Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme akikagua mradi wa maji katika kitongoji cha Litete wilayani Namtumbo. |
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumzia maadhimisho ya wiki ya maji mkoani Ruvuma yanayoanzia Machi 16 hadi 22 mwaka huu. |
Na Albano Midelo, Ruvuma
SERIKALI ya Awamu ya Tano imetoa zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Maji Mkoani Ruvuma.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema fedha hizo ni kwaajili ya miradi ya Wilaya za Songea,Mbinga na Tunduru.
“Tunapokwenda kuadhimisha wiki ya Maji kuanzia Machi 16 hadi 22 sekta ya maji imefanya kazi kubwa sana ya kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya kumtua mama ndoo maji kichwani’’,alsema Mndeme.
Amesema kupitia Wakala wa Maji Vijijini RUWASA NA Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira SOUWASA,kazi kubwa imefanyika ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 7 kwaajili ya uwekezaji wa maji ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Hata hivyo amesema hadi sasa fedha iliyopokelewa ni zaidi ya shilingi bilioni tano na kwamba kiwango cha usambazaji wa maji safi wilaya ya Songea kimeweza kuongezeka kutoka asilimia 74 hadi asilimia 86.2.
Kwa mujibu wa Mndeme wilaya ya Mbinga imepokea zaidi ya shilingi bilioni moja na kwamba huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 52.2 hadi asilimia 70.8 na wilaya ya Tunduru imepokea fedha zaidi ya shilingi milioni 600 na kiwango cha usambazaji maji kimeongezeka kutoka asilimia 55 hadi 66.
Hata hivyo Mndeme amesema licha ya mafanikio hayo kuna changamoto za vyanzo vya maji katika Manispaa ya Songea ambazo zinasababisha upungufu wa maji kutoakana na ongezeko kubwa la idadi ya watu na mahitaji ya Maji yanaongezeka.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Mkoa kupitia SOUWASA umefanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo kuhakikisha mtandao wa mabomba unawafikia watumiaji maji kikamilifu.
Mndeme amewapongeza RUWASA Mkoa wa Ruvuma kwa kupambana na kuhakikisha Maji yanapatikana Mijini na Vijijini katika Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa wakazi zaidi ya milioni 1.34.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Rebman Ganshonga amesema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2019 hadi Februari 2021 RUWASA Ruvuma imepokea zaidi ya shilingi bilioni 20 kutoka serikali kuu katika kutekeleza uboreshaji miradi ya maji.
No comments:
Post a Comment