Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo. |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.Seleman Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo huku akielekeza wakurugenzi wote katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha maeneo yote yenye viwanja vya michezo yanayomilikiwa na shule hayavamiwi kuanzia sasa.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo jijini Dodoma katika majumuisho ya kikao kazi endelevu kilicho zikutanisha wizara tatu ambazo ni wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais - TAMISEMI lengo likiwa ni kuweka mikakati ya kuimarisha sekta ya michezo nchini.
Aidha, Waziri. Jafo amewataka wakuu wa shule kuhakikisha wanazingatia somo la Michezo linafundishwa kama ilivyo kwa masomo mengine ili kutoa nafasi ya kutosha kwa watoto kushiriki michezo mbalimbali.
Kwa Upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema wizara yake inaitazama michezo kama ajira na hivyo itahakikisha inaweka mikakati na kutengeneza Mitaala inayotoa fursa kwa wanafunzi kushiriki michezo pindi wawapo shuleni.
Naye akihitimisha Kikao hicho Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameeleza kufuraishwa kwake na namna viongozi hao pamoja na wataalamu kutoka katika wizara zote tatu walivyoshiriki kwa maoni,michango na ufafanuzi wa namna ya kuendeleza Jitihada hizo pamoja katika kutimiza adhima ya Serikali ya kuinua na kuendeleza michezo nchini.
Kikao hicho ni miongoini mwa mikakati ya wizara zote tatu katika safari ya kuhakikisha Tanzania inangara kitaifa na kimataifa katika sekta ya michezo.
No comments:
Post a Comment