TASAF YAWAINUA KIUCHUMI WANANCHI 2,212 MANISPAA YA SINGIGA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 17 March 2021

TASAF YAWAINUA KIUCHUMI WANANCHI 2,212 MANISPAA YA SINGIGA


Mariam Kassim mkazi wa Kata ya Ipembe Manispaa ya Singida akipika vitumbua katika ofisi yake iliyopo Mtaa wa Soko mjini hapa leo,  baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Wateja wakinunua vitumbua ofisini kwa Mariam Kassim.

Mnufaika wa TASAF, Pili Radhaman ambaye ana mradi wa kuuza kokoto, akiwa mbele ya nyumba yake (Tembe) aliyokuwa akiishi kabla ya kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)



Muonekano wa nyumba ya kisasa aliyoijenga Pili Ramadhan.

Mnufaika wa TASAF, Hassan Ng'imba ambaye ana mradi wa kuuza kokoto, akiwa mbele ya nyumba yake (Tembe) aliyokuwa akiishi kabla ya kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Muonekano wa nyumba ya kisasa aliyoijenga  Hassan Ng'imba.


Hassan Ng'imba mkazi wa Mtaa wa Mnung'una Manispaa ya Singida akiponda kokoto katika kiwanda chake kidogo, ambazo lori moja huziuza kati ya sh. 130,000 hadi 140,000 baada  ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  TASAF.

Mwanahamisi Athuman mkazi wa Kibaoni ambaye anajishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na ufugaji akielezea mafanikio yake baada ya kuwezeshwa na mpango huo.

Shamba la mahindi la Mwanahamisi Athuman.

Mratibu wa TASAF Manispaa ya Singida, Juma Mkumbo Nzovu, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF ndani ya Manispaa hiyo.

Mnufaika wa mpango huo, Joyce Lissu ambaye anajishughulisha na ufugaji wa nguruwe akielezea mafanikio yake baada ya kuwezeshwa na TASAF.


Na Dotto Mwaibale, Singida 

WANANCHI 2,212 katika Manispaa ya Singida mkoani hapa wamenufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Manispaa ya Singida, Juma Mkumbo Nzovu wakati wa ziara ya maofisa wa mpango huo na waandishi wa habari ya kuwatembelea wanufaika hao iliyoanza jana mkoani hapa.

Nzovu  alisema tangu mradi huo uanze manispaa hiyo imepokea takribani sh.bilioni 4.5 kwa ajili ya ruzuku za TASAF ambazo zimegawanyika katika maeneo mbalimbali.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ruzuku ya msingi na masharti, ajira za muda yaani PWP, shughuli za wasichana balehe na wanawake vijana AGYW ambao wanapata ruzuku ili waweze kutimiza malengo yao wakiwa shuleni na wengine kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanyia biashara. 

" Mpango huu wa TASAF umeweza kuwasidia walengwa wengi kwa kujipatia kipato kwa kuwekeza, kujenga nyumba bora na sasa hivi hakuna malalamiko tena ya kuwa na uhaba wa chakula kwani wanajipatia kupitia ruzuku hizo za TASAF." alisema Nzovu.

Aidha Nzovu alisema zipo changamoto chache lakini nyingi ambapo wamezitoa zinaendelea kufanyiwa kazi na TASAF na madu mfupi ujao tutapata majibu.

Alitaja moja ya changamoto kubwa kuwa ni Kaya nyingi ambazo ni duni zaidi katika manispaa hiyo kuwa na uhitaji wa kujiunga kwenye mpango huo wa TASAF ambapo wanaamini watakumbukwa ili nao waingie.

Mariam Kassim mkazi wa Kata ya Ipembe mnufaika wa mpango huo anayejishughulisha na biashara ya kuuza vitumbua alisema TASAF imemsaidia sana kwani hivi sasa anamtaji mkubwa na ana ndoto ya kujenga nyumba kubwa na kununua gari.

" Awali niliogopa kujiunga na TASAF nikidhani walikuwa ni Freemason lakini baadae niliwaelewa kwani walinikuta nikiwa napika kilo mbili tu za vitumbua ambapo baada ya kunipa ruzuku niliendelea hadi nikapata sh.650,000 na hadi leo naendelea na biashara hii ambayo imeniwesha kuwasomesha watoto wangu na mmoja ana malizia shahada yake chuo kikuu.

Alisema mbali ya kufanya biashara hiyo ya vitumbua kupitia mpango huo anafuga kuku na amejiunga katika kikundi cha kukopeshana pesa.

Mnufaika mwingine Hassan Ng'imba anasema hapo awali hata huo mlo mmoja na familia yake  ilikuwa ni changamoto lakini baada ya kujiunga na mpango huo wanapata milo yote mitatu na ameweza kujenga nyumba ya kisasa na kuwa hivi sasa anajishughulisha na mradi wa kuuza kokoto kupitia kiwanda chake kidogo kilichopo mtaa wa Mnung'una pia amejiunga katika kikundi cha kukopeshana fedha.

Wanufaika wengine wa mpango huo ni Mwanahamisi Athuman, mkazi wa Kibaoni ambaye anajishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na ufugaji, mwingine ni Pili Radhaman ambaye ana mradi wa kuuza kokoto na Joyce Lissu ambaye anajishughulisha na ufugaji wa nguruwe ambapo wote kwa pamoja wamefanikiwa kujenga nyumba za kisasa na kusomesha watoto wao. 

No comments:

Post a Comment