MKURABITA YASHIRIKI UZINDUZI WA KITUO CHA USAJILI WA BIASHARA ZANZIBAR - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 9 February 2021

MKURABITA YASHIRIKI UZINDUZI WA KITUO CHA USAJILI WA BIASHARA ZANZIBAR

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Immaculate Senje (katikati) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Islam Seif Salum (kushoto) wakikata kwa pamoja utepe wakati wa uzinduzi wa kituo cha usajili wa biashara katika Ofisi za Baraza la Mfumo wa Utoaji Leseni Zanzibar. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa wizara hiyo, Khamis Ahmada Shauri. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA.


Katibu Mkuu, Salumu na Makamu Mwenyekiti wa  Mkurabita, Senje wakitembelea ofisi za taasisi mbalimbali zinazotoa huduma katika kituo hicho.


Viongozi hao wakipata maelezo kutoka kwa watumishi wa taasisi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mkurabita, Glory Mbilimnywa akiangalia moja ya ofisi za taasisi.


Katibu Mkuu  Salumu (kulia), akizungumza wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mkurabita.

Mkurugenzi wa Biashara na Mazoko wa wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Shauri akisoma risala ya urasimishaji Zanzibar.

Mratibu wa  Mkurabita, Dk. Seraphia Mgembe akitoa maneno ya utangulizi wakati wa kikao hicho.



Mjasiriamali Mariamu akitoa ushuhud wa jinsi alivyofanikiwa baada ya  kurasimisha biashara yake.


Na Richard Mwaikenda, Zanzibar

MPANGO wa Kurasimisha Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar wamezindua Kituo Jumuishi cha Usajili wa  Biashara eneo la eneo la Darajani Unguja, Zanzibar.

Uzinduzi wa kituo hicho kilichopo katika Ofisi za Baraza la Mfumo wa Utoaji Leseni Zanzibar, kilizinduliwa kwa kukata kwa utepe na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Immaculate Senje pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Islam Seif Salum.

Baada ya kukata utepe walikagua ofisi za taasisi mbalimbali ziliopo katika kituo hicho ambapo walipata maelezo ya utendaji wa kila taasisi kutoka kwa watumishi.

Wajumbe wengine wa Kamati ya Uongozi na watendaji wa Mkurabita nao walipata wasaa wa kukitembelea kituo hicho ambacho ni msaada mkubwa  kwa wafanyabiashara kwani kinawapunguzia usumbufu kutoka na uwepo wa taasisi zote muhimu katika utoaji leseni na huduma zinginezo.

Awali akielezea kuhusu kituo hicho, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa wizara hiyo, Khamisi Ahmada Shauri, alisema kuwa Mkurabita imetoa zaidi ya sh. mil. 57 ambapo kati ya hizo sh. mil. 27 zimetumika kwa ajili ya urasimishaji na utoaji mafunzo Pemba na Unguja na zaidi ya sh. mil. 29 zimetumika katika ujenzi mdogo wa kituo hicho pamoja na ununuzi wa Kompyuta 4, Printa 2, viti 6 meza sita, kabati 1, kiyoyozi,kununua, Wife na vifaa vingine vidogo vidogo.

Ametaja taasisi zilizopo kwenye kituo hicho kuwa ni; Baraza la Manispaa ya Mjini, Wakala wa Dawa, Chakula na Vipodozi, Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Mapato Zanzibar, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali na Benki ya Watu Zanzibar.

Amesema Kituo hicho kinatarajiwa  kutoa huduma kwa wafanyabiashara walioko Manispaa za mjini pamoja wanaopata huduma kutoka kwa Mkemia Mkuu wakati wa uingizaji wa bidhaa za kemikali nchini. 

"Hii itaweza kuwarahisishia wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi katika sehemu moja na kupunguza urasimu, kupunguza muda wa kuzunguka ofisi ofisi mbalimbali kupata huduma,"alisema Mkurugenzi.

Mkurugenzi Shauri alimalizia kwa kutoa shukrani za dhati kwa Mkurabita kwa kuweza kuanzishwa kwa kituo hicho , kwa vile kitaweza kusaidia sana wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi na wepesi sambamba utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuhamasisha urasimishaji wa biashara na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma ya Serikali kwa Wananchi.

Akizungumza maneno ya awali kabla ya mkumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe aliomba  taasisi za serikali za Zanzibar kuchangia kwa kutenga kwenye bajeti zao fedha za kusaidia urasimishaji wa biashara za wanyonge ili jambo hilo liwe endelevu kwa manufaa ya wananchi.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Salumu alikubaliana na ushauri huo na kuahidi kulifanyia kazi ili taasisi hizo zitenge  kiasi cha fedha katika bajeti ya mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Mkurabita, Immaculate Senje alizipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Ardhi ya Zanzibar kwa kushiriki katika suala la urasimishaji na utoaji mafunzo kwa wajasiriamali.

"Naamini jambo hili tukiliendeleza litaleta manufaa makubwa kwa wananchi wetu na hatimaye maendeleo ya Taifa," alisema Senje.

Wafanyabiashara waliorasimisha biashara zao hadi  sasa kwa upande wa Zanzibar ni 461.

No comments:

Post a Comment