Brigedia Generali John Julius Mbungo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Taasisi inayosimamia haki za wananchi nchini.
Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Barabara Tanzania, (TANROADS) Mkoa wa Pwani unatarajia kuilipa sh. milioni 6 familia ya Ally Segamba ya Kijiji cha Ujamaa Palaka kilichopo wilayani Kisarawe.
Fedha hizo ambazo kwa mujibu wa familia hiyo ni Shilingi Milioni 6,000,000 ni kwa ajili ya malipo yaliyotokana na Tanroads kuingia mkataba na familia hiyo Desemba 10, mwaka jana kuchimba kokoto kwenye shamba lao.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Segamba alisema tangu mkataba huo kwisha walifuatilia malipo yao Tanroads bila mafanikio baada ya kuwekewa mizengwe ya hapa na pale.
“Tulipoona tunafuatilia tulipwe fedha zetu bila mafanikio tuliandika barua ya malalamiko kwa uongozi wa Tanroads ambayo nakala tulizipeleka kwa Rais John Magufuli, Mkurugenzi wa Takukuru nchini, Takukuru Mkoa wa Pwani na kwa Maveterani wa UVCCM Taifa kuomba msaada wao,” alisema mwanafamilia huyo.
Aliongeza walifikia hatua hiyo baada ya kuona Tanroads wamekiuka makubaliano yaliyomo kwenye mkataba yanayoelekeza malipo yao yafanyike siku saba baada ya mkataba kwisha lakini wao hawajafanya hivyo.
“Tulichobaini kinachowafanya Tanroads watusumbue kutulipa kuna baadhi ya watendaji wa wakala hao wa barabara mkoa wa Pwani kutaka wapewe mgawo kwa kisingizio cha mtu ambaye hahusiki katika shamba letu waliyemtengenezea nyaraka feki ili naye aonekane ni mmiliki wa shamba letu waliyeingia naye mkataba wa kuchimba kokoto katika shamba letu la mirathi ili fedha hizo zitakapolipwa naye apewe mgawo ambao watagawana.”
Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana na Mhandisi wa Tanroads mkoani humo, Livingstone Urio aliyekuwa miongoni mwa maafisa wa Tanroads waliosaini mkataka huo, alikataa kuzungumza chochote kwa kuwa si msemaji ambapo alimtaka mwandishi wetu awasiliane na Meneja wa Tanroads wa mkoa, Mhandisi Yudas Msangi.
Msangi alikiri kuufahamu mkataba huo na kuahidi kuilipa familia hiyo fedha zao ndani ya wiki mbili baada ya mkandarasi kuandaa malipo yao na kuwapelekea.
“Siyo kwamba hatuwalipi, tulikuwa tunasubiri mkandarasi anayesimamia miradi mingi aandae malipo yao atuletee ndipo tuwalipe, jana (juzi) ndiyo katuletea hivyo tutawalipa ndani ya hizi wiki mbili, lakini wao wenyewe wanamigogoro hivyo pesa hizo tutazipeleka kule kijijini,” alisema Msangi.
No comments:
Post a Comment