Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka watendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kufanyakazi kwa bidii na wale watakaoonekana kushindwa kutekeleza majukumu yao Serikali itaawachukulia hatua ikiwa ni pamoja kuwaondoa.
Dkt Abbasi ameyasema hayo Machi 03,2021 jijini Dar es Salaam alipofanya vikao vya kukagua utekelezaji wa kazi na maagizo ya viongozi kwa Baraza hilo pamoja na pia Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA).
"Katika siri sita za mageuzi na mafanikio ambazo nimekuwa nikiwaeleza siku zote ni kuwa na timu yenye ari, maadili na inayojituma, hili kwa watendaji ni jambo la muhimu sana katika Serikali yetu ya kimageuzi kufanikiwa katika malengo ya kuivusha Tanzania, na hapa BMT wapo watu kama hawajaelewa hili," alisema Dkt. Abbasi.
Katibu Mkuu Dkt. Abbasi ameongeza kuwa kuna baadhi ya hatua zimeanza kuchukuliwa kutokana na utendaji mbovu akiwemo aliyekuwa Kaimu Msajili wa Vyama vya Michezo.
"Mtendaji Mkuu pendekeza ndani ya siku saba mtu mwingine wa Kukaimu nafasi hiyo ulete wizarani, huyu Msajili aliyekuwepo hapa amesharejeshwa kwenye majukumu ya taaluma yake."alisisitiza Dkt.Abbasi
Aidha, Dkt. Abbasi alitumia kikao hicho na BMT kuonya baadhi ya watendaji akiwemo mmoja wa watumishi wa Idara ya Utawala katika Baraza hilo kuwamua kubadilika la sivyo atabadilishwa.
"Wizara inapokea malalamiko mengi kuhusu utendaji wako sasa inawezekana ni majungu au kweli una tatizo. Kazi ya Idara ya utawala ni kufanikisha mambo sio kukwaza watumishi na kuwatengenezea jakamoyo. Sasa wewe nilikuwa niondoke na wewe leo, lakini ngoja tukupe muda kukuangalia zaidi."Dkt. Abbasi
Hata hivyo, awali Dkt. Abbasi alizungumza na Menejimenti ya COSOTA ambapo alisisitiza watendaji hao kukamilisha maboresho ya mifumo yanayoendelea, ili wasanii na wabunifu wengine waanze kupata migao yao huku akisisitiza moja ya nguzo kuu za Wizara kwa sasa ni pamoja na kuona utawala na utendaji bora kuanzia Wizarani, taasisi hadi kwa wadau wa sekta zote.
"Wizara ikiongozwa na Mhe. Waziri wetu Innocent Bashungwa na Naibu wake Abdallah Ulega kwa sasa katika nguzo muhimu za mageuzi katika sekta zetu nne tumekubaliana hili la utawala bora kuanzia Wizarani, kwenye Taasisi na hadi kwenye asasi za wadau wetu ni muhimu na tutalisimamia ipasavyo. Zama za uzembe, majungu, mizungu na watu kuwekeza katika fitna na akadabraha zimekwisha. Tunanyoosha mambo, kila mtu alipo anyooke kabisa kabla hatujafika kumnyoosha." Aliendelea kusisitiza Dkt. Abbasi.
No comments:
Post a Comment