatayo:

  1. Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya;

  2. Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa kuendana na vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki;

  3. Kudhibiti uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni;

  4. Kuendeleza nidhamu ya matumizi ya fedha za umma; na

  5. Kuongeza matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani kwenye eneo la usalama wa mifumo (systems security).


  1. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha usimamizi wa fedha za umma kwa taasisi zinazotoza ada, Serikali inaweka utaratibu mpya na endelevu wa kusimamia mapato na matumizi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala wa Meli Tanzania (TASAC). Hivyo, kuanzia mwaka 2021/22, mapato yataendelea kukusanywa na taasisi hizo kupitia mfumo wa GePG na kuingizwa kwenye akaunti za makusanyo (holding account) zilizopo Benki Kuu. Aidha, taasisi hizi zitapatiwa fedha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na fedha kutolewa kwenye akaunti ya makusanyo baada ya kupata ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali. Vilevile, Serikali itafanya ufuatiliaji wa matumizi ya taasisi hizi kila robo mwaka. 


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia utaratibu wa utoaji fedha kwa Taasisi za Uhifadhi (TANAPA, NCAA, TAWA) ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake. Katika kutekeleza azma hii Serikali itatoa fedha za matumizi mengineyo kwa miezi miwili unapoanza mwaka wa fedha na kuendelea kutoa kwa mwezi mmoja mmoja kila mwezi. Hatua hii itaziwezesha taasisi hizi kuwa na akiba ya fedha za kukidhi mahitaji ya mwezi unaofuata kwa kipindi chote cha mwaka.

Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 ni ya kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Bajeti hii itajielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa katika  maeneo matano (5) ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22. Maeneo hayo ni: Kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu. 


  1. Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uchumi shindani na shirikishi, Serikali itajielekeza katika kugharamia miradi ambayo itajikita katika: Kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kusimamia utulivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara za kufungua fursa za kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kupunguza msongamano mijini na barabara za vijijini, madaraja, usafiri wa majini na angani, mageuzi ya TEHAMA pamoja na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali, nishati, bandari na viwanja vya ndege. Eneo hili limetengewa jumla ya shilingi trilioni 7.44 ikijumuisha shilingi trilioni 3.13 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo. 


  1. Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya kielelezo itakayotekelezwa ni: Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Makaa ya Mawe - Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Ruhudji MW 358; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Rumakali MW 222; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu za Daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; na kuendeleza Kanda Maalumu za Kiuchumi.


  1. Mheshimiwa Spika, katika eneo la kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, msukumo utawekwa kwenye miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Katika eneo hili, kipaumbele ni pamoja na: Kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi wa mazao ya kilimo; kuimarisha vituo vya utafiti na huduma za ugani; kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi; kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi; kuboresha huduma za uhimilishaji mifugo; na kujenga machinjio ya kisasa na minada ya mifugo.


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka mkazo kwenye ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini. Aidha, Bajeti hii itajielekeza katika kugharamia miradi na programu inayolenga kuboresha huduma za utalii, fedha na bima pamoja na kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa dawa muhimu na vifaa tiba. Jumla ya shilingi trilioni 1.38 zimetengwa kugharamia utekelezaji wa miradi katika eneo hili.


  1. Mheshimiwa Spika, katika eneo la kukuza uwekezaji na biashara, Serikali itagharamia programu zitakazoimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa katika kukuza biashara. Masoko yanayolengwa ni yale yatakayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, ikiwemo bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu. Vilevile, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint). Eneo hili limetengewa jumla ya shilingi bilioni 31.6.

  2. Mheshimiwa Spika, ili kuchochea maendeleo ya watu, miradi itakayotekelezwa italenga kuboresha maisha ya watu kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu na mafunzo kwa ujumla, afya na ustawi wa jamii, huduma za maji na usafi wa mazingira na kinga ya jamii ikijumuisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF. Aidha, Serikali itaendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini, kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kuendelea na utekelezaji wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Jumla ya shilingi trilioni 4.43 zimetengwa. 


  1. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuendeleza rasilimali watu, Serikali itagharamia programu inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu katika ngazi zote za elimu ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujiajiri. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali zilizopo nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jumla ya shilingi bilioni 50.5 zimetengwa.



  1. Mheshimiwa Spika, hotuba yangu niliyowasilisha leo asubuhi ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 imeainisha kwa kina maeneo ya kipaumbele ambayo Serikali itayatekeleza kupitia Bajeti ya mwaka 2021/22.


  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi ya kielelezo, Serikali itatekeleza miradi mingine ya uboreshaji wa miundombinu ambayo itagharamiwa na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Miradi hiyo ni Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) wa kukabiliana na mafuriko kwenye Bonde la Mto Msimbazi utakaogharimu dola za Marekani milioni 120. Mradi huu utahusisha ujenzi wa daraja katika eneo la Jangwani, na upanuzi na ujenzi wa kingo za mto Msimbazi. Mradi wa pili unahusisha uboreshaji wa barabara za kukuza fursa shirikishi za kijamii na kiuchumi ambapo Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 300 na mchango wa Serikali ni dola za Marekani milioni 50. Mradi huu unalenga kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yenye tija kubwa ya uzalishaji wa mazao ya kilimo. 


  1. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeanza mazungumzo na Benki ya Dunia kupitia dirisha la International Development Association (IDA) kwa ajili ya mradi wa uboreshaji miundombinu katika Majiji na Miji 45. Utekelezaji wa mradi huu utaanza katika mzunguko wa 20 (IDA 20) unaotegemewa kuanza Julai 2022 na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 500. Mradi utahusisha ujenzi wa miundombinu ya msingi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi wa miji husika.

Maeneo Mengine Muhimu


Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022 

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajiandaa kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351. Kama mojawapo ya maandalizi ya utekelezaji wa Sensa ya Mwaka 2022 Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa upande wa Tanzania Bara na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar imekamilisha kuandaa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka, 2022. Kitabu hiki kinaainisha namna ya usimamizi na utekelezaji wa zoezi zima la Sensa, gharama ya kufanya Sensa pamoja na muundo wa Sensa utakavyokuwa katika ngazi zote za kiutawala.



  1.  Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi bilioni 328.2 zinatarajiwa kutumika kugharamia sensa ya mwaka 2022. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Sensa nchini, Sensa ya Mwaka 2022 itatumia teknolojia ya vishikwambi (tablets) katika utengaji wa maeneo ya kijiografia na ukusanyaji wa takwimu uwandani. Matumizi ya teknolojia hii yana manufaa makubwa, hasa katika kupunguza gharama na muda wa kukusanya na kuchakata takwimu, hali inayowezesha kutoa matokeo ya Sensa ndani ya muda mfupi.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni jukumu la kila mtu, natoa wito kwa kamati zote za Sensa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote, Waheshimiwa Wabunge  pamoja na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha katika maandalizi ya Sensa na wajitokeze wote siku ya kuhesabu watu. Lengo ni kuhakikisha Watu waliolala nchini usiku wa kuamkia siku ya Sensa (usiku wa sensa) wanahesabiwa na kuchukuliwa taarifa zao za kiuchumi, kijamii, mazingira na makazi wanayoishi na mengine mengi kwa ajili ya kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi. 


Maslahi ya Wafanyakazi

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wa umma na wa sekta binafsi katika kukuza Pato la Taifa. Kwa kutambua hilo, Serikali itachukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya wafanyakazi kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8. Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, ambapo kiwango hicho kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015/16 hadi asilimia 8 itakayoanza kutekezwa mwaka 2021/22;

  2. Kufuta tozo ya asilimia 6 iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu (Value Retention Fee) kwa wanufaika; na

  3. Kutenga jumla ya shilingi bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619.


Maslahi ya Madiwani, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata

  1. Mheshimiwa Spika, Madiwani wenzetu wanafanya kazi nzuri sana za kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu. Hawa ni wabunge wakaazi wa kwenye kata zetu ambao kila siku wako na wananchi wetu kwenye kusimamia shughuli za maendeleo. Hata hivyo, katika baadhi ya halmashauri madiwani wamekuwa wakikopwa posho zao, na wengine hufikia  hatua ya kupiga  magoti kwa wakurugenzi watendaji ili walipwe. Hali hii imekuwa ikipunguza ufanisi katika halmshauri zetu kwa madiwani wengi kufanya maamuzi yanayopendekezwa na wakurugenzi watendaji hata kama hayana maslahi kwa Taifa ili waweze kulipwa posho zao. Jambo hili limeongelewa kwa hisia kali sana na Waheshimiwa Wabunge hapa bungeni. Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani, napenda niwaeleze kuwa MAMA YETU amesikia kilio chenu na  alinielekeza mimi pamoja na Waziri wa TAMISEMI kulitafutia ufumbuzi suala hili. 


  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza  kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho za kila mwezi za Waheshimiwa Madiwani moja kwa moja tena kwenye akaunti zao kwa Halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato. Halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato (Daraja A) zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za Madiwani kupitia kwenye akaunti zao. 


  1. Mheshimiwa Spika, Maafisa Tarafa ni viunganishi muhimu wa ngazi za kata na Wilaya zetu ambapo wengi wao hufanya kazi nzuri sana ya kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika maeneo yao. Kwa kutambua umuhimu wao, Serikali ya CCM iliwapatia pikipiki viongozi hawa ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Hata hivyo, wengi wao wanashindwa kugharamia ununuzi wa mafuta na matengenezo ya vitendea kazi hivi na kulazimika kuwachangisha wananchi na hata wengine kuomba msaada kwa wadau mbalimbali. Hali hii inapunguza sana ufanisi katika Tarafa zetu. Kupitia hotuba hii, napenda niwajulishe Maafisa Tarafa wote nchini kuwa MAMA YETU amesikia kilio chenu. Hivyo, napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu  ianze kulipa posho ya shilingi 100,000/= kwa mwezi kwa kila Afisa Tarafa ili waweze kumudu gharama za mafuta na matengenezo ya pikipiki. 


  1. Mheshimiwa Spika, Watendaji Kata ndio wasimamizi wa kazi za sekta zote na ni watendaji wakuu kwenye kata. Wengi wao wanafanya kazi katika mazingira magumu ili kufanikisha shughuli za maendeleo katika kata zetu ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato na masuala ya usalama. Idadi kubwa ya watendaji hawa hutumia mishahara yao kufanya kazi mbalimbali ikiwemo ufutiliaji wa mapato ya Serikali kwa kukodi pikipiki ili kufanikisha shughuli zilizopo. Kwa ujumla  wanafanya kazi nzuri sana ya kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu. Jambo hili limeongelewa kwa hisia kali sana na Mheshimiwa Rose Busiga, Mbunge wa Viti Maalum (Geita), ambaye ni mtendaji wa kata mstaafu na kuungwa mkono na wabunge wengi hapa bungeni. Waheshimiwa wabunge, MAMA YETU amesikia kilio hiki na kutuelekeza kulitafutia ufumbuzi suala hili. Hivyo, napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali kuanza kulipa posho ya shilingi 100,000/= kwa mwezi kwa kila Mtendaji Kata kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.  


Madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

  1. Mheshimiwa Spika, wastaafu wetu walilitumikia Taifa hili kwa uzalendo, uadilifu na bidii kubwa sana. Hatuwezi kuhesabu mafanikio ya nchi yetu bila kutaja mchango wa wazee hawa. Kumekuwepo na changamoto za muda mrefu za ulipaji wa mafao yao kutokana na ufanisi mdogo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika kuhudumia wastaafu wetu. Hali hiyo kwenye mifuko yetu imechangiwa, pamoja na mambo mengine, na uwepo wa madeni ambayo mifuko inaidai Serikali na hivyo kusababisha wastaafu wetu kukosa au kusubiri kwa muda mrefu ili kulipwa mafao yao. Jambo hili pia limejadiliwa kwa hisia kali na Waheshimiwa Wabunge hapa bungeni. Wazee wetu hawa hupata shida sana, ambapo baadhi yao hufadhiliwa malazi kwa kulala misikitini na makanisani na wengine hutegemea wahisani kuhudumia familia zao kinyume na mchango walioutoa katika ujenzi wa nchi hii. MAMA YETU amesikia kilio cha wazee hawa na kutuelekeza Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kukamilisha zoezi la kitaalamu ili kujua hali halisi ya madeni na namna bora ya kulipa madeni hayo.


  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kulipa madeni yanayodaiwa na mifuko kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalum isiyo taslimu (Non-cash Special Bond) zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25. Utaratibu wa hatifungani una faida mbalimbali zikiwemo: kuipa Serikali nafasi ya kibajeti ya kuendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo; kuiwezesha Serikali kuyatambua madeni hayo kwenye kanzidata ya madeni; na kuzuia madeni hayo kuendelea kuongezeka kulingana na tathmini ya thamani ya madai (actuarial valuation). Aidha, utaratibu huo utaboresha mizania ya hesabu na mtiririko wa mapato yanayotokana na riba ya hatifungani hizo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hatua hii inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la wazee wetu kudai haki yao kwa damu na machozi yaliyodumu kwa muda mrefu. 


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea malalamiko kuhusu kucheleweshwa kwa michango ya watumishi kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na baadhi ya ofisi za Serikali kutopeleka kabisa michango hiyo. Jambo hili limekuwa likisababisha usumbufu kwa watumishi punde wanapostaafu. Hivyo, napendekeza kulipa michango hiyo moja kwa moja kutokea Hazina kwa taasisi zote ambazo watumishi wanalipwa na Hazina. Taasisi ambazo zinalipa watumishi kutokana na vyanzo vyao vya mapato zitaendelea kupeleka michango ya watumishi wao kwa ufuatiliaji wa karibu wa Serikali. Serikali itafanya uhakiki na kulipa madeni ya michango ambayo haijawasilishwa kwenye mifuko hadi sasa. 


Jeshi la Polisi

  1. Mheshimiwa Spika, katika jeshi la polisi kwa askari wapiganaji, kuna utaratibu wa wapiganaji kufanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi kwa miaka 12 kabla hawajapata ajira za kudumu. Jambo hili huwasababishia wapatapo mkataba wa kudumu wawe wamechelewa kwa miaka 12 ikilinganishwa na mtumishi mwingine aliyeingia pamoja kazini katika idara nyingine. Jambo hili linamadhara hasi katika itifaki ya utumishi na mafao ya mpiganaji anapostaafu. Hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha askari wa Jeshi la Polisi. Kutokana na changamoto hiyo, MAMA YETU amesikia kilio cha askari hao na alituelekeza tukae na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kutafuta suluhisho la jambo hili. Napendekeza kuanzia mwaka 2021/22 askari wa Jeshi la Polisi wataingia mkataba wa kipindi cha miaka 6 na kuingia katika ajira ya kudumu. 


Kurahisisha Kasi ya Utekelezaji wa Miradi

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi na ufanisi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango itafanya mabadiliko katika Kanuni ya 21 ya Sheria ya Bajeti, SURA 439 ili kuondoa changamoto iliyopo ya fedha ambazo hazijatumika hadi tarehe 30 Juni kila mwaka kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Mabadiliko hayo yatatoa fursa kwa Maafisa Masuuli kuwasilisha taarifa  ya fedha kuvuka mwaka hadi tarehe 30 Juni kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali badala ya siku 15 kabla ya mwaka wa fedha kumalizika. Fedha hizo zitawekwa kwenye Akaunti ya Amana kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli ambazo hazijakamilika wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha husika. Kwa msingi huo, kuanzia sasa hakutakuwa na fedha zenye miadi zitakazorejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka wa fedha isipokuwa pale ambapo Maafisa Masuuli wamekiuka masharti ya Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348.


Kodi ya Majengo 

  1. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi ya majengo, hali iliyosababisha Serikali kubadili njia za ukusanyaji mara kwa mara. Kabla ya mwaka 2017/18, Serikali za Mitaa zilikuwa na jukumu la kukusanya mapato hayo lakini hazikufanya vizuri. Kuanzia mwaka 2017/18, Serikali ilitumia Mamlaka ya Mapato kukusanya kodi hiyo, ambapo pia haikufanya vizuri. Ukusanyaji wa kodi hii kwa kutumia Serikali za Mitaa au TRA umekuwa ukitumia njia za kizamani ambazo zinahusisha watu kusafiri, kupanga foleni na kukusanya fedha taslimu (cash). Utaratibu huu unatumia gharama kubwa, muda na ni hatarishi kwa mapato. Katika kuhakikisha kodi hii inafikia malengo, Serikali imeandaa utaratibu mzuri wa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya majengo. 

Tozo ya Wajasiliamali

  1. Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara na watoa huduma wadogo nchini wameendelea kutambulika kupitia vitambulisho vya wajasiriamali. Tangu kuanza kwa zoezi la utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara na watoa huduma wadogo nchini, jumla ya vitambulisho 2,335,711 vimegawiwa ambavyo vimewezesha kukusanya jumla ya shilingi bilioni 46.71. Lengo ni kuendelea kuwatambua wafanyabiashara wadogo na kuwawekea mazingira rafiki ya ufanyaji biashara. Katika mwaka 2020/21, Serikali imefanya maboresho ya vitambulisho hivyo kwa kuweka picha na jina la mjasiriamali ili kuongeza udhibiti na kufungua fursa kwa wajasiriamali kuweza kutumia vitambulisho hivyo kupata huduma za kibenki na bima ya afya. Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea na uratibu wa kugawa vitambulisho hivi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndiyo yenye mfumo wa kusajili wafanyabiashara hao, kuchapisha vitambulisho na kuwapatia Halmashauri husika kwa ajili ya kugawa.


  1. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI

  1. Mheshimiwa Spika, napenda sasa kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na kurekebisha taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kurejesha ukuaji wa uchumi katika hali ya kawaida baada ya athari zilizotokana na UVIKO-19 sambamba na kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika ili kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje. Vile vile, marekebisho yanalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo na viwanda, kuongeza kipato kwa waajiriwa na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (BluePrint) kwa kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza na kurahisisha ulipaji wake au kuzifuta baadhi ya tozo na ada hizi. Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu Sheria zifuatazo:

  1. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;

  2. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;

  3. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147; 

  4. Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;

  5. Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;

  6. Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290;

  7. Sheria ya Kodi ya Majengo, SURA 289;

  8. Sheria ya Ardhi, SURA 113;

  9. Sheria ya Ushuru wa Stempu, SURA 189;

  10. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82;

  11. Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, SURA 41;

  12. Sheria ya Ukaguzi wa Umma, SURA 418; 

  13. Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134

  14. Sheria ya Usajili wa Magari, SURA 124;

  15. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168;

  16. Sheria ya Raia wa Kigeni (Uratibu wa Ajira) Na. 1 ya mwaka 2015;

  17. Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa Wakala, Mamlaka za Udhibiti na Idara zinazojitegemea;

  18. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;

  19. Kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali; 

  20. Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220;

  21. Sheria ya Petroli, SURA 392; na

  22. Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, SURA 306.


  1. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148

  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo:

  1. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyumba vya ubaridi (cold rooms) vinavyotambuliwa kwa H.S Code 9406.10.10 na 9406.9010. Lengo la msamaha huu ni kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mbogamboga na maua nchini ili kuchochea kilimo cha kisasa;

  2. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madini (precious metals) na makinikia yatakayoingizwa nchini kwa ajili ya kuchenjuliwa, kuongezewa thamani na kuuzwa kwenye masoko ya madini yanayotambulika nchini. Lengo la pendekezo hili ni kuviwezesha viwanda vya uchenjuaji vilivyoanzishwa nchini kupata malighafi ya kutosha kwa ajili ya uchakataji na hatimaye kuongeza ajira na mapato ya Serikali;

  3. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za bima ya mifugo. Lengo la marekebisho haya ni kuchochea shughuli za ufugaji nchini;

  4. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa na huduma zitakazoingizwa au kununuliwa hapa nchini kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mafuta ghafi (EACOP). Lengo la marekebisho haya ni kutoa unafuu wa kodi katika utekelezaji wa miradi tajwa;  

  5. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta ghafi yanayotambulika kwa H.S Code 2709.00.00 kwa lengo la kutoa unafuu kwa mlaji ikiwemo Kampuni ya uendeshaji wa bomba la mafuta (EACOP);

  6. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye Nyasi Bandia zinazotambulika kwa HS Code 5703.30.00 na 5703.20.00 kwa ajili ya Viwanja vya Mpira vilivyoko kwenye Majiji. Msamaha huo utahusisha ridhaa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuendeleza michezo na kukuza vipaji nchini;

  7. Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kadi za kutengeneza vitambulisho vya taifa zinazotambulika kwa H.S Code 3921.11.90.00 na malighafi nyingine za kutengeneza kadi hizo zinazotambulika kwa H.S Code 3921.11.90.00 zitakazoingizwa nchini na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Lengo la pendekezo hili ni kupunguza gharama za kutengeneza Vitambulisho vya Taifa na kuharakisha upatikanaji wake;

  8. Kumekwepo na ukiritimba katika kupokea fedha za misaada kwenye  miradi ya maendeleo kwa hitaji la kisheria la kusubiri idhini ya Baraza la Mawaziri likae ili kuidhinisha  misamaha. Napendekeza Kutoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Taasisi zisizo za kiserikali (NGO’s), kwenye bidhaa na huduma zitakazotumika kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi husika. Aidha, taasisi zitakazonufaika na msamaha huo ni zile ambazo zina mikataba na Serikali yenye kipengele kinachotoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani;

  9. Sekta ya mawasiliano imekuwa ikikua vizuri na kuwa kiungo muhimu cha kuongeza wigo wa wananchi ambao wako kwenye ulimwengu wa kidijitali na kwenye sekta ya fedha (Financial Inclusion). Napendekeza  kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye simu janja za mkononi (smart phones) HS Code 8517.12.00, vishikwambi (Tablets) HS Code 8471.30.00 au 8517.12.00 na modemu (modems) HS Code 8517.62.00 au 8517.69.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano ili kufikia lengo la asilimia 80 ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 iliyopo sasa;

  10. Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mikebe inayotumika kuhifadhia maziwa inayotambuliwa kwa H.S Code 7310.29.20 ambayo kwa sasa haitumiki kwa ajili ya kazi hiyo na badala yake napendekeza kutoa msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mikebe ya kubebea maziwa inayotambulika kwa H.S Code 7310.29.90, 7310.10.00 na 7612.90.90. Lengo la Pendekezo hili ni kuwapunguzia gharama wazalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya maziwa nchini;

  11. Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taa zinazotumia umeme wa jua zinazotambulika kwa H.S. Code 85.13 na 94.05. Lengo la pendekezo hili ni kuwianisha msamaha huu sambamba na msamaha unaotolewa chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ambayo inasamehe Kodi kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha nishati ya umeme wa jua pekee na kurahisisha usimamizi wake. Aidha, pendekezo hili linalenga kuweka usawa katika ulipaji kodi kwa watumiaji wa taa zinazotumia nishati za aina zote; 

  12. Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye huduma ya usafirishaji na huduma zinazohusiana na usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia bomba linalojengwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Uganda (EACOP). Lengo la pendekezo hili ni kuwezesha huduma tajwa kutekelezwa bila kodi sanjari na uzoefu wa kimataifa kwa bidhaa zilizopita hapa kwenda nchi jirani au ng’ambo; 

  13. Kuzitambua bidhaa za mtaji zilizomo kwenye Sura ya 84, 85 na 90 ya Kitabu cha Ushuru wa Pamoja wa Forodha wa Afrika Mashariki kuwa bidhaa za mtaji zitakazostahili kupata kivutio cha ahirisho la malipo ya VAT. Lengo la pendekezo hili ni kuwianisha maana ya bidhaa za mtaji kwenye Sheria za kodi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwenye kifungu tajwa;

  14. Kubadilisha utaratibu wa kutoa msamaha kwenye miradi ya Serikali inayogharamiwa na fedha za serikali na fedha za wafadhili ambapo mnufaika wa msamaha huo atawasilisha maombi kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania badala ya utaratibu wa kuwasilisha kwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya kupata ridhaa na kutoa Tangazo la Serikali (GN) kwa kila mradi. Utaratibu huu utarahisisha na kuharakisha utoaji wa misamaha badala ya utaratibu wa sasa kutokana na TRA kuwa na ofisi kwa kila mkoa nchini kote ambazo zinaweza kupokea, kuchambua na kusimamia matumizi sahihi ya misamaha; na

  15. Kuhusu Zanzibar, Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kurudisha utaratibu wa kurejesha VAT kwa bidhaa zinazonunuliwa Tanzania Bara na kutumika Tanzania Zanzibar. Hii inatokana na mfumo wa kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa bidhaa za viwandani pekee kutowanufaisha wafanyabiashara wa Zanzibar wanaonunua bidhaa na kutozwa VAT Tanzania Bara na kutozwa tena VAT bidhaa hizo zinapopelekwa Zanzibar. Aidha, inapendekezwa marejesho ya VAT yatakayofanyika kwa bidhaa zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar yafanyike pia kwa bidhaa zitakazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara sambamba na marekebisho ya vifungu husika vya Sheria za VAT kwa pande zote mbili za muungano. Ili kuwa na ufanisi wa marejesho, maboresho ya mifumo yatafanyika ili isomane baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kutokana na utaratibu huu, kiwango cha asilimia sifuri ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kilichokuwa kinatozwa bidhaa hizo kitasitishwa.


Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 55,499.97.


  1. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332

  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya   Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza Kodi ya Mapato yanayohusiana na ajira kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8 kama ilivyobainishwa katika Jedwali Na. 1A na 1B


Hatua hii inachukuliwa ikiwa ni dhamira ya Serikali ya muda mrefu kuwapunguzia mzigo wa Kodi wafanyakazi. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato kwa shilingi milioni 14,178.06;

  1. Kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwenye hatifungani za Serikali. Sheria ya Kodi ya Mapato ilisamehe Kodi ya Mapato kwenye hatifungani kwa mwaka 2002/03 pekee. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha soko la ndani la hatifungani linaendelea kusaidia kugharamia miradi ya Serikali;

  2. Kumekuwepo na ukiritimba katika kupokea fedha za kutoka kwa nchi wahisani zinazokwenda kutekeleza Miradi ya maendeleo. Napendekeza Kurejesha utaratibu wa Mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya Fedha kutoa msamaha kwa kutoa tangazo la Serikali (GN) bila sharti la kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za wafadhili kupitia mikataba iliyoingiwa  baina ya nchi hizo na Serikali yenye kifungu kinachoruhusu msamaha wa kodi ya mapato. Lengo la marekebisho haya ni kuharakisha utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa kwa misaada na mikopo yenye gharama nafuu ambayo utekelezaji wake umekuwa ukichelewa kusubiri ridhaa ya Baraza la Mawaziri;

  3. Kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia mbili (2) kwenye malipo yanayohusisha mauzo ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanapouzwa kwenye kampuni na mashirika yote yanayojihusisha na usindikaji na ununuzi wa mazao.  Kwa sasa, Taasisi za Serikali pekee kama vile (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ndizo zinakata kodi hiyo kwa kiwango cha asilimia mbili (2). Aidha, pendekezo hili halitahusisha wakulima wadogo na wale wanaouza mazao yao kwenye masoko ya msingi (AMCOS) na kwenye magulio. Lengo la pendekezo hili ni kuweka usawa katika utozaji wa kodi kwa Kampuni zote zinazojishughulisha na mazao ya Kilimo, mifugo na uvuvi. Pendekezo hili linatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 43,954.2;

  4. Kufanya maboresho ya Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuwezesha ukokotoaji wa gharama za uchakavu kwa kiwango maalum cha asimilia tano (5) kwenye gharama za mali za ujenzi wa bomba la mafuta (EACOP). Lengo la pendekezo hili ni kuwianisha gharama za uchakavu na muda wa matumizi wa bomba husika kwa kuzingatia masharti ya mkataba uliosainiwa baina ya Serikali za Uganda na Tanzania;

  5. Kuweka utaratibu maalum wa utozaji kodi kwa wachimbaji wadogo wa madini wenye mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni 100 kwa mwaka kama ifuatavyo: -

  1. Kutoza kodi wachimbaji wadogo wa madini kwa kiwango mfuto cha asilimia tatu (3) kwenye thamani ya mauzo ya madini pindi yanapopatikana;

  2. Kuweka muda wa ulipaji kodi kuwa ni wakati wanapouza madini na kulipa mrabaha kwenye Tume ya Madini au maeneo maalum yaliyoanzishwa chini ya sheria ya madini;

  3. Kuweka wajibu kwa mchimbaji mdogo wa madini kama mwajiri wa kukata kodi ya mapato ya ajira kutoka kwa wafanyakazi wake pale tu madini yatakapokuwa yamepatikana na kuuzwa katika masoko ya madini;

  4. Kuweka muda maalum wa kulipa kodi ya zuio ya ajira kuwa ni wakati mchimbaji mdogo anapouza madini na kulipa mrabaha katika masoko ya madini au vituo vingine vya uuzaji na ununuzi wa madini vinayotambuliwa na Tume ya Madini; na

  5. Kuweka kiwango cha kodi cha mapato ya ajira (PAYE) cha asilimia 0.6 ya thamani ya mauzo ya madini ambayo italipwa na mwajiri (mchimbaji mdogo wa madini) kwa niaba ya wafanyakazi wake.


Lengo la mapendekezo haya ni kurahisisha utozaji na ulipaji wa kodi kutoka kwa wachimbaji wadogo wa sekta ya madini ili kuongeza mchango wa kodi ya mapato kutoka kwenye sekta hiyo. Hatua hizi kwa pamoja zinatarajia kuongeza mapato ya Serikali shillingi milioni 29,776.14


  1. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa,  SURA 147

  1. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kifungu cha 124(2) cha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuvihuisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, kutokana na biashara za bidhaa hizi kuzorota kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19, napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli isipokuwa vinywaji vikali na bia zitakazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini


  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zifuatazo:

  1. Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kwenye bia zinazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 765 kwa lita za sasa hadi shilingi 620 kwa lita. Lengo la mapendekezo haya ni kuchochea kilimo cha shayiri hapa nchini;

  2. Kuanza kutoza Ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nyuzi na kamba za plastiki (synthetic fibres) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi au kuzalishwa hapa nchini zinazotambuliwa kwa heading 55.11 na 56.07 isipokuwa zile zinazotumika kwenye Uvuvi (HS Code 5607.50.00). Lengo la marekebisho haya ni kulinda mazingira na kuchochea uzalishaji na matumizi ya bidhaa za katani. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 2,644; na

  3. Kuanzisha tozo ya ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye pikipiki zilizotumika kwa zaidi ya miaka 3 zinazoingizwa nchini zinazotambuliwa kwa HS Code 8711. Lengo la marekebisho haya ni kudhibiti uingizaji wa pikipiki chakavu na kulinda mazingira. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ya mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 263.7.

Hatua za kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,907.7.


  1. Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004

  1. Mheshimiwa Spika, Kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (EAC Pre-Budget Consultative Meeting of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 7 Mei 2021 mjini Arusha, kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha (EAC-Common External Tariff) na Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2021/22. Mapendekezo hayo yanalenga katika Kuboresha Maisha ya Watu Kupitia Maendeleo ya Viwanda na Kutengeneza Ajira kwa ajili ya Ustawi wa Pamoja wa Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


  1. Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Mawaziri wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2020/21. Hatua hizo ni kama zifuatazo:

  1. Mapendekezo ya hatua mpya za Viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria yanayotambulika kwa HS Codes 8702.10.99 na 8702.20.99 yanayoingizwa nchini kwa ajili ya mradi wa mwendokasi. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa mabasi hayo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi;

  2. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyuzi za pamba (cotton yarn) zinazotambulika kwa Headings 52.05, 52.06 na 52.07. Lengo la hatua ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo na kuongeza thamani ya zao la pamba (value addition) nchini;

  3. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye matairi mapya ya pikipiki (new pneumatic tyres of rubber) yanayotambulika kwa HS Code 4011.40.00. Lengo la hatua ni kuongea mapato ya Serikali kwa kuwa matairi haya ni bidhaa zilizokamilika kwa ajili ya mtumiaji;

  4. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye siagi ya karanga (peanut butter) inayotambulika kwa HS Code 2008.11.00. Lengo la hatua ni kulinda wazalishaji wa bidhaa hiyo nchini;

  5. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye nyaya (wire of other alloy steel) zinazotambulika kwa HS Codes 7229.20.00 na 7229.90.00. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa wazalishaji wanaotumia bidhaa hiyo kama malighafi;

  6. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye milk cans zinazotambulika kwa HS Codes 7310.10.00 na 7310.29.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwenye sekta ya maziwa nchini;

  7. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye LABSA (Organic surface-active agents – Anionic) inayotambulika kwa HS Code 3402.11.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa sabuni za unga na maji nchini;

  8. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 au 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kuchakata ngozi zinazotambulika kwa HS Code 3208.20.00 na 3210.00.10 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa ngozi nchini;

  9. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 au 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza mbolea zinazotambulika kwa HS Codes 2710.99.00, 2528.00.00 na 3505.20.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbolea nchini;

  10. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya tumbaku iliyochakatwa vinavyotambulika kwa HS Code 5310.10.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa tumbaku nchini;

  11. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya chai iliyochakatwa vinavyotambulika kwa HS Codes 4819.20.90, 5407.44.00 na 3923.29.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa chai (tea blenders) nchini;

  12. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi ya kutengeneza masufuria ya aluminium inayotambulika kwa HS Code 7606.92.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa masufuria hayo nchini;

  13. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwa waunganishaji wa pikipiki za matairi matatu bila kujumuisha fremu kwa kuwa zinatengenezwa hapa nchini (CKD for three-wheel motorcycles excluding chassis and its components) zinazotambulika kwa HS Code 8704.21.90 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waunganishaji wa pikipiki hizo nchini ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo;

  14. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 au 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza mabomba ya plastiki (glass reinforced plastic pipes) zinazotambulika kwa HS Codes 3920.61.10, 7019.39.00, 7019.31.00, 6006.90.00, 7019.12.00, 3920.10.10, 4016.93.00, na 3907.91.00 kwa utaratibu wa duty remission. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa mabomba hayo nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya maji; na

  15. Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye mabati (Flat-rolled products of other alloy steel, of a width of 600mm or more, not further worked than hot-rolled, in coils) yanayotambulika kwa HS Code 7225.30.00. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa wazalishaji wanaotumia bidhaa hiyo kama  malighafi.


  1. Mapendekezo ya kuendelea na utekelezaji wa Viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (UVIKO-19) vikiwemo Barakoa (Masks), kipukusi (sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators), na mavazi maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE). Msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “duty remission”. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo;

  2. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers, Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) machines zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00 na 8470.90.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya vifaa hivi katika kuhasibu mapato ya Serikali;

  3. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juu yanayodumu kwa muda mrefu (UHT Milk) vinavyotambulika kwa HS codes 4819.50.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa maziwa hapa nchini. Utaratibu wa Duty Remission utakaotumika kutoa unafuu huo;

  4. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifuniko vya chupa za mvinyo (corks and stoppers) vinavyotambulika kwa HS Codes 4503.10.00 kwa kuzingatia kuwa havizalishwi hapa nchini. Hatua hii inalenga kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mvinyo ili kuhamasisha na kuendeleza kilimo cha zao la zabibu nchini pamoja na ajira. Utaratibu wa Duty Remission utakaotumika kutoa unafuu huo;

  5. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za marumaru zinazotambulika kwa HS Code 6907.21.00; 6907.22.00; na 6907.23.00 zinazoingizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kulinda na kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru pamoja na kuongeza ajira; 

  6. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye chai inayotambulika kwa HS Code 09.02 inayoagizwa kutoka nje. Lengo la pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha kilimo cha chai hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo;

  7. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye magunia ya kitani (sacks and bags of jute or other textile bast fibers of heading 53.03) yanayotambulika kwa HS Code 6305.10.00 yanayoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyotengeneza magunia ya katani, kukuza na kuendeleza kilimo cha zao la mkonge hapa nchini pamoja na kuongeza ajira na mapato ya Serikali;

  8. Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye unga wa kakao unaoingizwa kutoka nje unaotambulika kwa HS Code 1805.00.00. Lengo ni kuchochea na kuhamasisha kilimo cha zao la kakao nchini pamoja na kuongeza mapato ya Serikali;

  9. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia kahawa vinavyotumiwa na viwanda vya kusaga kahawa nchini. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 7310.21.00; 6305.10.00; 3923.50.10; 3923.50.90 na 3920.30.90. Hatua hii inalenga kuongeza thamani kwenye zao la kahawa na kuvipa unafuu wa gharama viwanda vinavyosaga kahawa hapa nchini. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;

  10. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia korosho. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS code 3923.21.00. Hatua hii inalenga kuongeza thamani kwenye zao la korosho na kuvipa unafuu wa gharama viwanda vinavyochakata korosho hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;

  11. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia pamba. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3920.30.90; 6305.39.00 na 7217.90.00. Hatua hii inalenga kuvutia uwekezaji ili kuongeza thamani ya zao la pamba nchini;

  12. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotumbulika kwa HS code 3506.91.00 Hot Melt Adhesive; PE film HS Code 3920.10.90, Empty bag for Baby Diapers HS Code 6305.33.00, Plastic cask HS Code 3926.90.90; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye Super Absorbent Polymer HS Code 3906.90.00, Wet strength paper HS Code 4803.00.00, Non-woven HS Code 5603.11.00, Polyethylene laminated Nonwovens HS Code 5903.90.00, Spandex HS Code 5402.44.00 na Dust free paper HS Code 4803.00.00. Aidha, msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “Duty Remission”. Hatua hii inatarajiwa kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji na kuongeza ajira; 

  13. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito vinavyotambulika kwa HS Codes 6804.10.00; 7018.90.00; 7020.00.99; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye HS Codes 3606.90.00; 6813.20.00; 8202.20.00; 8202.99.00; 8203.20.00; 8205.10.00; 8423.89.90; 8513.10.90; na 9002.19.00. Hatua hii inalenga kuchochea uongezaji wa thamani kwenye madini. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifaa hivyo; 

  14. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye makaratasi (HS Code 4805.24.00 na 4805.25.00) yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio aina ya maboksi (corrugated boxes). Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika. Lengo la hatua hii ni kuwapa unafuu wazalishaji wa vifungashio hivyo hapa nchini ili wananchi waweze kuvipata kwa bei nafuu;

  15. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotambulika katika HS codes 3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00; 6304.91.90 na 7607.19.90. Utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “duty remission”. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbegu hapa nchini;

  16. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye kahawa inayotambulika kwa Heading 09.01 inayoagizwa kutoka nje ya nchi. Lengo la pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha kilimo cha kahawa hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo;

  17. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products of iron or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.”  Bidhaa hizi hutambulika katika HS Codes 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00; 7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuendelea kutoza viwango hivyo ni kulinda viwanda vya hapa nchini, kukuza ajira pamoja na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje;

  18. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS codes 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00 na 7210.90.00 kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton), kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuwalinda wazalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini kutokana na ushindani wa nje;

  19. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;

  20. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kitakachokuwa  kikubwa. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS Code 7212.30.00; 7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;

  21. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye nondo kwa mwaka mmoja. (Reinforment bars and hallow profile). Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika Hs codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7213.99.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.90.00; 7214.99.00; 7215.10.00; 7215.50.00; 7215.90.00; 7225.90.00; 7225.92.00; 7225.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na 7306.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini na kuongeza ajira;

  22. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga (horticultural products) zinazotambulika kwa HS codes 0603.11.00; 0603.12.00; 0603.13.00; 0603.14.00; 0603.15.00; 0603.19.00; 0604.20.00; 0604.90.00; 0701.90.00; 0702.00.00; 0703.10.00; 0703.20.00; 0703.90.00; 0706.10.00; 0706.90.00; 0710.10.00; 0710.21.00; 0710.22.00; 0710.30.00; 0714.10.00; 0714.20.00; 0804.30.00; 0804.40.00; 0804.50.00; 0805.10.00; 0805.40.00; 0805.50.00; 0806.10.00; 0807.11.00; 0807.20.00; 0808.10.00; 0808.30.00; 0910.11.00 na  0910.12.00.  Lengo la hatua hii ni kulinda wakulima wa ndani ili kuendeleza kilimo cha matunda, mbogamboga na maua hapa nchini; 

  23. Kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles HS Code 3916.10.00; 3916.20.00; 3916.90.00 ambazo hutumika kwa ajili ya kutengenezea fremu za milango, madirisha n.k. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali;

  24. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini ambazo zinazotambulika kwa HS codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00 na 4804.41.00. Lengo la hatua hii ni kuendelea kulinda viwanda vinavyozalisha karatasi hizo hapa nchini;

  25. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 35 kwenye ngano inayotambulika kwa HS Code 1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa utaratibu wa “Duty Remission” ambapo wanaonufaika na unafuu huu ni wenye viwanda vya kusaga ngano. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa Viwanda vinavyozalisha unga wa ngano;

  26. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwa utaratibu wa duty remission kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates” (ABL) HS Code 3920.10.90 ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya dawa ya meno kwenye viwanda vya ndani. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa gharama kwa viwanda vinavyozalisha dawa ya meno nchini;

  27. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 10 kwa utaratibu wa “Duty Remission” kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin (HS Code 1511.90.40) kwa viwanda vinavyotengeneza sabuni nchini. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda vya kuzalisha sabuni nchini;

  28. Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety match boxes) vinavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 25 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha viberiti nchini dhidi ya bidhaa zenye ruzuku kutoka nje na hivyo kuwa na ushindani sawa katika soko;

  29. Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye bidhaa za chuma za misumari zinazotambulika kwa HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins, corrugated nails, and staples other than those of heading 83.05) badala ya asilimia 25 pekee. Hatua hii inalenga kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo nchini.

  30. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo zinazotambulika kwa HS code 1601.00.00. Lengo ni kuendelea kulinda wajasiriamali wa ndani wanaozalisha bidhaa hizo;

  31. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye chingamu (chewing gum HS Code 1704.10.00), biskuti (Heading 19.05) na peremende (HS code 1704.90.00) zinazoagizwa kutoka nje. Lengo ni kuendelea kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hizo na kukuza ajira;

  32. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye chokoleti (chocolates) Heading 18.06 kwa mwaka mmoja. Lengo ni kulinda viwanda vya ndani na kukuza ajira;

  33. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauces) zinazotambulika katika HS code 2103.20.00. Hatua hii inalenga kulinda viwanda vinavyosindika nyanya nchini; 

  34. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye maji ya kunywa (mineral water) yanayotambulika katika HS code 2201.10.00. Hatua hii inalenga kulinda viwanda vinavozalisha maji ya kunywa nchini;

  35. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama zilizoainishwa katika SURA ya 2 katika Viwango vya pamoja vya ushuru wa forodha (meat and edible meat offal of Chapter 2) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuendelea kulinda na kuchochea sekta ya ufugaji nchini;

  36. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya kula yanayotambulika kwa HS codes 1507.10.00, 1580.10.00, 1511.10.00, 1512.11.00, 1513.11.00, 1514.11.00, 1514.91.00, 1515.11.00, 1515.21.00 na 1515.30.00. Hatua hii inalenga kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula nchini, kuongeza ajira mashambani, viwandani pamoja na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi;

  37. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 10 au 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na mwisho (semi-refined and refined) yanayotambulika kwa HS codes 1507.90.00, 1508.90.00, 1509.90.00, 1510.00.00, 1511.90.10, 1511.90.30, 1511.90.90, 1512.19.00, 1512.29.00, 1513.19.00, 1513.29.00, 1514.19.00, 1514.99.00, 1515.19.00, 1515.20.00, 1515.50.00 na 1515.90.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta ya kula nchini, kuongeza ajira viwandani na mashambani pamoja na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi;

  38. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye Gypsum Powder HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda wazalishaji wa Gypsum Powder nchini;

  39. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha asilimia 100 kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap) la uzalishaji hapa nchini; 

  40. Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje badala ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi kikubwa kwa lengo la kutoa unafuu kwa watumiaji nchini;

  41. Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza viatu vya ngozi na nguo. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ukuaji wa sekta ya nguo na viatu vya ngozi nchini; na

  42. Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa utaratibu wa “Duty Remission kwenye malighafi ya kutengeneza leaf springs za magari inayotambulika kwa HS Code 7228.20.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo nchini.


  1. Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa kuweka thamani ya chini ya bidhaa isiyopaswa kutozwa ushuru wa Forodha kuwa Dola za Marekani 50.

  2. Serikali inapendekeza kuliachia jukumu la uthaminishaji wa vitenge vinavyoingizwa nchini kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili uthaminishaji wa bidhaa hiyo uzingatie Kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2004). Sambamba na hatua hiyo, napendekeza utaratibu wa kuthaminisha vitenge kuwa dola za Marekani kati ya 0.55 hadi dola za Marekani 1 kwa mita ya kitenge cha Polyester na dola za Marekani kati ya 0.60 hadi dola za Marekani 1 kwa mita ya kitenge chenye pamba inapotokea thamani iliyowasilishwa (declared) kuwa chini ya kiwango hicho maalumu kwa kuzingatia taratibu za uthaminishaji wa bidhaa hizo.

  3. Kuondoa sharti la kuweka dhamana ya asilimia 15 ya ziada ya Ushuru wa Forodha inayopaswa kurejeshwa (refundable) kwenye sukari ya matumizi ya viwandani. Lengo la hatua hii ni kuwaongezea wazalishaji ukwasi (liquidity) kwa kutowazuilia mtaji wa uzalishaji (working capital). Hata hivyo, wazalishaji watakaobainika kufanya udanganyifu watarejeshewa sharti hili pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine zilizopo kisheria.


Hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 32,626.38.

  1. Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanyia Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438 kama ifuatavyo: 

  1. Kufuta kifungu cha 92A kwa lengo la kuziwezesha mahakama kukusanya mapato yanayotokana na adhabu na faini zinazolipwa mahakamani badala ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kama ilivyo kwa faini na adhabu kwa makosa mengine ambayo mahakama huyatolea maamuzi na hivyo kurahisisha ukusanywaji wa mapato hayo;

  2. Kufuta kifungu cha 70(2) ili kumpa Mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato kutekeleza matakwa ya Sheria husika na kurahisisha upunguzaji au uondoaji wa riba na adhabu ya madeni iwapo kutakuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo; na

  3. Kufanya marekebisho ya Kanuni Na. 15 ya ukokotoaji wa kodi za kimataifa (Transfer Pricing Regulations) kwa kufuta kifungu kinachoweka adhabu ya asilimia 100 kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya Sheria. Lengo la hatua hii ni kuwaondolea walipakodi adhabu kubwa ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji nchini.


  1. Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:

  1. Kubainisha mazingira ambayo Kampuni iliyolipa tozo ya huduma haitawajibika kulipa tozo ya uzalishaji. Marekebisho hayo yanalenga kutatua mgongano uliojitokeza kwenye kutafsiri kifungu husika; na

  2. Kupunguza ada za matangazo kama ifuatavyo:

  1. Mabango yanayowaka kutoka shilingi 18,000 hadi shilingi 13,000;

  2. Mabango yasiyowaka kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 10,000;

  3. Matangazo ya ukutani kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 10,000;

  4. Matangazo ya kielectroniki kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 10,000;

  5. Matangazo kwenye magari kutoka shilingi 15,000 hadi shillingi 10,000 kwa watangazaji wanaotangaza bidhaa za watu wengine;

  6. Matangazo ya muda mfupi/promosheni kwa siku kutoka shilingi 55,000 hadi shilingi 50,000; na

  7. Kila mabango 100 ya promosheni ya kwanza au sehemu ya fungu la mabango 100 ya kwanza kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 50,000.


Ada zote hizi zinatozwa kwa futi za mraba. Kushushwa kwa ada hizi kutapunguza gharama za kutangaza biashara nchini na hatimaye kukuza ushindani kwenye biashara.

 

  1. Sheria ya Kodi ya Majengo, SURA 289;

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya kodi ya majengo, SURA 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za LUKU. Kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, na kwa kuwa Sheria ya Kodi ya Majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo, napendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha shilingi 1,000/= kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU). Aidha, napendekeza kiwango cha shilingi 5,000/= kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU). Serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja.


  1. Sheria ya Ardhi, SURA 113

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi, SURA ya 113 na Kanuni zake za mwaka 2001 kwa kupunguza tozo ya mbele (premium) inayotozwa wakati wa umilikishaji wa ardhi kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza tozo kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 0.5 kwa umiliki mpya wa ardhi; na

  2. Kupunguza tozo kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 kwa urasimishaji. 

Lengo la pendekezo hili ni kuhamasisha wamiliki wa ardhi kukamilisha taratibu za kupata hatimiliki na kufanikisha sehemu kubwa ya ardhi kuandikishwa na kupunguza migogoro. Hatua za kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 9,000.


  1. Sheria ya Ushuru wa Stempu, SURA 189

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kuifanyia Marekebisho Sheria ya Ushuru wa Stempu kwa lengo la kuhuisha viwango vilivyopo sambamba na mfumuko wa bei kwa kuwa viwango hivyo ni vya muda mrefu tangu mwaka 2006. Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:

  1. Ushuru wa Stempu kutoka shilingi 500 hadi shilingi 2,000;

  2. Ushuru wa Stempu kwenye Katiba za Makampuni kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000;

  3. Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za Ubia ambazo mtaji wake unazidi shilingi 100,000 lakini hauzidi shilingi 1,000,000 kutoka shilingi 2,000 hadi shilingi 5,000;

  4. Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za Ubia ambazo mtaji wake unazidi shilingi 1,000,000 kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000; na

  5. Ushuru wa Stempu kwenye nyaraka za kumaliza ubia kutoka shilingi 1,000 hadi 10,000.


Hatua za kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Stempu kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,500.89.

 

  1. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi kama ifuatavyo:

  1. Kupandisha kiwango cha chini cha idadi ya waajiriwa wanaostahili kulipiwa kodi kutoka 4 wa sasa hadi 10. Lengo la marekebisho haya ni kuwapunguzia mzigo wa kodi waajiri wenye idadi ndogo ya waajiriwa na kuchochea ukuaji wa uwekezaji wa uwekezaji nchini;

  2. Kufuta tozo ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi kwa hospitali zinazomilikiwa na taasisi za kidini kwa kuwa taasisi hizi zimekuwa zikiisaidia sana Serikali kufikisha huduma za afya hata kwenye maeneo ambayo Serikali haijaweza kupeleka huduma kutokana na ufinyu wa Bajeti. Aidha, taasisi hizi zimekuwa na ushirikiano na Serikali kwa makubaliano maalum kwa baadhi ya maeneo ya kutoa huduma za afya. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa utoaji huduma za afya kwa vituo vya Afya; na 

  3. Kuanzisha utaratibu mahsusi wa ulipaji wa tozo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuwa ni asilimia 0.4 ya thamani ya mauzo ya madini itakayolipwa na mchimbaji mdogo wa madini pindi atakapouza madini hayo kwenye masoko na vituo vya madini vinavyotambulika na Tume ya Taifa ya Madini.


  1. Sheria ya Michezo ya Kubatisha, SURA 41 

  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza   kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Gaming tax on Winnings) kutoka asilimia 20 hadi asilimia 15 kwenye Michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (Sports betting); 

  2. Kuongeza kiwango cha Kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (sports betting) kwa mapato ghafi (Gross Gaming Revenue - GGR) kutoka asilimia 25 ya mauzo ghafi hadi asilimia 30 ya mauzo ghafi. Ongezeko la asilimia 5 litapelekwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini; 

  3. Kutoza kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha inayoendeshwa kwa kompyuta (Virtual Games); na

  4. Kutoza Kodi ya michezo ya kubahatisha kwa asilimia 10 ya mapato ghafi kwenye michezo ya kubahatisha iliyo chini ya majaribio.


Lengo la hatua hizi ni kuleta usawa wa utozaji kodi katika michezo ya kubahatisha. Hatua hizi za marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 14,925.38.



  1. Sheria ya Ukaguzi wa Umma, SURA 418

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma, SURA 418 kama ifuatavyo;

  1. Kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa na uwezo wa kisheria wa kukagua mashirika yaliyoanzishwa chini ya Sheria ya Makampuni ambayo Serikali ina umiliki wa hisa ili kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kukagua mashirika/makampuni hayo. Kwa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anakagua mashirika/makampuni hayo bila kuwa na nguvu za kisheria, hali inayoweza kuleta mgogoro wa kisheria; na

  2. Kumwezesha Waziri mwenye dhamana ya Fedha kuwasilisha Bungeni majibu kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye kikao kinachofuata cha Bunge baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwasilisha taarifa yake badala ya utaratibu wa sasa ambapo taarifa zote huwasilishwa kwa pamoja katika kikao kimoja cha Bunge.

  1. Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili kuruhusu Serikali kudhamini kampuni au taasisi yoyote kukopa kiasi kisichozidi thamani ya Hisa za Serikali ya Tanzania kwenye mradi husika baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri.


  1. Sheria ya Usajili wa Magari, SURA 124

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Magari SURA 124, kwa kupunguza ada ya usajili wa magari kwa namba binafsi kutoka shillingi 10,000,000 hadi shillingi 5,000,000 kila baada ya miaka mitatu. Lengo la hatua hii ni kuwezesha wamiliki wa magari kuchagua namba binafsi ya usajili wa gari kwa gharama nafuu na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kwa kuwa kiwango cha sasa hakina mwitikio mzuri. 


Hatua hizi za marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Magari inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 270.


  1. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA 168

  1. Mheshimiwa Spika, vijana wengi wamejiajiri kwenye sekta ndogo ya kuendesha bajaji na pikipiki zikijulikana kama bodaboda. Hata hivyo, Vijana hawa hupata usumbufu mkubwa wa kulipa faini kutoka kwenye vipato vyao pale panapotokea uvunjaji wa Sheria ya Usalama Barabarani umefanywa na abiria wao. Hali hii imekuwa ikisababisha baadhi yao kushindwa kulipa faini na hivyo kuzitelekeza pikipiki zao kwenye vituo vya polisi. Mheshimiwa Rais alielekeza jeshi la Polisi kujikita kwenye kutoa elimu kuhusu usalama barabarani badala ya kuwekeza kwenye makosa na kugeuza faini kuwa chanzo cha mapato. Hivyo basi, Napendekeza kupunguza adhabu zinazotolewa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani SURA 168 kwa makosa ya Pikipiki na Bajaji kutoka shilingi 30,000 za sasa hadi shilingi 10,000 kwa kosa moja. Lengo la hatua hii ni kuweka adhabu kwa kuzingatia uwezo wa kulipa.  Aidha, adhabu kwa makosa mengine ya vyombo vya moto zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria zinaendelea kubaki kama ilivyo sasa. 


  1. Sheria ya Raia wa Kigeni (Uratibu wa Ajira), Na. 1 ya mwaka 2015

  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Raia wa Kigeni (Uratibu wa Ajira), Na. 1 ya 2015 kama ifuatavyo:

  1. Kuweka adhabu ya kiasi cha shilingi 500,000/= kwa kila mwezi kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kushindwa kuwasilisha ritani za kila mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamishna wa Kazi. Lengo la pendekezo hili ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari;

  2. Kuweka adhabu ya kifungo cha miezi 12 au faini ya shilingi millioni kumi (10) au vyote kwa mwajiri aliyeajiri raia wa kigeni na kushindwa kuwasilisha ritani za mwezi zenye taarifa za raia wa kigeni aliowaajiri ikiwemo taarifa zao za mishahara kwa Kamisha wa kazi. Lengo la pendekezo hili ni kuhimiza uwajibikaji wa hiari.





  1. Marekebisho ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa, Wakala, Mamlaka za Udhibiti na Idara zinazojitegemea


  1. Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa, Wakala, Mamlaka za Udhibiti na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo: 


  1. Wizara ya Kilimo

Kuanzisha Tozo za Umwagiliaji kwa watumiaji wa miundombinu ya umwagiliaji ili kuwezesha miradi hiyo kuwa endelevu na kuwezesha ujenzi wa miundombinu mipya. Viwango vinavyopendekezwa kama ifuatavyo:

  1. Kutoza ada ya shillingi 60,000 kwenye usajili wa vyama vya umwagiliaji; na 

  2. Kutoza ada ya Huduma ya umwagiliaji ya asilimia tano (5) ya mavuno ya msimu kwa eneo la vyama vya umwagiliaji.

  1. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Kufanya marekebisho kwenye Kanuni za Jumuiya ya Kijamii, SURA 337 ili kuhuisha viwango vilivyokuwa vinatumika awali na kuanzisha tozo katika maeneo ambayo hayakuwa yanatozwa. Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:

  1. Kutoza tozo ya shilingi 100,000 ya uharibifu wa cheti cha Jumuiya ya Kijamii unaolazimu kupewa cheti kipya;

  2. Kutoza tozo ya shilingi 50,000 ya kukosea kwa jina kulikosababishwa na mwombaji atakayepaswa kupewa cheti kipya;

  3. Kutoza tozo ya shilingi 50,000 ya kubadili taarifa za anuani ya Posta au makao makuu ya Jumuiya;

  4. Kuongeza ada ya kuwasilisha maombi ya usajili wa Jumuiya ya Kijamii kutoka shilingi 10,000 hadi shilingi 50,000;

  5. Kuongeza ada ya mwaka kwa taasisi za kidini kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 100,000;

  6. Kuongeza ada ya mwaka kwa taasisi zisizo za kidini kutoka shilingi 40,000 hadi shilingi 50,000;

  7. Kuongeza ada ya mwaka kwa jumuiya za dini kutoka nje ya Nchi kutoka Dola za Marekani 30 hadi Dola za Marekani 60;

  8. Kuongeza ada ya mwaka kwa jumuiya zisizo za kidini kutoka nje ya Nchi kutoka Dola za Marekani 30 hadi Dola za Marekani 60;

  9. Kuongeza tozo ya maombi ya kubadili jina la jumuiya kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000;

  10. Kuongeza tozo ya maombi ya marekebisho ya katiba ya jumuiya kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000; 

  11. Kuongeza tozo ya maombi ya nakala kwa ajili ya ushahidi katika vyombo vya utoaji haki kwa jumuiya kutoka shilingi 50,000/= hadi shilingi 100,000;

  12. Kuongeza tozo ya maombi ya nyaraka kwa jumuiya yenyewe kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 50,000;

  13. Kuongeza tozo ya upotevu wa cheti cha jumuiya kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000;

  14. Kuongeza tozo ya upotevu wa cheti cha jumuiya kwa mara ya pili kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 200,000;

  15. Kuongeza ada ya upekuzi kwa jumuiya yenyewe kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000; na

  16. Kuongeza ada ya upekuzi kwa mwombaji mwingine kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 200,000.


  1. Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

Kuanzisha kanuni za ada na tozo za Shirika la Viwango ya mwaka 2021 ambazo zinaanzisha ada na tozo mpya pamoja na kupitia ada na tozo zilizokuwa zinatozwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) hapo awali. Mapendekezo hayo yameainishwa katika Kiambatisho Na. 5.


  1. Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu

Kufanya marekebisho kwenye kanuni za ada na tozo za Hifadhi za Bahari na maeneo Tengefu ya mwaka 2009 ili kupitia ada na tozo mbalimbali zilizoanzishwa kwa ajili ya hifadhi za bahari na maeneo tengefu kama ilivyoambatishwa kwenye Kiambatisho Na. 6.


  1. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya  Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali. 

  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na Matangazo ya Serikali (Government Notices). 

  1. Kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya kufanya Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali 

  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Idara na Taasisi zinazojitegemea ili Kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa janga la homa kali ya mapafu duniani. Hatua hizi ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Marekebisho hayo yatajumuisha: 

  1. Wizara ya Maliasili na Utalii

Kupunguza ada ya leseni ya Biashara ya Utalii (TTBL) kwa Wakala za Safari kutoka Dola za Marekani 2000 hadi Dola za Marekani 500 ili kuhamasisha biashara ya utalii.


  1. Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Kutoza ada ya shilingi 40,000 kwenye kibali cha kupeleka nyama nje ya nchi kwa nyama zote bila kujali aina ya nyama badala ya ada ya shilingi 100 kwa kilo moja ya nyama ya ng’ombe na shilingi 50 kwa kilo moja ya nyama ya mbuzi na kondoo.


  1. Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.

Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, SURA 263 kwa kupunguza kiwango cha mchango kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia 1.0 inayotozwa sasa hadi asilimia 0.6 ya mapato ghafi ya wafanyakazi. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa kutosha kwa biashara zilizopo na uwekezaji mpya utakaofanyika nchini.


  1. Tume ya nguvu za mionzi Tanzania

Kufuta ada ya Utambuzi wa Mionzi ambayo inatozwa kwa kiwango cha asilimia 0.2 ya Malipwani kwenye mizigo ya vyakula inayosafirishwa kwenye nchi ambazo hazina sharti la uhitaji wa cheti cha utambuzi wa mionzi. Lengo la hatua hii ni kupunguza tozo kero na gharama za biashara na hivyo kuchochea mauzo ya bidhaa nje ya nchi sambamba na kupunguza utoroshaji wa mazao hayo kwenda nchi jirani kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi. 


  1. Idara ya Uhamiaji

  1. Kuondoa ada ya kibali cha kuingia nchini (VISA/PASS FEE) kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka nchi ya Msumbiji kwa ajili ya Mpango wa kubadilishana Wanafunzi wa Elimu ya Juu baina ya Tanzania na Msumbiji (TAMOSE). Lengo la pendekezo hili ni kutekeleza matakwa ya makubaliano kati ya nchi hiyo na Tanzania kuondoleana ada hizo ambapo Msumbiji imeshaanza kutekeleza makubaliano hayo; na

  2. Kuhusu Zanzibar, napendekeza kutekeleza utaratibu wa kuruhusu mapato yanayotokana na Kodi na tozo za Muungano kwenye mapato yanayotokana na tozo za VISA ili yaweze kutumika pale yalipokusanywa (Derivation Principle) kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano. Mapendekezo haya yanafanya suala hili liondolewe kwenye orodha ya changamoto za Muuungano. Mapato yatokanayo na tozo za VISA upande wa Zanzibar yaonekane kwenye bajeti upande wa Zanzibar, kuidhinishwa na kutumika Zanzibar.


  1. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji SURA 427 kwa kufuta na kupunguza ada na tozo zifuatazo:

  1. Kufuta tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye kilimo cha mbogamboga na maua;

  2. Kufuta tozo ya Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence) cha Kinga na tahadhari ya moto inayotozwa kwenye Vituo vya Mafuta nchini; 

  3. Kufuta tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye mashamba makubwa na nyumba za makazi yaliyopo ndani ya mashamba hayo yaliyokuwa yakitozwa kati ya shillingi 100,000 hadi 1,000,000;

  4. Kuongeza ukubwa wa eneo lisilopaswa kutozwa tozo ya Ukaguzi wa Kinga na tahadhari ya moto linatumika kwa maonyesho ya biashara kuanzia mita za mraba zisizopungua 2000 hadi mita za mraba 10,000; na

  5. Kuongeza idadi ya wanafunzi wa bweni kwa shule zisizopaswa kutozwa tozo ya Ukaguzi wa Kinga na tahadhari za moto kutoka wanafunzi wasiozidi 100 hadi wanafunzi 200.


  1. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira

Kufanya marekebisho kwenye kanuni ya ada na tozo Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2019 kama ifuatavyo:

  1. Kupunguza ada ya kuharibu dawa zilizoisha muda wa matumizi yake kutoka shilingi 1,000,000 hadi shilingi 100,000; na 

  2. Kupunguza ada ya kila mwaka ya mazingira kutoka shilingi 200,000 hadi shilingi 100,000. 

 

  1. Bodi ya Nyama Tanzania

Kutoza ada ya shilingi 70,000 kwa Cheti cha Kukubaliwa kupeleka nyama nje ya Nchi badala ya kiwango cha asilimia 1 ya malipwani.


  1. Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)

Kupunguza tozo ya ukaguzi wa Umeme kwa kipimo kimoja (electrical inspection, electrical insulation test and general inspection) kutoka shilingi 590,000 hadi 150,000. Tozo hii inatozwa kabla ya kuanza biashara ya mafuta. Pendekezo hili linatarajia kuchochea mazingira wezeshi ya biashara nchini hususan katika maeneo ya vijijini.


  1. Utoaji Leseni za Bima kwa Makampuni

Napendekeza kubadili utaratibu wa sasa wa makampuni ya bima kulazimika kuomba leseni upya kila mwaka na badala yake makampuni yanayofanya vizuri yawe na leseni ya kudumu, na makampuni yalioko kwenye hali ya uangalizi yapewe leseni ya miaka mitatu huku yakiwa kwenye uangalizi na yakiimarika na kufanya vizuri yaingie kwenye leseni za kudumu. Taratibu za ufuatiliaji na malipo ya kila mwaka yaendelee kama ilivyo sasa. Lengo ni kupunguza ukiritimba.


  1. Uboreshaji wa Mazingira ya Ufanyaji Biashara

Sambamba na hatua za kikodi zilizolenga kupunguza gharama ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara, Serikali itakamilisha mfumo wa kimtandao wa kuwa na dirisha moja la upatikanaji wa vibali mbalimbali katika Idara zote zinazohusika na usajili na vibali ili kuwapunguzia wawekezaji mizunguko ya kutembea ofisi zaidi ya moja kuhangaika nenda rudi kutafuta vibali vinavyotolewana ofisi zaidi ya moja. Lengo la hatua hii nikurahisisha mazingira ya kufanya biashara kama ilivyobainishwa kwenye Blueprint.


  1. Maeneo Mahususi


  1. Barabara za Mijini na Vijijini

  1. Mheshimiwa Spika, hali ya barabara vijijini hairidhishi ambapo bado vipo vijiji ambavyo havina barabara kabisa. Barabara nyingi zinazosimamiwa na TARURA zina hali mbaya. Kwa sasa mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA una urefu usiopungua kilomita 108,946.2 ambazo zinaunganisha maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini. Hadi Desemba 2020, mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA wenye kiwango cha lami ulifikia kilometa 2,250.69, sawa na asilimia 2.1 tu, changarawe kilometa 27,809.26 (asilimia 25.6) na udongo  kilometa 78,886.25 (asilimia 72.4). 

  2. Mheshimiwa Spika, hali hii ya barabara ina madhara makubwa sana kwa jamii yetu kwani baadhi ya akina mama wajawazito wanapoteza maisha kwa kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya. Aidha, wapo wengine ambao wanajifungulia njiani kutokana na kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya. Vilevile, wapo baadhi ya wanafunzi wanaosombwa na maji na kufariki kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, hususan katika maeneo ya vijijini. Kadhalika, bado kuna changamoto ya usafirishaji wa mazao na bidhaa kutoka au kwenda barabara kuu katika baadhi ya maeneo. Serikali imeona ipo haja ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato kuongezea katika mgawo wa sasa kupitia Mfuko wa Barabara ili kufanikisha ugharamiaji wa mtandao wa barabara hizo.


  1. Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Mijini na Vijijini

  1. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini bado hairidhishi. Maji hayana mbadala, maji ni uhai, maji ni maisha kwa viumbe hai vyote. Bado vipo vijiji ambavyo havina kisima hata kimoja cha maji safi na salama na badala yake hutumia maji ya mapalio, maji ya madimbwi, maji ya mito wanayochangia na wanyama. Tanzania ina vyanzo vikubwa na vya uhakika vya maji  ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika, Ziwa  Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Rukwa, Ziwa Chala, Mto Kiwira, Ruvu, Rufiji na Ruvuma pamoja na mingine. Aidha, kuna uwezekano wa kutumia  mabwawa makubwa kama ya Kidunda, Ndembela na Farkwa kama yangekamilika lakini  utekelezaji wake haujaanza pamoja na fidia kutolewa na Serikali kutokana na uhaba wa fedha. Ipo miradi mingi katika mikoa ya Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora, Tanga na Simiyu inayotakiwa kutekelezwa katika mwaka 2021/22, lakini haikuwa katika bajeti. Mikoa mingine ambayo sikuitaja hapa iko kwenye bajeti ya Wizara husika.


  1. Mheshimiwa Spika, hali ya ukosefu wa maji safi na salama ina madhara makubwa sana kwa jamii yetu. Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa inampa nafuu mwanamke katika kufanya shughuli zake za kiuchumi, lengo likiwa ni kumtua mama ndoo kichwani na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakumba akina mama na mabinti katika harakati za kutafuta maji. Aidha, kuna baadhi ya wanafunzi wanakosa masomo na kuharibu maisha yao kutokana na uhaba wa maji katika maeneo yao. Hivyo, Serikali imeona ipo haja ya kuongeza fedha za kugharamia miradi ya maji kwa kubuni vyanzo mbadala vya mapato kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji hususan katika maeneo ambayo yana uhaba mkubwa wa maji.


  1. Afya na Bima ya Afya kwa Wote

  1. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya ni sekta muhimu katika ustawi wa jamii yetu na ni moja ya mahitaji muhimu sana katika maisha ya sasa ya mwanadamu. Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana katika sekta hii, ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mabadiliko ya hali za kiafya kwenye kizazi cha leo. Aidha, wananchi katika maeneo mbalimbali wametumia nguvu kubwa katika kutafuta ufumbuzi wa masuala ya upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga maboma karibu na maeneo yao. Majengo yaliojengwa kwa nguvu za wananchi yamekaa kwa muda mrefu, kati ya  miaka mitano (5) hadi 15. Hadi kufikia Juni 2021, kuna  jumla ya maboma 8,004 ya zahanati ambayo yapo katika mikoa mbalimbali nchini na yapo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa.  Vilevile, yapo maboma kwenye ngazi ya vituo vya afya zaidi ya 1,500 ambayo yametumia nguvu ya wananchi na yanahitaji kukamilishwa. Serikali itaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma hayo pamoja na kuajiri wataalamu wa afya na kuimarisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba.


  1. Mheshimiwa Spika, kuna mradi mkubwa wa bima kwa wote (Universal Health Care) unaolenga kuwafikia watanzania wote. Tanzania ina jumla ya kaya milioni 12.827, ambapo asilimia 20 ya kaya hizo inakadiriwa kuwa ni kaya zisizokuwa na uwezo. Katika kufanikisha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya kwa wananchi wote, Serikali itahitaji zaidi ya shilingi bilioni 149 katika mwaka wa kwanza kwa ajili ya kaya zisizo na uwezo. Kiasi hicho cha fedha kitaendelea kuongezwa kila mwaka ili ifikapo mwaka 2034/35, wananchi wote wawe wamefikiwa na bima ya afya. Serikali imeendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo vituo vya kutolea huduma za afya kwa ngazi mbalimbali vimeendelea kujengwa ili bima ya Afya iweze kutumika na kuwanufaisha wananchi wote. 

  1. Elimu

  1. Mheshimiwa Spika, kuhusu sekta ya elimu kuna kazi kubwa bado iko mbele yetu. Bado kuna shule ambazo zina wanafunzi wengi kuliko idadi ya madarasa na zipo zinazogawa mikondo ili wanafunzi wengine wasome asubuhi na wengine wasome mchana. Hali hii inapunguza muda wa wanafunzi kusoma. Zipo shule ambazo kwenye darasa moja wanaweka uzio wa ubao kutenganisha ili chumba kimoja wasome wanafunzi wa madaraja mawili. Aidha, zipo shule ambazo miundombinu yake imechakaa sana kiasi cha kutishia usalama wa watoto na walimu wetu. Yapo pia madarasa yaliyoezekwa kwa nyasi na yana sakafu ya vumbi. Kadhalika, mwaka ujao utakuwa wa kwanza wa kupokea wanafunzi kidato cha kwanza waliodahiliwa darasa la kwanza kwa mpango wa elimumsingi bila ada. Jambo hili lisipoangaliwa mapema litakuja kusababisha wanafunzi kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na kukosa pa kwenda hadi miundombinu ijengwe kwa zimamoto. Kwa hatua ya maendeleo nchi yetu iliyofikia katika sekta mbalimbali, hali hii haipendezi na haitakiwi kuendelea. Kujenga miundombinu ya shule zetu kwa kusubiri irushwe kwenye mitandao ya kijamii ndio tuone inatutia aibu, au kusubiri watoto wakose pa kwenda au wakose pa kukaa ndipo tukimbizane na kufukuzana, ni ishara ya kutopanga vizuri. Hili tusingependa liendelee kuwepo.


  1. Mheshimiwa Spika, kila mwaka kuna wanafunzi kati ya asilimia 15 - 20 wanatoka kwenye mfumo wa elimu kwa kutoendelea na kidato cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kupata ujauzito, utoro na hali ngumu ya maisha. Ukosefu wa mpango wa kugharamia mahitaji ya sekta ya elimu ndiyo chanzo cha tatizo hili.



  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya juu, zaidi ya wanafunzi 11,000 wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu ambao tayari walishapata udahili katika vyuo mbalimbali walikosa mikopo. Naongelea mkopo, sio fedha ya bure, bali ni mkopo ambao ataurejesha. Katika jamii nyingi za kitanzania, mtoto akikosa mkopo huku akiwaona wenzake wanaendelea, inamfadhaisha sana. Ni mfadhaiko kwake na familia nzima. Kwa hatua ya maendeleo ambayo nchi yetu imepata katika sekta mbalimbali hali hii haipendezi na haitakiwi kuendelea. Serikali inakusudia kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa inaongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwanufaisha vijana wote wenye sifa za kupata mkopo.


  1. Miradi ya Kielelezo ya Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la  Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR)

  1. Mheshimiwa Spika, Miradi ya bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) sio tu ni miradi ya kielelezo bali ni miradi “mama” kwa kila mtanzania. Ni miradi inayoashiria uhuru wa nchi yetu, ni miradi inayoashiria kujitegemea kwa nchi yetu, ni miradi inayoashiria heshima ya mtanzania na inajengwa na mtanzania. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais, kutokamilika kwa miradi hii itakuwa laana kwa Taifa letu. Hatutajengewa miradi hii na mtu yeyote, tutawaenzi wabeba maono wa miradi hii kwa kujenga na kuikamilisha. Mwalimu Nyerere alibeba maono ya miradi hii, Rais Magufuli alianzisha miradi hii, Rais Samia anakwenda kuijenga miradi hii. Niwahakikishie watanzania hapatakuwepo GOFU hata la Mradi mmoja wala kusimama kwa mradi unaotekelezwa hata kwa mwezi mmoja. 

  

  1. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na maeneo mahsusi hayo niliyotangulia kuyasema, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria zifuatazo:


  1. Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220

Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta kama ifuatavyo: 

  1. Kuongeza Ushuru wa barabara kwa shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli;

  2. Kufanya marekebisho ya kifungu cha 4 A(a) cha sheria ili kuelekeza fedha zitakazokusanywa kutokana na ongezeko la ushuru wa barabara na mafuta la shilingi 100 kwa aina zote za mafuta ziwe kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini kupitia TARURA. 


Hatua hii ya marekebisho ya Sheria inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 322,158.20. 



  1. Sheria ya Petroli, SURA 392

Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Petroli ili kuongeza tozo ya Mafuta ya Taa kutoka shillingi 150 hadi shillingi 250. Lengo la hatua hii ni kupunguza uchakachuaji wa mafuta kufuatia ongezeko la ushuru wa mafuta kwenye dizeli na petroli. 


  1. Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, SURA 306

Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki kama ifuatavyo:

  1. Kutoza tozo ya shillingi 10 hadi shilingi 10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa. Kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa. Pendekezo hili litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha shillingi milioni 1,254,406.14; na

  2. Kutoza kiasi cha shilingi 10 hadi shilingi 200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji. Pendekezo hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha shillingi milioni 396,306.0.


  1. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa,  SURA 147

Kutokana na vinywaji vikali kuwa na kiwango kikubwa cha kilevi, napendekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia 30 ili kuwa na uwiano wa viwango vya kodi kati ya Vinywaji kali na Bia. Hatua hii inatarajia kuiongezea mapato Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 60,769.35.

Utekelezaji wa hatua hizi nne kwa pamoja unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,033,639.66. 


  1. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.

  1. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kikodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2021, isipokuwa pale itakapoelezwa vinginevyo. Aidha, Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).


  1. Njia Mbadala za Kutekeleza Miradi Mikubwa

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 nchi yetu ilifanikiwa kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati cha chini (Lower Middle-Income Country). Kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kati kunaifanya nchi yetu kutakiwa kujiendesha kiuchumi bila kutegemea kwa kiwango kikubwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ambayo, hupewa nchi zenye kipato cha chini. Hivyo, ni lazima Serikali iboreshe mbinu inazotumia na kubuni mbinu mpya za kupata mapato. Katika kutekeleza hatua hii, Serikali imeanza kufanya uchambuzi wa vyanzo mbadala vya rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vile ufadhili mchanganyiko (Blended Finance). Wafadhili wanaotoa aina hii ya ufadhili hutoa fursa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, kurekebisha au kujumuisha (restructuring or consolidation) deni lake kwa makubaliano ya kutumia sehemu ya malipo ya deni katika uhifadhi wa mazingira au kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii.


  1.  Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2021/22, Serikali inadhamiria kukamilisha mchakato wa Tathmini na Ukadiriaji wa Kukopesheka kwa Nchi (Sovereign Credit Rating). Hatua hii inalenga kutuwezesha kujua nafasi yetu katika masoko ya fedha ya kimataifa na jinsi wakopeshaji wanavyotuona hasa katika uwezo wa kusimamia uchumi na kulipa madeni yetu. Hatua hiyo itatuwezesha pia kuongeza wigo wa wakopeshaji ambao wako tayari kutukopesha, hususan katika Masoko ya Mitaji ya Kimataifa (International Capital Markets). Serikali itaanza mara moja mchakato wa wazi wa kutekeleza na kukamilisha kazi ya Sovereign Credit Rating ndani ya mwaka 2021/22.


  1. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya rasilimali fedha, Serikali itaangalia uwezekano wa kutumia Hati Fungani zitakazotolewa na Halmashauri za Manispaa na Majiji kama njia mbadala ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati. Hatua hii itapunguza mzigo kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali hasa kwa Halmashauri zenye miradi ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa na uhakika wa uwezo wa miradi hii kujiendesha kwa faida (bankable projects). Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (United National Capital Development Fund - UNCDF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (Capital Markets and Securities Authority - CMSA) imeanza mchakato wa kuhakikisha kwamba Halmashauri, Manispaa na Majiji yatakayokidhi vigezo na masharti ya matumizi ya Hati Fungani hizi yanaanza kutumia utaratibu huu.


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kutumia Masoko ya Hati Fungani za Kimataifa maarufu kama “Eurobonds” ikiwa ni chanzo cha kuaminika na thabiti cha kugharamia miradi ya maendeleo kwa kuzingatia Mkakati wa Deni la Muda wa Kati (Medium Term Debt Strategy - MTDS). Hatua hii inakwenda sambamba na hatua nyingine inayopendekezwa katika hotuba hii ya kufungua soko la dhamana za Serikali ili kuruhusu wawekezaji wa nje ya Tanzania na Afrika Mashariki kununua hati fungani zetu ili kuongeza ukwasi katika soko la ndani.


  1. Mheshimiwa Spika, Soko la Eurobond ulimwenguni linakadiriwa kuwa na zaidi ya dola za Marekani trilioni 30 zilizotolewa kwa nchi zinazotafuta rasilimali fedha kwa njia ya mikopo kutoka kwenye masoko ya kimataifa yenye ukwasi mkubwa ili kugharamia miradi ya maendeleo. Njia hii pia hutumiwa na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika wanapotafuta fedha kwa ajili ya kufadhili miradi yao kote duniani. Aidha, nchi mbalimbali za kusini mwa Jangwa la Sahara zinazofanya vizuri kiuchumi zimekuwa zikitumia Soko la eurobond kama chanzo thabiti na chenye masharti rafiki katika kugharamia utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo. Tanzania itahitaji kufanyiwa tathmini ya kukopesheka ili kufikia masoko ya mitaji ya kimataifa kupitia eurobonds. Hivyo, zoezi la kukadiria au kutathmini kukopesheka kwa Tanzania ni hatua isiyoepukika.


  1. Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2010 tulipopitisha Sheria ya PPP hatujapata mafanikio ya kujivunia katika eneo hili pamoja na faida kubwa na nyingi ambazo Taifa linaweza kupata kupitia mfumo wa PPP hasa katika miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi na utaalamu kutoka sekta binafsi. Utekelezaji wa miradi ya PPP hupunguza mzigo kwenye deni la Serikali na hata katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na hutoa nafuu ya kibajeti (Fiscal Space) kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu mengine ambayo hayawezi kugharamiwa na sekta binafsi. Hivyo, ni muhimu kutumia PPP kwenye miradi mbalimbali inayokidhi Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura 103.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia manufaa ya PPP, Serikali itaongeza kasi ya kushughulikia miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi ikiwa ni pamoja na: Ujenzi wa viwanda vya dawa muhimu na vifaa tiba; ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne na Kituo Changamani cha Biashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Aidha, wananchi na wawekezaji wengine wanaalikwa kubainisha maeneo ambayo wanaweza kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya PPP kulingana na uwezo wao wa mitaji na utaalamu.


  1. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2021/22

  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2021/22, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 36.33 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 22.18, sawa na asilimia 13.5 ya Pato la Taifa. Aidha, Serikali inalenga kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 2.99 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 863.9.

  1. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.96, sawa na asilimia 8.1 ya bajeti yote. Kiasi hicho kinajumuisha fedha za miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.67 na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 282.3. Napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo kwa kuendelea kutoa fedha za misaada na mikopo nafuu ili kufanikisha miradi na programu mbalimbali za maendeleo zitakazotekelezwa katika bajeti ya mwaka 2021/22. 


  1. Mheshimiwa Spika, kipekee ningependa kuwatambua Washirika wetu wa Maendeleo kama ifuatavyo: Serikali za Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Korea ya Kusini, Japan,Ufaransa, Ujerumani, Norway, Poland, Ubelgiji, Uholanzi, Uswisi, Uingereza, Sweden na Marekani. Vilevile, kuna Mashirika ya Kimataifa ambayo ni Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi katika Afrika, Mfuko wa Abu Dhabi, Mfuko wa Kuwait, Mfuko wa kimataifa wa kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na malaria, Umoja wa Ulaya, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Umoja wa mataifa na mashirika yote yaliyopo chini yake, Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya Kimataifa, Mfuko wa Mazingira, pamoja na Shirikisho la GAVI. Ninapenda pia kuyatambua Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya ndani na nje pamoja na mashirika ya ufadhili - philanthropies kwa misaada yao kwenye sekta mbalimbali.


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 7.34 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 4.99 ni mikopo ya ndani ambayo inajumuisha shilingi trilioni 3.15 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi trilioni 1.84 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, shilingi trilioni 2.35 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/22, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.33 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 23.0 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 13.33 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.66 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, shilingi trilioni 8.15 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni 4.19 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 200.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.


  1. Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi trilioni 13.33 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani ni shilingi trilioni 10.37 na fedha za nje shilingi trilioni 2.96. Aidha, fedha za maendeleo zinajumuisha, shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya miradi ya reli ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa; shilingi trilioni 2.08 kwa ajili ya miradi ya barabara, ujenzi wa madaraja, na viwanja vya ndege; shilingi trilioni 2.34 kwa ajili ya miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere; shilingi bilioni 589.4 kwa ajili ya miradi ya maji mijini na vijijini; shilingi bilioni 233.3 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi; shilingi bilioni 500 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; shilingi bilioni 215.6 kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022; na shilingi bilioni 312.1 kwa ajili ya elimumsingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 400.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya miradi ya maendeleo. 


  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2021/22 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 2. 











Jedwali Na. 2: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2021/22

  1. HITIMISHO


  1. Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa hotuba hii, napenda kumshukuru kwa dhati “MAMA YETU” kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Ninamuahidi Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa wabunge na Watanzania wote kwamba, nitaibeba dhamana hii kwa uadilifu, weledi na uwezo wangu wote na ninamuomba Mwenyezi Mungu anijalie afya njema, hekima na busara katika kutekeleza majukumu hayo. Naomba nielezee masuala machache muhimu kabla ya kuhitimisha hotuba hii.


  1. Mheshimiwa Spika, kwanza natoa pongezi kwa “MAMA YETU” kwa matumaini makubwa aliyowapa watanzania. “MAMA YETU” ameonesha ni Kiongozi Makini, ni Kiongozi Shupavu, ni Kiongozi Mchapa Kazi, ni Kiongozi Mwadilifu, ni Kiongozi Msikivu, ni Kiongozi aliye na dira thabiti na maono ya kuendelea kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa. Ameweka wazi kuwa hataki kodi ya dhuluma, hataki kuendesha Serikali kwa mapato ya dhuluma, ameweka wazi kusimama imara kwenye masuala ya mapato na matumizi ya Serikali, ameweka wazi kuwa atakuwa imara kwenye vita dhidi ya rushwa.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa kauli hizo “MAMA YETU” ameonesha kuwa, kukaa kwake katika nafasi mbalimbali katika Serikali za awamu mbalimbali SMT na SMZ kumemfanya awe kiongozi aliyeandaliwa na KUIVA na aliye tayari kuiongoza nchi kwa ufanisi mkubwa. Itakumbukwa mbali na nafasi zingine nyingi alizoshika katika miaka yake takribani ishirini Serikalini, MAMA YETU amekuwa Waziri katika Awamu ya Nne na amekuwa Makamu wa Rais katika Awamu ya Tano. “Kuna style za uongozi amejifunza”.


  1. Mheshimiwa Spika “kuna style za uongozi amejifunza” kupitia Awamu hizo alikopewa nafasi kuhudumu katika nafasi mbalimbali. “MAMA YETU” alikuwa Waziri katika awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Mheshimiwa Kikwete alikuwa Mzalendo wa kweli, alikuwa na maono (Visionary Leader), alikuwa mwalimu, alikuwa mzazi, alikuwa mlezi na kiongozi, alikuwa rahim sana, alikuwa mvumilivu sana aliyeamini kwenye Mifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi. Hii naweza kuifananisha kama “Refa kwenye mchezo” wa mpira wa miguu, ambaye anachezesha mechi zake akiwa na “kadi ya njano tu”, kadi nyekundu anaiacha nyumbani. Ukicheza rafu mara ya kwanza anakuonya kwa kukuelekeza, ukicheza rafu mara ya pili anakupa kadi ya njano, ukikosea anakupa kadi ya njano tena na alipotakiwa kutoa kadi nyekundu mara nyingi alionya kwa mdomo, kwa kuwa kadi nyekundu alikuwa anaiacha nyumbani. Rais Kikwete aliamini sana kwenye Mifumo na Utendaji wa Kitaasisi. Kwa mtazamo wangu, jinsi “MAMA YETU” alivyoanza ni dhahiri amepata funzo kwenye awamu hiyo ikiwemo funzo la Uzalendo, maono na kuamini kwenyeMifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi”, na hapa naweza kusema ameichukua “kadi ya njano”, anayo na ameanza kutumia kama mnavyoona.


  1. Mheshimiwa Spika, “MAMA YETU” alikuwa Makamu wa Rais katika awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Rais Magufuli alikuwa mzalendo wa kweli, alikuwa na Maono (Visionary Leader), alijitoa kwa nguvu zote (Dedicated), alikuwa na uthubutu sana, mtu wa vitendo sana na muumini wa matokeo na kuchukua hatua za papo kwa papo. Kama refa wa mchezo wa mpira wa miguu, alikuwa akienda kuchezesha Mechi zake akiwa na “kadi nyekundu tu”,  kadi ya njano alikuwa anaiacha nyumbani. Ukicheza rafu mara ya kwanza tu anakupa kadi nyekundu, wakati mwingine hata asipoiona rafu yeye, mchezaji au shabiki akisema ameona rafu anakupa kadi Nyekundu (no nonsense), hata mimi mwenyewe niliwahi kutembelewa na kadi nyekundu nikakosa michezo kadhaa. Hayati Dkt. Magufuli aliamini kwenye nidhamu ya hali ya juu ya mchezo. “MAMA YETU” alikuwa Line one na Mheshimiwa Majaliwa akiwa Line two. Hivyo, “MAMA YETU” amepata mafunzo kwenye awamu hiyo ya Uzalendo, Uthubutu, mtu wa vitendo kuamini kwenye matokeo na nidhamu kazini na ameichukua “kadi ya nyekundu”.


  1. Mheshimiwa Spika “kuna style za uongozi amejifunza”. “MAMA YETU” anazo kadi zote, “kadi ya njano” na “kadi nyekundu”. MAMA YETU” ni Mzalendo wa kweli, ni Mwadilifu sana, ana Uthubutu, ana Maono, anaamini kwenyeMifumo, Taasisi na Utendaji wa Kitaasisi”, hataki maneno anataka vitendo. Nitoe rai kwa watumishi wote wa umma na watanzania kwa ujumla tuchape kazi kwa bidii, kwa uadilifu na uzalendo mkubwa. Kwa watumishi wa umma tusimamie matumizi ya fedha za walipa kodi kwa uadilifu mkubwa na kwa watanzania tulipe kodi bila shuruti. Tabia moja ya refa asiyependa kuonea upande wowote, huwa hawezi kupendelea upande wowote. Kwenye michezo ya mieleka huwa mnapewa tahadhari ya don’t try this at home, kwenye maslahi ya nchi wanaotaka kumjaribu MAMA YETU nawaonya Don’t try at all”. Tujiepushe na kadi Nyekundu


  1. Mheshimiwa Spika, lazima tujenge utamaduni wa kuheshimu mali na rasilimali hapa nchini (mali za umma na mali binafsi). Kwa upande wa mali za umma, lazima tutangulize uzalendo na uadilifu tunapotekeleza majukumu yetu. Serikali inapoteza fedha nyingi kwenye kutekeleza Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutojali thamani ya fedha kwenye miradi. Watumishi wa Serikali wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kuongeza gharama za miradi ikilinganishwa na gharama halisi ingawa wanafuata taratibu zote za ununuzi. Taratibu za ununuzi zinapokamilika, watumishi na wafanyabiashara hawa hugawana fedha na kiasi kidogo tu kilichosalia ndicho kinaelekezwa kwenye mradi husika na hatimaye kupata mradi ulio chini ya kiwango. Ukiwafuatilia kisheria hupati moja kwa moja pa kuwashika, hivyo wanakuwa wameiba kwa kuzingatia sheria. Nawaelekeza wote wanaohusika na ununuzi wa umma kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na kutanguliza mbele uzalendo na uadilifu. Serikali itachukua hatua za makusudi katika kuimarisha usimamizi wa sheria na taratibu za ununuzi.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mali binafsi, ni lazima tuheshimu biashara zetu na mali zinazotokana na biashara hizo. Kuna hatua tunazozifanya sekta zote za umma na binafsi zinadumaza uchumi wetu. Kwa mfano, kuna tabia ya kutolipa madeni kwenye benki zetu, jambo ambalo linapunguza uwezo wa benki kutoa mikopo kwa watu wengine. Aidha, wapo watu wengine ambao wakidaiwa kwa makusudi ya kuchelewesha malipo wanakimbilia mahakamani. Tusitumie vibaya vyombo vyetu vya sheria. Vilevile, kuna baadhi ya wakopeshaji ambao hawaheshimu mali za wateja wao. Mfano, mteja anakuwa amelipa sehemu kubwa ya mkopo wake lakini ikitokea mkopeshaji, rafiki au dalali akaipenda dhamana iliyowekwa, hufanya njama ya kupiga mnada dhamana hiyo kwa bei isiyolingana na thamani ya dhamana au sehemu ya deni iliyobaki sio hata robo ya dhamana hiyo. Natoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia kila eneo panapokuwa na minada kwenye sekta binafsi na hata sekta ya umma na pale patakapoonekana kuwepo kwa njama za kudhulumu wamiliki wa mali au kuchepusha sehemu ya mali zinazouzwa kwa mnada hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa.


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Kuna wanaodhani tunapoongelea kukusanya kwa weledi, sheria na haki wanachukulia tutaacha kukusanya kodi. Nataka nisisitize kuwa, tutakusanya Mapato ya Serikali. Tutakusanya Mapato ya Serikali. Tutakusanya Mapato ya Serikali. Nitoe rai kwa watumishi wote wa Serikali wanaohusika na kukusanya kodi, maduhuli na ushuru kuelewa vizuri maelekezo haya kwa kuzingatia sheria, weledi na kutenda haki kama Mheshimiwa Rais alivyoelekeza.  Nimeanza kusikia visingizio kila kona, mara mfumo, mara mtandao mara EFD haifanyi kazi. Kwa watoza kodi na walipakodi wote visingizio hivi vitaturudisha kwenye ukaguzi. Tusiwekeze kwenye kusaidiwa kukwepa kodi bali tusaidiwe kwenye kufuata sheria. Akiwepo mtumishi akakusaidia kukwepa kodi nawe ukampa asante unatengeneza tatizo tu sio unafuu kwani kuna siku utakuja kukaguliwa huku aliyekusaidia akiwa amehamishwa au kuachishwa kazi. Nitumie fursa hii kumwelekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato kuweka watu mahususi wa kufanya doria kila kona, nchi nzima kuangalia mwenendo wa matumizi sahihi ya EFD na mifumo mingine ya malipo kuwa muda wote inafanya kazi. 


  1. Mheshimiwa Spika, tutasimamia nidhamu katika matumizi. Tutasimamia nidhamu katika matumizi. Tutasimamia nidhamu katika matumizi na tutaendeleza mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi. Nazijua mbinu zote za udanganyifu, nazijua njia zote za majizi na watakaoendelea na tabia za kudokoadokoa fedha za walipa kodi, nitawashukia kama mwewe. Kazi inaendelea, watanzania endeleeni kumwamini Mheshimiwa Rais wetu, yuko macho na wasaidizi wake tuko macho, tutapambana na MCHWA wote, kuna mengine mnayasikia, kuna mengine mnayaona na mengine hata hamyaoni, yote tunaendelea kuyafanyia kazi kwa maelekezo thabiti na ya kizalendo ya Mheshimiwa Rais wetu. Kinyiramba kuna msemo usemao “MWINDA KANGA HAPIGI YOWE.”

 

  1. Mheshimiwa Spika, tuendeleze kwa kasi na kukamilisha miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira, hususan ajira kwa vijana. Tutakamilisha ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, tutaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) mpaka itakamilika, tutamalizia ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa zilizosalia, tutakamilisha ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi na madaraja mengine kuwaunganisha wananchi wetu, tutaendelea na usambazaji wa umeme kutoka kila kijiji kwenda kila kitongoji na hatimaye kila nyumba.


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Jiji la Dodoma na kulifanya kuwa la kisasa. Shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa ofisi za wizara na taasisi zake katika mji wa Serikali Mtumba; kujenga barabara za mzunguko; na kuboresha miundombinu ya maji. Aidha, Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa katika eneo la Msalato.


  1. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie watanzania kupitia hotuba hii kuwa, tunaendelea kuijenga nchi, tunaendelea kuijenga nchi, ije mvua, lije jua, tunaendelea kuijenga nchi, uwe usiku au mchana, tunaendelea kuijenga nchi. Hakuna mradi hata mmoja utakaokwama, wala hakuna Sekta ya maendeleo itakayozorota. “KAZI INAENDELEA.”


  1. Mheshimiwa Spika, nampongeza Dkt. Philip Isdor Mpango aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, napenda kumpongeza kwa dhati kwa kazi nzuri aliyoifanya katika usimamizi wa uchumi kama Waziri wa Fedha wa Serikali ya Awamu ya Tano ulioiwezesha nchi yetu kuingia katika kundi la nchi za hadhi ya uchumi wa kipato cha kati cha chini. Vilevile, nampongeza kwa kazi nzuri iliyotukuka katika kuisimamia Wizara ya Fedha na Mipango ambayo kwa hakika imeweka msingi mzuri wa utekelezaji wa majukumu yangu.


  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mhe Rais Mwinyi, ameanza kazi vizuri sana na kuwapa matumaini mapya wananchi wa Zanzibar katika kukuza uchumi na maendeleo hasa kwa kuwekeza kwenye “Blue Economy”.


  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa kwa kuteuliwa na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza kwa uongozi wake hodari ndani ya Serikali na hapa Bungeni pamoja na kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025. 


  1. Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze wakuu wa mihimili mingine ya Dola kwa usimamizi na uongozi shupavu, nikianza na wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa kuongoza Bunge hili kwa umahiri na busara. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa uongozi makini wa Mhimili wa Mahakama unaozingatia, miiko,dira na dhima ya mhimili huo. Hakika uongozi wake umefanikisha upatikanaji wa HAKI kwa wanyonge na kujenga misingi imara ya utawala wa sheria hapa nchini.


  1. Mheshimiwa Spika, niruhusu pia kumpongeza Mheshimiwa Balozi Hussein Athman Kattanga kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma. Nampongeza kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini na kwa weledi mkubwa. Vilevile, nawapongeza Mheshimiwa Othman Masoud Othman kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 



  1. Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na Usalama. Kipekee, naomba niwatambue Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Nyakoro Sirro; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Diwani Athuman Msuya; Kamishna Jenerali wa Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, CP Salum Hamdun; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Gerald Kusaya Musabila; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John William Masunga. Utumishi wao uliotukuka na uzalendo wa hali ya juu umetuwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa amani Tunawaomba muendelee kutimiza wajibu wenu wa kulinda amani na usalama wa nchi yetu kwa moyo wa uzalendo.


  1. Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati napenda kuipongeza na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Omar Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kwa umakini wao katika kuchambua na kutoa maoni na ushauri ambao umesaidia kuboresha mapendekezo ya Bajeti hii. Aidha, ninawapongeza Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge za Kisekta kwa michango waliyotoa kupitia vikao vya Kamati za Kisekta iliyowezesha kuboresha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2021/22.


  1. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi na watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku hususan maandalizi ya bajeti hii. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Hamad Y. Masauni, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni. Ninamshukuru sana Katibu Mkuu Hazina na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel M. Tutuba, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Amina Kh. Shaaban, Adolf H. Ndunguru na Dkt. Khatibu M. Kazungu pamoja na watumishi wa kada zote wa Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru Profesa Florens D. Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kusimamia sekta ya fedha kwa weledi mkubwa. 


  1. Mheshimiwa Spika, namshukuru Ndugu Alphayo J. Kidata, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi mkubwa.  Kadhalika, namshukuru CPA Charles E. Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma kwa wakati pamoja na kuishauri Serikali. Ninamshukuru CPA Athumani S. Mbuttuka, Msajili wa Hazina kwa kuendelea kusimamia Mashirika ya Umma na kuhakikisha Serikali inapata mchango na gawio stahiki. Ninamshukuru pia Dkt. Albina Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kusimamia vizuri Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kuendelea na maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.


  1. Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri wote walioaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nyadhifa hizo. Aidha, niwapongeze pia wabunge wenzangu wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuaminiwa na vyama vyao na kuchaguliwa na wananchi ili kuwawakilisha bungeni. Kwa moyo wa dhati napenda kumshukuru mke wangu mpenzi Bi Neema Nchemba, kwa kunitia moyo na kuniombea wakati wote ninapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Vile vile, nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa Jimbo la Iramba Magharibi walioniamini na kunichagua tena kwa kishindo kuwa Mbunge wao. Ninawaahidi kuwa sitawaangusha.


  1. Mheshimiwa Spika, niwashukuru wafanyabiashara na wananchi wote ambao wameendelea kulipa kodi kwa hiari. Rai yangu kwao ni kuwa, tukitumia rasilimali za nchi yetu vizuri na kufanya kazi kwa umoja na bidii, tutaifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi na biashara sio tu kwa ukanda wa Afrika Mashariki bali kwa Afrika nzima. Vile vile, navishukuru vyombo vyote vya habari kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya Taifa letu.


  1. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru viongozi wa dini kwa sala na dua zao zilizotuwezesha kukamilisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa amani na utulivu. Aidha, nawashukuru kwa kuliombea Taifa katika kipindi kigumu tulichopitia cha kuondokewa na viongozi wa kitaifa pamoja na mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya korona. Sala na dua zao zimetuwezesha kupita kwa amani katika kipindi cha mabadiliko ya uongozi wa kitaifa na hatimaye kumpata Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ninawasihi waendelee kuliombea Taifa letu bila kuchoka.


  1. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa lakini si kwa umuhimu napenda nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja hii na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. 


  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


















.













.


























KIAMBATISHO NA. 5

MABORESHO YA TOZO ZA SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA


USAJILI WA CHAKULA NA BIDHAA ZA CHAKULA

S/N

AINA YA HUDUMA

TOZO YA SASA KWA DOLA ZA KIMAREKANI 

TOZO PENDEKEZWA KWA SHILINGI ZA KITANZANIA

1

Usajili wa maziwa na bidhaa za maziwa

450

600,000

2

Usajili wa nafaka na bidhaa za nafaka

400

                                  600,000

3

Usajili wa kunde

350

500,000

4

Usajili wa Karanga

350

500,000

5

Usajili wa bidhaa za mashina na mizizi

360

500,000

6

Usajili wa vinywaji visivyo vya kileo

350

500,000

7

Usajili wa vileo

300

500,000

8

Usajili wa sukari na asali

360

500,000

9

Usajili wa chumvi iliyowekewa iodini

280

500,000

10

Usajili wa mafuta ya kula

280

500,000

11

Usajili wa mahani ya chai na kahawa

450

600,000

12

Usajili wa kakao na bidhaa za kakao

400

600,000

13

Usajili wa viungo mbalimabali vya chakula, chai n.k na mimea

400

600,000

14

Usajili wa siki (vinega)

230

500,000

15

Usajili wa samaki na bidhaa za samaki 

370

600,000

16

Usajili wa nyama na bidhaa za nyama

400

600,000

17

Usajili wa matunda na bidhaa za matunda

330

500,000

18

Usajili wa maji ya kunywa

410

600,000

19

Usajili wa mboga za majani na bidhaa zake

330

500,000

20

Usajili wa chakula cha Watoto wachanga na formula za ukuzaji

900

1,000,000

21

Usajili wa virutubisho vya chakula

800

800,000

22

Usajili wa vyakula vya nafaka vilivyosindikwa kwa ajili ya watoto

850

1,000,000

23

Usajili wa viongezeo vya chakula

250

500,000

24

Usajili wa bidhaa tamutamu kama chocolate, pipi, biskuti, n.k

380

550,000

 



MAELEZO

1.

Tozo zinazopendekezwa zinajumuisha gharama za kutathmini bidhaa, upimaji wa maabara na ukaguzi sokoni kwa muda wa miaka mitano. Tozo hizi zinapendekezwa kupunguzwa ili kuendana na dhamira na muongozo wa serikali wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara

2.

Tozo hizi zinapendekezwa kupungua kwa sababu sehemu ya gharama za ukaguzi na ufuatiliaji wa muenendo wa bidhaa sokoni zimeshughulikiwa katika mifumo mingine jumuishi ndani ya TBS

3.

Tozo zilizopunguzwa zinatarajiwa kuongeza idadi ya wasajiliwa na bidhaa zitakazosajiliwa, hivyo mapato ya Shirika hayataathiriwa.



                                                    TOZO BORESHWA ZA UPIMAJI KATIKA MAABARA



Na.


VIPIMO

TOZO ZA SASA KWA DOLA ZA KIMAREKANI

TOZO ZA VIPIMO PENDEKEZWA KWA SHILINGI ZA KITANZANIA


MAABARA YA KEMIA

1

Hydroquinone kwenye vipodozi

435

150,000/=

2

Kojiki asidi kwenye vipodozi

435

150,000/=


MAABARA YA CHAKULA

3

Kiasi cha unyevu

30

30,000/=

4

Crude fibre

55

30,000/=

5

Acid insoluble ash

55

30,000/=

6

Protini

55

60,000/=

7

Asidi ya foliki

65

50,000/=

8

Madini joto

60

30,000/=

9

Total ash

45

30,000/=

10

Volatile oils

55

30,000/=

11

Sumukuvu  

120

150,000/=

12

Aflatoxins 

225

150,000/=

13

Kiasi cha chumvi 

35

30,000/=

14

Chromate test

25

30,000/=

15

physical tests (kila moja)

5

10,000/=

16

Slip point (Melting point)

25

30,000/=

17

Acid value

50

30,000/=

18

Unsaponifiable matter

50

30,000/=

19

Peroxide value

50

30,000/=

20

Insoluble impurities

25

30,000/=

21

Soap content

20

30,000/=

22

Relative density

10

20,000/=

23

Refractive index

10

20,000/=

24

Saponification value

50

30,000/=

25

Rangi ( ICUMSA)

30

20,000/=

26

Ethyl alcohol (Ethanol) content

25

30,000/=

27

pH

10

15,000/=

28

Carbon dioxide

20

20,000/=

29

Polarisation

25

30,000/=

30

Water insoluble matter

25

30,000/=

31

Sulphated ash

50

30,000/=

32

Acidity

25

30,000/=

33

Brix (Total soluble solids)

15

20,000/=

34

Specific gravity

10

20,000/=

35

Total carbohydrates

30

20,000/=

36

Fat content

60

45,000/=

37

Ascorbic acid

65

30,000/=

38

Water soluble ash

50

30,000/=

39

Alkalinity

25

30,000/=

40

Kiasi cha sukari

50

30,000/=

41

Kafeini

65

50,000/=

42

Alkalinity of water-soluble ash

40

30,000/=

43

Density

10

20,000/=

44

Sorbic acid

55

20,000/=

45

Total solids

30

20,000/=

46

Volatile acidity

25

30,000/=

47

Aldehydes

25

50,000/=

48

Methanol (for Alcoholic Beverages and Spirits)

50

50,000/=

49

Total acidity

25

20,000/=

50

Chloride (as NaCl)

35

30,000/=

51

Free Fatty acids (FFA)

25

30,000/=

52

Higher alcohols (for Alcoholic beverages and Spirits)

45

50,000/=

53

Hydroxymethyl furfural (HMF)

50

50,000/=

54

Dry matter

30

30,000/=

55

Kiasi cha nyama

55

20,000/=

56

Sulphur dioxide

50

30,000/=

57

Total cocoa solids

15

20,000/=

58

Fat free cocoa solids

15

20,000/=

59

Cocoa butter

35

35,000/=

60

Purity

50

30,000/=

61

Vitamini (kila moja)

65

50,000/=

62

Madini tembo (kila moja)

55

35,000/=

63

Mabaki ya viuatilifu

120

300,000/=

64

Mabaki ya dawa (pesticide residues)

135

150,000/=

65

Vikolezo vya utamu 

65

50,000/=

66

Kihifadhi (kila kimoja)

65

50,000/=

67

Rangi za chakula

65

50,000/=

68

Total plate count

130

30,000/=

69

Yeast and Moulds

160

30,000/=

70

Salmonella spp (kila moja)

155

40,000/=

71

Escherichia coli

130

40,000/=

72

Coliforms

125

30,000/=

73

Staphylococcus aureus

150

40,000/=

74

Listeria spp 

150

40,000/=

75

Bacillus spp (kila moja)

165

40,000/=

76

Pseudomonas aeruginosa

125

40,000/=

77

Shigella

155

40,000/=

78

Enterobacteriaceae

130

30,000/=

79

Clostridium spp (kila moja)

165

40,000/=

80

Sulfite reducing anaerobes

125

40,000/=

81

Streptococcus spp (kila moja)


125

40,000/=


MAELEZO

Gharama za vipimo vya kimaabara zinapendekezwa kupunguzwa ili kukidhi matakwa ya “Government Blueprint For Regulatory Reform” yanayolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.










USAJILI WA VIPODOZI


S/N

AINA YA HUDUMA

TOZO YA SASA KWA DOLA ZA KIMAREKANI

TOZO PENDEKEZWA KWA SHILINGI ZA KITANZANIA

1.

Usajili wa vipodozi

100

440,000




MAELEZO



Tozo hii inapendekezwa kuongezwa ili kukidhi gharama za upimaji





TOZO ZA MAABARA YA METROLOGY 

S/N

AINA YA HUDUMA



AINA YA KIFAA

UWEZO AU KIWANGO CHA KUPIMA

TOZO ZA SASA KWA SHILINGI ZA KITANZANIA

TOZO ZA SASA KWA DOLA ZA KIMAREKANI

TOZO PENDEKEZWA KWA SHILINGI ZA KITANZANIA

TOZO PENDEKEZWA KWA DOLA ZA KIMAREKANI

1

TUNGAMO

Mzani mdogo

(0-200) g

      120,000

155

135,000.00

195

Mzani wa uchambuzi

Up to 200 g

          80,000

103

90,000.00

129

Mzani wa uchambuzi

(201-2000) g

      75,000.00 

97

90,000.00

129

Mzani wa dijitali

(2100-6000) g

      70,000.00 

91

90,000.00

129

Mzani usio wa digitali

(0-20) kg

      70,000.00 

91

90,000.00

129



Mzani wa uzito

(10-50) kg

      80,000.00 

103

90,000.00

129

(51-150) kg

      110,000.00 

142

135,000.00

194

(151-250) kg

      150,000.00 

194

220,000.00

285

(251-500) kg

      250,000.00 

323

350,000.00

453


Daraja la kupimia Uzito

(500-5000) kg

  1,000,000.00 

1294

1,400,000.00

1,811

Above 5 Tone to 40 Tone

  1,200,000.00 

1552

1,600,000.00

2,070

Above 50 Tone

  1,700,000.00 

2199

2,200,000.00

2,846

Mzani mkubwa wa kuchanganyia 

(500-2000) kg

      950,000.00 

1229

1,300,000.00

1,682

Mzani wa kuninginiza

-

90,000.00

116

100,000.00

129

Mobile Weighing Crane

(0-20) Tone

1,500,000.00

1940

2,200,000.00

2,846


Mzani wa Kupimia ndege

3781kg (Red pad)

200,000.00

259

350,000.00

453

4143kg

200,000.00

259


350,000.00

453


(Yellow pad)

2039kg

200,000.00

259


350,000.00

453


(Green pad)



Seti ya Mawe ya Tungamo

1mg to 1000 g

25,000.00

32

25,000.00

32

(2000-5000) g

20,000.00

26

20,000.00

26

From 10 kg and above

30,000.00

39

30,000.00

39

2

KANI

Mashine ya kukandamizia

 

      700,000.00 

906

    1,200,000.00 

1,552

CBR (proving) ring

 

      400,000.00 

517

600,000.00

776

Torque Wrench

 

      110,000.00 

142

160,000.00

207

Load Cell

 

      780,000.00 

1009

1,200,000.00

1,552

Rebound Hammer

 

      200,000.00 

259

250,000.00

323

Tensile Machine

 

      260,000.00 

336

350,000.00

453

Marshall machine

 

      400,000.00 

517

600,000.00

776

Torque meter

 

      150,000.00 

194

180,000.00

233

Tension meter

 

      90,000.00 

116

100,000.00

129

3

JOTO RIDI

Vipima  joto:
i).Vipima joto vyenye vimiminika

(0-200)'C

      85,000.00 

110

90,000.00

129

(201-600) t

      95,000.00 

123

99,000.00

142

(-30-200)'C

      85,000.00 

110

90,000.00

129

ii). Vipima joto vya dijtali
a). Mfumo wa kipima joto na kichwa cha kusomea
( Pt.100 probes/RTDs)

(-30-200)'C

      85,000.00 

110

90,000.00

129

(200-600)'C

      95,000.00 

123

99,000.00

142

More than three points

      110,000.00 

142

108,000.00

155

(-30-1200)'C

      110,000.00 

142

117,000.00

168

b) Thermocouple probes

c) Kipima joto aina ya kalamu

iii). Dial Temp. Gauges

(-30-200)'C

      85,000.00 

110

90,000.00

129

(200-600)'C

      85,000.00 

110

90,000.00

129

(-30-600)'C

      110,000.00 

142

108,000.00

155

iv). Kipima joto na unyevunyevu

(-30-200)'C

      110,000.00 

142

108,000.00

155

Dry block

 

      260,000.00 

336

315,000.00

453

Water bath

 

      120,000.00 

155

135,000.00

194

Ugezi wa nukta moja

 

      95,000.00 

123

135,000.00

194

Ugezi wa nukta zisizo zidi tatu

 

      160,000.00 

207

180,000.00

259

Ugezi wa nukta zaidi ya tatu

 

175,000.00

226

225,000.00

323

Autoclave (Ugezi wa nukta moja)


      215,000.00 

226

180,000.00

259

Autoclave (Ugezi wa nukta zisizo zidi tatu)

 

      215,000.00 

278

225,000.00

323

Autoclave (Ugezi wa nukta Zaidi ya tatu)

  

      110,000.00 

278

270,000.00

388

Friji/Friji la kugandisha

 

      120,000.00 

142

117,000.00

168

Ovens (Ugezi wa nukta moja)

 

      120,000.00 

155

135,000.00

194

Tanuri (Ugezi wa nukta zisizozidi tatu)

 

      120,000.00 

155

180,000.00

259

Ovens (Ugezi wa nukta zisizo zidi tatu)

  

      150,000.00 

155

225,000.00

323

  1. MUFFLE FURNANCES

 

      130,000.00 

194

180,000.00

259

  1. Incubators (Ugezi wa nukta moja)

 

      130,000.00 

168

162,000.00

194

Incubators(Ugezi wa nukta zisizo zidi tatu)

  

      130,000.00 

168

145,800.00

259

Incubators(Ugezi wa nukta Zaidi ya tatu)

  

      100,000.00 

168

225,000.00

323

HOT PLATES(Ugezi wa nukta moja))

 

      100,000.00 

129

135,000.00

194

HOT PLATES(Ugezi wa nukta zisizo zidi tatu)

  

      100,000.00 

129

180,000.00

259

HOTPLATES(Ugezi wa nukta Zaidi ya tatu)

  

      165,000.00 

129

180,000.00

259

Vyumba vya kupima Unyevynyevu

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

Vyumba vya Baridi

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

Sahani za Kugandishia

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

Blast freezers

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

Vyumba vya baridi /Chill rooms

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

VIDHIBITI JOTO

 

      165,000.00 

213

180,000.00

259

Thermographs

 

      85,000.00 

110

90,000.00

129


UGEZI PAMOJA NA UCHORAJI (Incubators, Oven, Liquid bath, Refregirators)


Ugezi wa nukta moja


-

-

540,000.00

776

Ugezi wa nukta tatu


-

-

720,000.00

1,035

Ugezi wa nukta Zaidi ya tatu


-

-

900,000.00

1,294

UGEZI PAMOJA NA UCHORAJI (Autoclave)


Ugezi wa nukta moja


-

-

720,000.00

1,035


Ugezi wa nukta tatu


-

-

900,000.00

1,294


Ugezi wa nukta Zaidi ya tatu


-

-

1,080,000.00

1,552




-




4

KEMIA NA VINGINE

Refractometer

 

      90,000.00 

116

108,000.00

155

Mita ya pH 

 

      90,000.00 

116

108,000.00

155

Mashine ya kuchambua Unyevunyevu

 

      90,000.00 

116

108,000.00

155

Hydrometer

 

      90,000.00 

116

108,000.00

155


Mita ya Wiani

 

      100,000.00 

129

108,000.00

155

5

UJAZO


Upimaji wa uwezo wa ujazo

(0-1000)ml

      40,000.00 

52

36,000.00 

52

(1001 to 2000) ml

      50,000.00 

65

      45,000.00 

65

Above 2000 ml

      60,000.00 

78

      54,000.00 

78

Pycnometer

(50-100)ml

      40,000.00 

52

    36,000.00 

52

TOT

 

      30,000.00 

39

      27,000.00 

39


Flaski ya ujazo

(0-50)ml

      40,000.00 

52

      36,000.00 

52

(51-1000) mI

      40,000.00 

52

      36,000.00 

52

(1001-2000)ml

      40,000.00 

52

    36,000.00 

52

Burettes

(11-100)ml

      40,000.00 

52

      36,000.00 

52

Measuring Cylinder

(0-2000)ml

      40,000.00 

52

              36,000.00 

52

6

UJAZO MDOGO

Bomba ndogo za kupimia ujazo mdogo 

(0-1000) µl

      40,000.00 

52

45,000.00

65

Above 1000  µl

      60,000.00 

78

54,000.00

78

Bomba ndogo za kupimia ujazo mdogo zenye Njia Zaidi ya moja

(0 -1000)

120,000.00


155


117,000.00


168


Chupa ya Mzunguko

(0-1000) ml

      30,000.00 

39

27,000.00

39

Bika

(0-1000) ml

      30,000.00 

39

27,000.00

39

Sindano

(1-10) ml

      30,000.00 

39

27,000.00

39

 

(0-5) M3

      500,000.00 

647

500,000.00

647

 

(0-10) M3

      750,000.00 

970

750,000.00

970

SYRUP TANKS



(0-15) M3

800,000.00 

1035

800,000.00

1,035

 

(0-20) M3

  1,000,000.00 

1294

1,000,000.00

1,294

 

(0-1000)1 

      160,000.00 

207

160,000.00

207

SIMTANK

(0-2000)1

      250,000.00 

323

250,000.00

323


Matenki ya ujazo mkubwa

(0-5000) M

  2,000,000.00 

2587

2,000,000.00

2,587

(6000-45000) L

12,000,000.00 

15524

12,000,000.00

15,524

ROAD TANKERS

(Each at a cost)

      450,000.00 

582

450,000.00

582

7

MUDA NA MASAFA

5 points measurements

(1-60)s

      90,000.00 

116

81,000.00

116

5 points measurements

(1 to60)min

      100,000.00 

129

90,000.00

129

5 points measurements

(61-180)min

      120,000.00 

155

108,000.00

155

5 points measurements

(180min-24Hrs)

      130,000.00 

168

117,000.00

168

5 points measurements

Above 1 day

      190,000.00 

246

171,000.00

246

Stomacher

Time/ RPM

      110,000.00 

142

99,000.00

142

Centrifuge

Time /RPM

      110,000.00 

142

99,000.00

142

Vortex/ Mixer

Time / RPM

      110,000.00 

142

99,000.00

142

Rotator

Time / RPM

      110,000.00 

142

99,000.00

142

Los Angeles

Time /RPM

      110,000.00 

142

110,000.00

142

Shaker

Time / RPM

      110,000.00 

142

99,000.00

128

Tachometer

Time /RPM

      120,000.00 

155

108,000.00

140

8

DIMENSIONAL(UREFU)

Measuring Tape

(0-30)m

      110,000.00 

142

      110,000.00 

142

Above 30 m

      160,000.00 

207

      200,000.00 

259

Dip tape

 

      110,000.00 

142

      200,000.00 

259

Height gauge

 

      100,000.00 

129

100,000.00

129

Depth /thickness gauge

 

      100,000.00 

129

100,000.00

129

Ruler

 

    100,000.00 

129

100,000.00

129

Dipstick Marking

 

      180,000.00 

233

180,000.00

233

Tank Marking

(0-2000) mm

      150,000.00 

194

150,000.00

194

(0-4000)mm

      230,000.00 

298

230,000.00

298

(0-6000) mm

      300,000.00 

388

300,000.00

388

Micrometer Screw

(0-50) mm

85,000.00

110


100,000.00

129

Gauge


155

Vernier Calipers

(0-150) mm

      95,000.00 

123

100,000.00

129

(0-500) mm

      100,000.00 

129

120,000.00

155

Dial Indicators/gauges

 

      85,000.00 

110

100,000.00

129

Height gauges

 

      85,000.00 

110

100,000.00

129

Set of Gauge Blocks

(0-10) mm

      40,000.00 

52

        40,000.00 

52

Above 10 mm

      45,000.00 

58

        45,000.00 

58

Penetrometer

 

      85,000.00 

110

100,000.00

129

GO-NO-GO gauge

 

      85,000.00 

110

100,000.00

129

9

SHINIKIZO

Pressure Gauge

(0-4) bar

      70,000.00 

91

72,000.00

103

Sphygmomanometer

(0-40) bar

      80,000.00 

103

90,000.00

129

Differential pressure

(41-100) bar

      100,000.00 

129

117,000.00

168

Pressure transmitter & switch

(101-400) bar

      115,000.00 

149

117,000.00

168

(401-1000) bar

      125,000.00 

162

135,000.00

194

(1001-4000) bar

      135,000.00 

175

135,000.00

194

Dead Weight Tester/Pressure balance

 

      200,000.00 

259

250,000.00

323

Pressure Safety Valves

(0-20) bar

      115,000.00 

149

200,000.00

259

(PSV)

(21-100) bar

      165,000.00 

213

200,000.00

259

(Above 100) bar

      215,000.00 

278

250,000.00

323

10

UMEME

 AC/DC

Potentiometer

 

      180,000.00 

233

220,000.00

285

Ohmmeter

 

      150,000.00 

194

170,000.00

220

Resistor

 

      100,000.00 

129

150,000.00

194

Ammeter

 

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Resistance meter

 

      100,000.00 

129

150,000.00

194

Voltmeter

 

      100,000.00 

129

150,000.00

194

Standard cell

 

      100,000.00 

129

150,000.00

194

Decade resistance Box

 

      180,000.00 

233

230,000.00

298

Megger

 

      150,000.00 

194

180,000.00

233

Levelling staff

 

      80,000.00 

103

100,000.00

129

DMM Voltage and Resistance Measurements

Range 61/2Digit

      200,000.00 

259

250,000.00

323

Range 5 1/2 Digit

      250,000.00 

323

300,000.00

388

Range 4 1/2 Digit

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Range 3 1/2 Digit

      100,000.00 

129

150,000.00

194

DMM Current Measurements

Range 6 1/2 Digit

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Range 5 1/2 Digit

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Range 4 1/2 Digit

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Energy meter

Single phase

      150,000.00 

194

200,000.00

259

Three phase

      250,000.00 

323

300,000.00

388


MAELEZO

Tozo hizi zinajumuisha gharama za uendeshaji kama vile utunzaji wa vifaa na manunuzi wa mahitaji ya ugezi.





TOZO ZA VIPIMO VIPYA VYA MAABARA  



Na. 

VIPIMO VIPYA

TOZO ZA VIPIMO ZINAZOPENDEKEZWA (SHILINGI ZA KITANZANIA) 

MAABARA YA UHANDISI UJENZI

1

Upimaji wa wiani (density) na kiwango cha unyevu kwenye lami (pavement) 

30,000/=

MAABARA YA UHANDISI WA MITAMBO

1

Upimaji wa utofauti wa mgandamizo kwenye chujio la mafuta na upepo

50,000/=

2

Upimaji wa joto la juu kwenye chujio la mafuta na upepo)

45,000/=

3

Upimaji wa ufanisi kamili wa maisha ya chujio la mafuta na upepo

165,000/=

4

Upimaji wa uwezo na ufanisi wa chujio la mafuta na upepo kuhimili vumbi

250,000/=

MAABARA YA KEMIA

1

Upimaji wa Spot kwenye rangi (thinner) 

20,000/=


MAABARA YA VIFUNGASHIO

1

Upimaji wa kiwango cha mvuke kinachopitishwa kwenye vifungashio vya vyakula (WVTR)

50,000/=

2

Upimaji wa kiwango cha hewa ya oksijeni kinachopitishwa kwenye vifungashio vya vyakula (OTR)

50,000/=


MAABARA YA NGUO NA NGOZI

1

Upimaji wa ugumu wa soli za viatu

30,000/=

2

Upimaji wa chromium kama chromic oxide (Cr2O3) kwenye bidhaa za ngozi

50,000/=

3

Upimaji wa uimara wa mshono kwenye mshono wa nguo

50,000/=

4

Upimaji wa uimara wa kifungo/kishikizo kwenye  nguo

40,000/=

5

Upimaji wa  uimara wa Poly Vinyl Chloride (PVC coated fabric) dhidi ya kuchomwa 

50,000/=

6

Upimaji wa mgandamizo kwenye mpira wa michezo

20,000/=

7

Upimaji wa kiasi cha unyevu kwenye bidhaa za nguo na ngozi

30,000/=

8

Upimaji wa rangi za bendera ya taifa (Pantone Matching System) 

20,000/=

MAABARA YA CHAKULA

1

Upimaji wa bakteria waaozalisha Hydrogen sulphide 

40,000/=

2

Upimaji wa Leuconostoc mesenteroides

40,000/=


MAELEZO

  1. Hizi ni tozo za vipimo vipya ambavyo Shirika limejenga uwezo wa upimaji kutokana na 

uwepo wa bidhaa mpya sokoni, viwango vipya na ukuaji wa teknolojia. 

  1. Hizi tozo zinajumuisha gharama za kununua, kemikali na mahitaji mengine ya upimaji 

  2.  pamoja na gharama za uendeshaji wa mashine.


TOZO YA UKAGUZI WA BIDHAA ZINAZOINGIA KUTOKA NJE YA NCHI

S/N

HUDUMA

TOZO

TOZO YA SASA

TOZO PENDEKEZWA

1.

Ukaguzi wa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi isipokuwa magari yaliyotumika

Tozo ya kuthibitisha ubora wa shehena

0.2% ya Gharama na Usafirishaji (C&F) kulingana na thamani ya mzigo iliyotathminiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

6 Tsh/Kg

MAELEZO


1.

Tozo ya kuthibitisha ubora wa shehena inakusudiwa kulipia gharama za ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa sokoni.


2.

Tozo ya zamani ilikokotolewa kwa kujumuisha gharama ya kusafirisha shehena nzima bila kuonyesha kiwango kilichotumika kwa kila bidhaa iliyopo kwenye orodha ya bidhaa zilizosafirishwa ili kutenganisha kati ya bidhaa zinazodhibitiwa na TBS na zile zinazodhibitiwa na taasisi nyingine.


3.

Tozo inayopendekezwa itatozwa kulingana na uzito wa shehena badala ya thamani yake.



KIMABATISHO NA. 6


MABORESHO YA TOZO ZA HIFADHI ZA BAHARI NA MAENEO TENGEFU, 2009.

MAREKEBISHO YANAYOPENDEKEZWA

S/N

TOZO ZA SASA

MAPENDEKEZO

A

ADA YA KIINGILIO KWA MTU MMOJA KWA SIKU KATIKA HIFADHI ZA BAHARI

1.

(i) Wenye umri zaidi ya miaka 15- 

  • Mtanzania-         Tshs. 2,000.00 

  • Asiye Mtanzania) - US$ 20




(ii) Umri kati ya miaka 5 hadi 15-


  • Mtanzania            -   Tshs. 1,000.00 

  • Asiye Mtanzania) -   US$ 10 











(iii) Watoto wenye umri chini ya miaka 5- 

  • Watanzania - Bure

  • Wasio Watanzania - Bure


  1. Kwa mtu Mwenye umri wa miaka 16 au zaidi-

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - Tshs. 10,000.00 

  • Wageni ambao sio raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 20

  • Wageni wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 10


(ii) Umri wa kati ya miaka 5 hadi 15- 


  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - Tshs. 2,000.00 

  • Wageni ambao sio raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 10

  • Wageni wasio raia wa nchi Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 5

 

Kuongeza kipengele kipya - 

(iii) Wanafunzi-

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- Tshs.  5,000.00

  • Ambao sio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 10

  • Wanafunzi wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 5


 (iv) Watoto wenye umri chini ya miaka 5     

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- Bure

  • Ambao sio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - Bure

  • Wanafunzi wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania – Bure







B.

ADA YA KIINGILIO KWA MTU MMOJA KWA SIKU KATIKA MAENEO TENGEFU 



(i) Wenye umri zaidi ya miaka 15- 

  • Mtanzania-         Tshs. 2,000.00 

  • Asiye Mtanzania) - US$ 20






(ii) Umri kati ya miaka 5 hadi 15-

  • Mtanzania            -   Tshs. 1,000.00 

  • Asiye Mtanzania) -   US$ 5












(iii) Watoto wenye umri chini ya miaka 5- 

  • Watanzania - Bure

  • Wasio Watanzania - Bure


  1. Kwa mtu Mwenye umri wa miaka 16 au zaidi-

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - Tshs. 10,000.00 

  • Wageni ambao sio raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 15

  • Wageni wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 10



(ii) Umri wa kati ya miaka 5 hadi 15- 

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - Tshs. 2,000.00 

  • Wageni ambao sio raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 10

  • Wageni wasio raia wa nchi Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 5


Kuongeza kipengele kipya - 

(iii) Wanafunzi-


  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- Tshs.  5,000.00

  • Ambao sio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - US$ 10

  • Wanafunzi wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - US$ 5


(iv) Watoto wenye umri chini ya miaka 5     

  • Raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- Bure

  • Ambao sio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - Bure

  • Wanafunzi wasio raia wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye vibali vya makazi Tanzania - Bure


C.

MALIPO YA BOTI NA ADA ZA UVUVI WA MICHEZO KATIKA HIFADHI ZA BAHARI



(i) Boti binafsi za burudani zisizo za kibiashara zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 5 (tano) - US$ 100

 


(ii) Boti za burudani za kibiashara zikiwemo za kukodi zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 5 (tano) - US$ 200 


(iii) Boti za uvuvi wa michezo zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 5 (tano)   - US$ 200 


(iv) Meli/Boti za abiria za utalii  zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 5 (tano)   - US$ 1,000


(v) Ada ya uvuvi wa michezo kwa watalii wanaotumia Boti zinazomilikiwa na wawekezaji waliosajiliwa kwenye Hifadhi za Bahari au boti za michezo zilizoingia kihalali kwenye maeneo ya Hifadhi kwa muda usiozidi siku 5 (tano)- US$ 50 




(vi) Ada kwa wavuvi waliopo kwenye boti za uvuvi wa michezo kwa muda usiozidi siku 5 - US$ 50 


(i) Boti binafsi za burudani zisizo za biashara zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 7 (saba) - US$ 100



(ii) Boti za burudani za kibiashara zikiwemo za kukodi zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 7 (saba) - US$ 200.



(iii) Boti za uvuvi wa michezo zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 7 (saba)   - US$ 200 


(iv) Meli/Boti za abiria za utalii  zinazoingia na kukaa kwa muda usiozidi siku 7 (saba)   - US$ 1,000



(v) Ada ya uvuvi wa michezo kwa watalii wanaotumia Boti zinazomilikiwa na wawekezaji waliosajiliwa kwenye Hifadhi za Bahari au boti za michezo zilizoingia kihalali kwenye maeneo ya Hifadhi kwa muda usiozidi siku 7 (saba) - US$ 50 



(vi) Ada kwa wavuvi waliopo kwenye boti za uvuvi wa michezo kwa muda usiozidi siku 7 - US$ 50 


Kipengele kipya-


(viii) Kibali cha Boti za kasi kwa mwezi - US$ 100 


(x) Kibali cha Boti za kioo za ndani kwa mwezi -US$ 100 

D.

BOTI ZILIZOSAJILIWA ZINAZOFANYA KAZI KWENYE MAENEO TENGEFU



(i) Ada ya Boti za abiria kwa mwezi zenye uwezo wa kubeba watu 7 (saba) - US$ 300 







(i) Ada ya Boti za abiria kwa mwezi zenye uwezo wa kubeba watu 7 (saba)  hadi ishirini (20)- US$ 100 


(ii) Ada kwa mwezi kwa Boti yenye uwezo wa kubeba abiria ishirini na moja (21) na kuendelea - US$ 150 


Kipengele kipya

(iii) Meli kubwa za watalii kwa siku 7 (saba) - US$ 1000 

(iv) Kibali cha Boti za kasi kwa mwezi - US$ 100.

(v) Kibali cha Boti za kioo za ndani kwa mwezi -US$ 100

E.

TOZO ZA UWEKEZAJI (CONCESSION)



(i) Kibali cha kuendesha shughuli za kijamii (mf. migahawa, na kambi za usiku) katika maeneo Tengefu - USS 1,200 kwa mwezi.






















(ii) 

Kibali cha kuendesha shughuli za kijamii (Mf. Hoteli za kitalii na kambi za usiku) katika Hifadhi za Baharu tozo ni - US$ 1,500 kwa mwezi.








  1. Kibali cha kuendesha shughuli za kijamii (mf.  Migahawa, kambi za usiku) kulingana na aina tofauti za uwekezaji;


AINA ZA UWEKEZAJI


(i)  Maeneo Tengefu (US$)


    A            B             C          D

40,000    20,000   10,000    2,500


      (ii) Hifadhi za Bahari (US$)


    A             B              C        D

25,000    10,000    3, 000    1,000


AINA YA UWEKEZAJI

A = Hoteli za Nyota Nne na kuendelea

B = Nyota Tatu 

C = Hoteli za Nyota Mbili, Huduma za Kuzamia na huduma nyingine za   

        michezo ya kwenye maji

D = 

Nyumba za kulala wageni, Nyumba za mapumziko,

Hosteli, Malazi ya nyumbani ya watalii (Home stay),maduka ya zawadi na Migahawa


Zingatia: Kiasi pendekezwa ni kadirio la chini kwa kila aina.


(ii) Tozo za uwekezaji maeneo yenye rasilimali za upekee (prime area) - US$ 50,000 kwa mwaka.

Kipengele kipya


(iii) Kodi za kutua ndege za baharini na helikopta - US$ 100 kwa kila mtuo.


(iv) Waongoza watalii watatakiwa kulipa kodi ya kuongoza watalii - US$ 50 kwa mwaka.


F.

TOZO ZA KUPIGA PICHA KIBIASHARA



Upigaji picha wa aina tofauti mf. picha mnato,filamu kwa ajili ya biashara ndani ya maeneo Tengefu au Hifadhi za Bahari atalipa US$ 1,000 kwa siku saba (7).


Upigaji picha wa aina tofauti mf. picha mnato,filamu kwa ajili ya biashara ndani ya maeneo Tengefu au Hifadhi za Bahari atalipa US$ 200.00 kwa siku.


G.

MGAWANYO WA MAPATO KATI YA MPR NA WADAU WAKUU



Kiasi cha mapato baada ya makato (net revenue) kitagawanywa kati ya MPRU na jamii ambazo ziko katika maeneo ya hifadhi kwendana na sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kitagawanywa kama ifuatavyo;


  1. Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU)-70%


(ii)  Halmashauri ya Wilaya


(iii) Jamii zilizoko katika maeneo ya Hifadhi- 20%   



Kiasi cha mapato baada ya gharama za uhifadhi kitagawanywa kati ya hifadhi  na jamii inayozunguka hifadhi husika   kuendana na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kitagawanywa kama ifuatavyo;




(i)Kugharamia Uhifadhi  - 70%


 

(ii) Mamlaka ya Serikali za mitaa hifadhi inakopatikana  - 5%


(iii) Jamii zilizoko katika maeneo ya Hifadhi- 10%


 (iv) Gawio la Mfuko Mkuu wa Serikali (Consolidated Fund) 15%






No comments:

Post a Comment