HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2021/22 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 9 February 2021

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2021/22

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

-------------


HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA 

SERIKALI NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 

KWA MWAKA 2021/22 












DODOMA

8 FEBRUARI, 2021

  1. UTANGULIZI


  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha leo hii kukutana ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki na kwako wewe Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kifo cha Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM). Tunamwomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake kwa amani. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa tena kwa ushindi wa kishindo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa  Kassim Majaliwa Majaliwa na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo muhimu katika uongozi wa nchi yetu. Uongozi wao madhubuti unaozingatia maslahi mapana kwa Taifa ulikiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi katika majimbo 256 kati ya majimbo 264 yaliyopo. 


  1. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamisi (Mb), na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo. Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.


  1. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bajeti chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini (CCM) na  Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi (CCM) kwa maoni yao wakati wa majadiliano ya vikao vya kamati. Maoni hayo yamezingatiwa katika kuboresha Mapendekezo ya Mwongozo  wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22. Aidha, napenda kuhakikishia kuwa maoni yatakayotolewa na Bunge lako Tukufu, yatazingatiwa katika kuboresha Mwongozo na Mpango huu. Hivyo, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge katika nafasi yenu ya uwakilishi wa wananchi, mtumie weledi na uzoefu wenu katika kutoa maoni, ushauri kuhusu maeneo muhimu na miradi inayopendekezwa. 


  1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22 yamezingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2011/12 – 2025/26; Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025; Hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 na 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba, 2015 na 2020 mtawalia; Sera na Mikakati mbalimbali ya Kisekta.


  1. Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango kimegawanyika katika sura saba (7): Sura ya kwanza ni utangulizi; Sura ya pili inaainisha mapitio ya hali ya uchumi; Sura ya tatu inaelezea mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; Sura ya nne inaelezea maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2021/22; Sura ya tano inaelezea ugharamiaji wa Mpango; Sura ya sita inaainisha mfumo na utaratibu wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za utekelezaji wa Mpango; na Sura ya saba ni viashiria hatarishi vya utekelezaji wa Mpango na hatua za kukabiliana navyo.

 

  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI


  1. Mwenendo wa Viashiria vya Uchumi


  1. Mheshimiwa Spika, uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara ambapo katika kipindi cha miaka minne (2016 – 2019), Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9. Ukuaji huu umeiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati wa chini (lower-middle income) kutoka kundi la nchi masikini kwa kufikisha wastani wa pato la mtu mmoja mmoja la shilingi 2,577,967 (sawa na dola za Marekani 1,080) mwaka 2019, ambalo ni zaidi ya kigezo cha dola za Marekani 1,036 cha kuingia katika kundi hilo. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi  cha Julai hadi Septemba 2020, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Aidha, Katika kipindi  cha Januari hadi Septemba 2020, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua kwa kasi ya ukuaji katika kipindi husika kumechangiwa na mvua zilizozidi wastani zilizosababisha mafuriko ambayo yaliharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi pamoja na athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa biashara. Aidha, athari kubwa za kiuchumi zilizojitokeza zaidi katika robo ya pili ya mwaka 2020 (Aprili hadi Juni) ambapo shughuli za kiuchumi za hoteli, biashara na elimu zilikuwa na ukuaji hasi kufuatia hatua zilizochukuliwa kwa muda na Serikali za kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi hasa mikusanyiko ikiwemo kufungwa kwa safari za anga pamoja na kusitishwa kwa shughuli zote za sanaa na burudani ikiwemo michezo. Kwa kipindi cha miezi tisa ya mwanzo wa mwaka 2020 (Januari hadi Septemba), sekta zilizokua kwa viwango vikubwa ni pamoja na Sekta ya Ujenzi (asilimia 13.6); Madini na Mawe (asilimia 9.9); Habari na Mawasiliano (asilimia 9.0); Uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo (asilimia 8.9); na Shughuli za kitaalamu,Sayansi na Ufundi (asilimia 8.8). Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazotarajia kuwa na ukuaji chanya mwaka 2020 kutokana na hatua za Serikali za kutowafungia watu ndani (lock down) na kuwaruhusu waendelee na shughuli za kiuchumi na kijamii wakati wa mlipuko wa homa kali ya mapafu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 3.3 katika kipindi cha mwaka unaoishia Desemba 2020 ikilinganishwa na asilimia 3.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kuimarika kwa mfumuko wa bei kulitokana na upatikanaji wa mazao ya chakula cha kutosha katika masoko ya ndani na nchi jirani.

 

  1. Mheshimiwa Spika, urari wa malipo nje ya nchi umeendelea kuimarika, licha ya kuwepo kwa changamoto za kudorora kwa shughuli za kiuchumi duniani kutokana na athari za COVID-19. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje (current account deficit) uliimarika kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 331.3, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 344.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji kwa ajili ya uagizaji wa bidhaa na huduma. Hadi Desemba 2020, kulikuwa na akiba ya fedha za kigeni ya dola za Marekani milioni 4,767.7, ambayo inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi  5.6. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi miezi 4.0 na zaidi ya lengo la miezi 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, Sekta ya benki imeendelea kuimarika ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku ya wenye amana na wakopaji. Kwa mwezi Desemba 2020,  kumekuwa na ongezeko la mapato na faida kutokana na uwekezaji katika rasilimali na mtaji ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2019. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020,  faida ya benki itokanayo na mali (Returns on Asset - ROA) ilifikia wastani wa asilimia 2.03 ikilinganishwa na asilimia 1.82 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Faida ya benki itokanayo na mtaji (Returns on Equity - ROE) ilifikia wastani wa asilimia 7.92 Desemba, 2020 kutoka asilimia 6.80 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 8.1 kwa mwaka 2019/20 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 6.8 mwaka 2018/19, ikiashiria kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zikichagizwa na uwekezaji wa sekta ya umma.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni imeendelea kuwa tulivu. Kwa mwaka 2019/20, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,289.1 ikilinganishwa na shilingi 2,282.3 mwaka 2018/19. Hii inamaanisha kuwa thamani ya shilingi ilipungua kwa kasi ndogo ya wastani wa asilimia 0.30 mwaka 2019/20 ikilinganishwa na asilimia 1.73 kwa mwaka 2018/19. Aidha, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,309.83 ikilinganishwa na shilingi 2,299.97 kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Hali hii inatokana na usimamizi thabiti wa Sera za Fedha na Bajeti. 


  1. Mheshimiwa Spika, hadi Desemba 2020, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 59.01, sawa na ongezeko la asilimia 7.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 54.85 kipindi kama hicho mwaka 2019. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 42.83 na deni la ndani ni shilingi trilioni 16.18. Ongezeko la deni limetokana na: ukopaji kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji; na malimbikizo ya riba ya deni la nje hususan nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris Club ambazo Serikali inaendelea kujadiliana nazo. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba, 2020 imeonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo unaokubalika kimataifa kwa viashiria vyote muhimu. Kwa mwaka 2020/21 thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 17.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; na thamani ya sasa  ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 113.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240. Aidha, ulipaji wa deni la nje kwa mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 13.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23.

 

  1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi yanapatikana katika Sura ya Pili ya Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango na Sehemu ya Kwanza, Sura ya Pili ya kitabu cha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22.

 

  1. Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2019/20


  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, mapato ya ndani yalifikia shilingi trilioni 20.29, sawa na asilimia 88.0 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.62 mapato ya kodi yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania,  sawa na asilimia 92.3 ya lengo. Aidha, shilingi trilioni 1.95 ni mapato yasiyo ya kodi, sawa na  asilimia 85.9 ya lengo na shilingi bilioni 717.2 ni mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, sawa na asilimia 93.7 ya lengo. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, fedha za misaada na mikopo nafuu zilizopokelewa zilikuwa shilingi trilioni 3.52 sawa na asilimia 126.3 ya lengo. Kuvuka lengo kwa misaada na mikopo nafuu kulitokana na Washirika wa maendeleo kuongeza viwango vya misaada waliyoahidi awali kutokana na mahusiano mazuri kati ya nchi yetu na Washirika hao wa maendeleo. Mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara iliyopatikana ni shilingi trilioni 1.82 sawa na asilimia 78.7 ya lengo. Kutofikiwa kwa lengo kumetokana na masharti magumu katika soko la mitaji la kimataifa.  Mikopo iliyopatikana kutoka soko la ndani ni shilingi trilioni 4.96 sawa na asilimia 100 ya lengo. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019/20, mapato yaliyokusanywa kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje ni shilingi trilioni 30.59, sawa na asilimia 92.4 ya lengo la mwaka la shilingi trilioni 33.11. Aidha, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya shilingi trilioni 28.57, sawa na asilimia 86.3 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 20.21 ni za matumizi ya kawaida sawa na asilimia 96.9 ya lengo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi trilioni 8.11 zilizotumika kulipa madeni ya fedha zilizokopwa kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, shilingi trilioni 7.30 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na shilingi trilioni 4.80 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, shilingi trilioni 8.37 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa fedha zilizopitia Mfuko Mkuu wa Serikali sawa na asilimia 68.3 ya bajeti ya maendeleo. Vile vile, jumla ya shilingi trilioni 1.46 ni fedha za Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi na hivyo kufanya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 80.2.

 

  1. Utekelezaji wa Bajeti kwa Kipindi cha Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2020/21


  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21, mapato yaliyokusanywa kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje ni shilingi trilioni 13.84 sawa na asilimia 87.3 ya lengo. Kati ya mapato hayo, mapato ya ndani yalifikia shilingi trilioni 10.45, sawa na asilimia 88.9 ya lengo. Kati ya mapato ya ndani: shilingi trilioni 9.05 zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, sawa na asilimia 89.5 ya lengo; shilingi trilioni 1.03 ni mapato yasiyo ya kodi, sawa na  asilimia 84.0 ya lengo; na shilingi bilioni 376.5 ni mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, sawa na asilimia 89.0 ya lengo. Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa malengo ya mapato ya ndani yanafikiwa ikiwemo: Kuendelea kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya kukusanyia mapato, kuhimiza matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea stakabadhi (EFD), kusimamia ukusanyaji kwa mfumo wa vitalu (Block management) na kuimarisha elimu na huduma ya walipakodi. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, Misaada na mikopo nafuu ilifikia shilingi bilioni 971.2, sawa na asilimia 63.1 ya lengo na mikopo kutoka masoko ya ndani shilingi trilioni 2.41, sawa na asilimia 94.6 ya lengo. Mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yalifikia kiwango cha juu ambacho hakijawahi kutokea cha shilingi trilioni 2.09 Desemba 2020. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, ridhaa ya matumizi iliyotolewa katika kipindi kilichoishia Desemba, 2020/21 ilikuwa shilingi trilioni 13.12, sawa na asilimia 82.8 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 10.52 ni fedha za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 95.2 ya lengo na shilingi trilioni 2.60 ni fedha za maendeleo, sawa na asilimia 54.2 ya lengo. Fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa zinajumuisha: shilingi trilioni 3.79 kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 97.7 ya lengo; shilingi trilioni 4.02 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali kwa fedha ambazo zilitumika kugharamia miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 92.9 ya lengo; na shilingi trilioni 2.71 kwa ajili matumizi mengineyo (ikijumuisha shilingi bilioni 177.8 zitokanazo na vyanzo vya ndani vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa), sawa na asilimia 95.3 ya lengo. Aidha, fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi trilioni 2.51 fedha za ndani na shilingi bilioni 86.2 fedha za nje. Vile vile, kiasi cha shilingi bilioni 734.1 ni fedha za Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi na hivyo kufanya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 69.5.




  1. Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2019/20 yanapatikana katika Sehemu ya Kwanza, Sura ya Pili ya kitabu cha Mwongozo.

 

  1. Utekelezaji wa Baadhi ya Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2019/20 na Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2020/21


  1. Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 ni pamoja na: 

 

  1. Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway- SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 49.2, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 901.8 zimetumika na shilingi bilioni 351.0 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. Aidha, ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam - Isaka (km 970) sehemu ya Dar es Salaam - Kilosa (km 283) umefikia asilimia 94.0 na Kilosa – Isaka (km 687) asilimia 99.8; kukarabati na kurejesha huduma za reli ya Tanga hadi Arusha (km 439); na kununuliwa kwa vichwa vipya 11 vya treni na kukarabatiwa kwa mabehewa 347 ya mizigo na mabehewa 20 ya abiria;


  1. Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Kununuliwa kwa ndege mbili (2) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Bombardier Dash 8 Q400 ambazo zimeanza kufanya kazi; na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya tatu (3) yamekamilika kwa asilimia 90 ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400. Ununuzi huo umeifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 315.2 zimetumika na shilingi bilioni 2.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; 


  1. Viwanja vya Ndege na Rada: Kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Geita (ambao utekelezaji umefikia asilimia 86), Songea (asilimia 91) na Mtwara (asilimia 49.0); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vinavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi bilioni 136.85; kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa  Musoma; kukamilika kwa ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege; kupanuliwa kwa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma; kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege (AGL) katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza; na kupanuliwa na kukarabatiwa kwa viwanja vya ndege vya Bukoba, Mwanza, Arusha, Nachingwea na Iringa. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 56.1 zimetumika na shilingi bilioni 4.5 zimetumika  katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. 


Kununuliwa kwa rada nne (4) za kuongoza ndege za kiraia na kufungwa katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Songwe na Mwanza na hivyo kuongeza kiwango cha usalama wa abiria katika viwanja vya ndani. Katika mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 jumla ya shilingi bilioni 12.5 zimetumika; 


  1. Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Julius Nyerere MW 2,115: Kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere ambapo utekelezaji umefikia asilimia 25.8. Utekelezaji wa mradi huu ulitumia shilingi bilioni 693.2 katika mwaka 2019/20 na shilingi bilioni 128.9 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;


  1. Miradi Mingine ya Umeme: hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya umeme ni: Kukamilika kwa asilimia 100 kwa miradi ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I MW 150, Kinyerezi II MW 240 na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako hadi Songea; kukamilika kwa asilimia 73 ya utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo MW 80; kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Bulyanhulu – Geita; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 76, kuendelea na utekelezaji wa  mradi wa Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea na kuhuisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na maandalizi ya mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; na kuunganishwa umeme kwa  jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 hadi Desemba 2020, sawa na asilimia 81.3. Katika mwaka 2019/20, shilingi bilioni 328.9 zimetumika na shilingi bilioni 172.9 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;


  1. Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania): Kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira; kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma kwa maeneo ya pembezoni mwa eneo la mradi; kukamilika kwa majadiliano ya maeneo mawili (2) kati ya matatu (3) ya mikataba ikiwemo ya Nchi Hodhi na wawekezaji, mkataba wa ubia, mkataba wa bandari na mkataba wa pango la ardhi;


  1. Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: Kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi; na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na kampuni za uwekezaji kuhusu Mikataba Hodhi ya utafutaji na uendelezaji wa mradi. Hadi kufikia Desemba 2020, shilingi bilioni 6.0 zimetumika katika maandalizi ya mradi, ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi;


  1. Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,209 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2019/20 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa; Kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa barabaya ya juu (Interchange) ya Ubungo; kukamilika kwa ujenzi wa madaraja makubwa 12 ambayo ni Magufuli (Morogoro), Nyerere (Dar es Salaam), Magara (Manyara), Kavuu (Katavi), Ruvu Chini (Pwani), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba (Rukwa), Lukuledi (Lindi), Lukuledi II (Lindi), Mara (Mara), Sibiti (Singida) na Mtibwa (Morogoro); na kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 95, Daraja jipya la Tanzanite (Dar es Salaam) asilimia 55.2, Kitengule (Kagera) asilimia 50 na New Wami (Pwani) asilimia 41.4; kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 5.8. Katika mwaka 2019/20, shilingi trilioni 1.93 zilitumika na shilingi bilioni 398.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;


  1. Uendelezaji wa Bandari: Katika Bandari ya Dar es Salaam shughuli zilizofanyika ni: Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 4 (gati namba 1-3 kwa ajili ya mizigo mchanganyiko na gati namba 4 kwa ajili ya mizigo ya kichele mfano ngano na mbolea); kukamilika kwa ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati na 5 hadi 7 (gati namba 5 kwa ajili ya mizigo ya kichele na gati namba 6-7 ni kwa ajili ya makontena). Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 207.6 zimetumika na shilingi bilioni 42.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. 


Katika Bandari ya Mtwara ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha umekamilika ambapo katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 43.6 zimetumika na shilingi bilioni 44.9 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. Katika Bandari ya Tanga ujenzi wa kina cha lango la bandari kutoka mita 4 hadi mita 13 na ujenzi wa gati mbili kwenye kina kirefu umekamilika. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 66.5 zimetumika na shilingi bilioni 20.4 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;

 

  1. Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu: Ziwa Victoria: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambao umefikia asilimia 35; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza; na kupatikana kwa makandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli za MV Umoja na MV Serengeti na kukamilika kwa maandalizi ya mikataba kwa ajili ya ukarabati wa meli hizo; na kukamilika ukarabati wa meli za MV Clarias na ML Wimbi. Aidha, shughuli nyingine zilizokamilika ni: Ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero; ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; ukarabati wa majengo na ofisi za bandari za Ziwa Victoria; kuboresha eneo la kushukia abiria Mwanza North; na ukarabati wa ‘Link Span’ ya bandari ya Mwanza South. Vile vile, katika Ziwa Tanganyika, mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 imesainiwa pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba; na ukarabati wa meli ya MT. Sangara. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 56.2 zimetumika kutekeleza miradi yote katika Ziwa Victoria na Tanganyika na shilingi bilioni 12.8 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. 

 

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja; na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 umekamilika na kuanza kufanya kazi. Katika mwaka 2019/20 shilingi milioni 233.9 zimetumika na shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;


  1. Uendelezaji wa Viwanda: Kujengwa kwa jumla ya viwanda vipya 8,477 kati ya mwaka 2015 – 2019, ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Ujenzi wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi 61,110 mwaka 2019. Katika mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 shilingi bilioni 5.5 zimetumika katika uratibu wa shughuli za viwanda; 


  1. Kiwanda cha Sukari Mkulazi: kuendelea na utekelezaji wa mradi ambapo shughuli zilizofanyika ni pamoja na: kulimwa na kupandwa miwa eneo lenye hekta 2,061 kwenye shamba la Mbigiri; kukamilika kwa ufungaji wa mifumo ya umwagiliaji shamba la Mbigiri kwenye eneo la hekta 700 na kuanza eneo lingine lenye ukubwa wa hekta 756. Vile vile, shughuli nyingine zilizofanyika ni kupatikana kwa mshauri elekezi wa mifumo ya umwagiliaji na mitambo ya kiwanda katika eneo la Mkulazi I.


  1. Kilimo: Kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji ambayo imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu – Mvomero yenye hekta 200 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98, Mvumi – Kilosa yenye hekta 249 (asilimia  100), Msolwa Ujamaa – Morogoro yenye hekta 675 (asilimia 98), Njage – Kilombero yenye hekta 325 (asilimia 100), Shamba la Mbegu Kilangali – Kilosa yenye hekta 400 (asilimia 80); kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 71,000 mwaka 2020; kukamilika kwa ujenzi wa maabara ya mbegu katika Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 45.9 zimetumika na shilingi bilioni 28.7 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;


  1. Mifugo: Kujenga kiwanda kipya cha Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd chenye uwezo wa kuzalisha jozi na soli za viatu 1,200,000 kwa mwaka na kuchakata ngozi futi za mraba 13,000,000 kwa mwaka; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha National Artificial Insemination Center - NAIC kilichopo USA River Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited (Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; kuendelea kuboresha huduma za malisho ya mifugo na majosho; na kuendelea kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 2.76 zimetumika na shilingi bilioni 1.77 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; 


  1. Uvuvi: Kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/16 hadi tani 497,567 zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/16 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi  kwenda masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/20, jumla ya kilo 777,750.0 za mabondo zilisafirishwa; na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi. Katika mwaka 2019/20 shilingi milioni 426.3 zimetumika na shilingi milioni 606.7 zimetumika katika nusu ya kwanza ya 2020/21;


  1. Madini: Kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini; kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kusainiwa kwa mkataba wa ubia wa kampuni ya LZ NICKEL na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuendeleza na kuchimba madini ya Nickel ambapo chini ya mkataba huo imeundwa kampuni ya ubia inayoitwa Tembo Nickel Corporation Limited (kwa umuliki wa hisa 84% kwa Kampuni ya LZ Nickel na Serikali ya Tanzania Hisa 16%); kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali za madini kwa kujenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24 wa Mirerani Manyara pamoja na kujenga One Stop Centre, kufunga vifaa vya ulinzi ikiwa ni pamoja na taa na CCTV Camera kuzunguka ukuta na barabara ya kuzunguka ukuta wa ndani; na kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya Mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Lwamgasa (Geita), Katente (Bukombe) na Itumbi (Chunya). Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 3.08 zimetumika na shilingi bilioni 3.3 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;

 

  1. Miradi ya Afya: Kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto (bone marrow transplant) na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wodi namba 18 ya Sewa Haji pamoja na ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa binafsi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili; Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la X-ray katika Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru – Dodoma;  kununuliwa kwa mashine za digital X-ray na ultrasound, vifaa vya maabara na mashine za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kuotesha vimelea BACTEC 960 (Mycobacteria Growth Indicator Tube - MGIT) na Blood culture machine katika Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu – Kibong’oto; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Burigi (Geita)

 

Vile vile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ambayo imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: kufikia asilimia 98 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala; kukamilika na kuanza kutumika kwa jengo la wagonjwa wa nje na kufikia asilimia 73 ya ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe; na ujenzi wa jengo la ghorofa moja la huduma za upasuaji, radiolojia na maabara na kufikia asilimia 50 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Simiyu. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 321.24 zimetumika na shilingi bilioni 64.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;

 

  1. Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Kukamilika kwa miradi 1,423 ya maji iliyotekelezwa mijini na vijijini ambayo imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji safi na salama. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90); utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega umefikia asilimia 98; kukamilika kwa asilimia 76 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji  wa Same – Mwanga – Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 511.5 zimetumika na shilingi bilioni 226.7 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;

 

  1. Elimu: Kujengwa kwa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za walimu 101, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 252.9 zimetumika na shilingi bilioni 124.8 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;  kukarabatiwa shule kongwe 84 kati ya 89; kuboreshwa kwa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi; kutolewa kwa mikopo ya elimu ya juu jumla ya shilingi trilioni 2.26; na kuimarishwa kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji katika taaluma za Anga na Chuo cha Ufundi Arusha katika taaluma ya Nishati. Katika mwaka 2019/20, shilingi bilioni 734.9 zimetumika na shilingi bilioni 159.0 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; na

 

  1. Ajira: Kutokana na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21, jumla ya ajira 12,773,126 zimezalishwa. Kati ya ajira hizo, ajira za moja kwa moja ni 11,891,772 na ajira zisizo za moja kwa moja ni 881,354. Aidha, jumla ya vijana 65,008 katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020  wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi  ikiwemo mafunzo ya uanagenzi katika fani za ujenzi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, ufundi magari, ufundi bomba, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, uchomeleaji na uungaji vyuma, kilimo na ufugaji, ushonaji, uchorongaji vipuli, uchapaji nyaraka na TEHAMA. Serikali imeendelea kulinda ajira za wazawa kwa kuhakikisha kuwa wageni wanaokuja  kufanya kazi nchini  wanakidhi vigezo vilivyoainishwa  katika Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya mwaka 2015.

 

  1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 yameainishwa katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Tatu).

 

  1. Changamoto za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti na Hatua na Kukabiliana nazo


  1. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na: uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko; kupungua kwa shughuli za kibiashara duniani kutokana na athari za COVID-19; na ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hususan kupitia njia za magendo, uhamishaji wa faida (transfer pricing) kwa kampuni zenye mtandao wa kimataifa na kutokutoa na kudai stakabadhi za kielektroniki (EFD receipt) wakati mauzo yanapofanyika. 


  1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa Mpango na Bajeti, Serikali itaendelea kuchukua hatua zifuatazo: kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na kuimarisha ukaguzi wake; kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa biashara duniani ili kutumia fursa zilizotokana na athari za COVID-19 kwa manufaa mapana ya nchi pamoja na kuchukua hatua za kisera na kiutawala kurejesha biashara zilizoathirika; na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kuendelea kuhamasisha umma juu ya matumizi ya stakabadhi za kielektroniki.

 

  1. MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22


  1. Mheshimiwa Spika, masuala ya msingi yatakayowezesha kufikia shabaha za uchumi jumla ni pamoja na: kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na nchi jirani ili kuwezesha kuendelea kwa shughuli za kiuchumi na kijamii; kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya kimataifa; kuhimili athari za majanga ya asili kama vile mafuriko na magonjwa ya mlipuko; na hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha ziada. 


  1. Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla yatakayozingatiwa katika muda wa kati ni pamoja na:

 

  1. Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2021 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.3 ifikapo mwaka 2023;


  1. Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati;


  1. Mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 na asilimia 16.3 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24;


  1. Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21;


  1. Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na


  1. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).


  1. Mfumo wa Awali wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2021/22


  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.26. Kiasi hiki ni sawa na ongezeko la asilimia 4.0 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21 ya shilingi trilioni 34.88. Ongezeko hili linatokana na: Mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha malipo ya deni la Serikali; mahitaji ya upandishwaji wa madaraja ya watumishi na ajira mpya; na mahitaji ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks Authority - TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority - TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority - NCAA). Mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya Halmashauri) yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi trilioni 26.03 mwaka 2021/22 kutoka makadirio ya shilingi trilioni 24.07 mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 8.6 katika muda wa kati. Uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 71.8 ya bajeti ya mwaka 2021/22 hadi asilimia 76.7 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24. Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi trilioni 21.47 mwaka 2021/22 kutoka shilingi trilioni 20.14 mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 7.1 katika muda wa kati. Mapato yasiyo ya kodi (yakijumuisha mapato ya Halmashauri, mapato ya utalii na mapato mengine yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania) yanakadariwa kuwa shilingi trilioni 4.56 mwaka 2021/22 na kuongezeka kufikia shilingi trilioni 5.60 mwaka 2023/24.

  2. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.89 sawa na asilimia 7.9 ya bajeti yote mwaka 2021/22. Katika kipindi hicho, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.99 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho shilingi  trilioni 3.15 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha shilingi trilioni 1.84 sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 2.35 mwaka 2021/22.

 

  1. Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni 36.26, ambapo shilingi trilioni 23.0 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 13.26 ni matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote. Matumizi ya kawaida yanajumuisha mishahara shilingi trilioni 8.15 (sawa na asilimia 31.3 ya makadirio ya mapato ya ndani), malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje shilingi trilioni 8.88 na matumizi mengineyo shilingi trilioni 5.97. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi trilioni 10.37 fedha za ndani na shilingi trilioni 2.89 fedha za nje. Makadirio ya matumizi ya maendeleo yamezingatia kukamilika kwa miradi mbalimbali kama vile maboma ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya ambayo yanahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji.

 

  1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu sera za mapato na matumizi katika muda wa kati yapo katika Sehemu ya Kwanza, Sura ya Tatu ya Kitabu cha Mwongozo.

 

  1. Maelekezo Mahsusi ya Mwongozo


  1. Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22 umeainisha maelekezo mbalimbali ambayo Maafisa Masuuli watatakiwa kuyazingatia wakati wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa. Hivyo, Maafisa Masuuli watatakiwa kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake. Baadhi ya maelekezo yaliyobainishwa katika Mwongozo huu ni kama ifuatavyo:


  1. Uandaaji


  1. Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga angalau asilimia 40 ya mapato ya ndani yasiyolindwa kwenda kwenye miradi ya maendeleo;


  1. Kuzingatia matakwa ya Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370 kwa kutenga na kuwasilisha katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ya Taasisi na asilimia 70 ya ziada ya mapato baada ya kutoa matumizi yaliyoidhinishwa;


  1. Kupata idhini kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha kabla ya kupokea mikopo, misaada na dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134;


  1. Kuzingatia viwango vya ukomo wa bajeti vitakavyotolewa na Serikali;


  1. Kushirikisha kikamilifu Kamati za Bajeti za kila Fungu katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti ili kuwepo kwa mipango na utekelezaji shirikishi katika Mafungu kama ilivyobainishwa katika Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za Mwaka 2015;


  1. Kutumia Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo (NPMIS) katika kuandaa na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 5 wa mwaka 2020/21; na


  1. Kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa kwa kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 3 wa mwaka 2019.


  1. Utekelezaji


  1. Kuhakikisha mapato yote katika Wizara na Taasisi za Umma yanaendelea kukusanywa kupitia Mfumo wa Government e-Payment Gateway (GePG);


  1. Kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 6 wa mwaka 2020 unaoelezea Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Msamaha wa Kodi ya Ongozeko la Thamani (VAT) katika Ununuzi wa Bidhaa au Huduma Katika Miradi inayotekelezwa kwa Fedha za Serikali na za Washirika wa Maendeleo;


  1. Kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Hazina Na. 2 wa Mwaka 2019 unaoelekeza utaratibu wa kuomba, kuhamisha, kupokea, kutumia, kuhasibu na kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya D-Fund na matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha Zinazopelekwa Moja kwa Moja kwenye Miradi;


  1. Kuhakikisha ununuzi wa umma unafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 na Kanuni zake kwa kufanya ununuzi wa pamoja na kutumia Mwongozo wa Matumizi ya Force Account wa Mei 2020 ili kupata thamani halisi ya fedha;


  1. Kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (TANePS) katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi;


  1. Kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanaingia Mkataba wa Utendaji Kazi pamoja na kuwasilisha utekelezaji wa Mikataba kila robo mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina;


  1. Kuepuka uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni kwa kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 3 wa mwaka 2019; na


  1. Kuhakikisha Wizara na Taasisi za Umma zinatumia Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE) kwa ajili ya malipo na shughuli za kihasibu kwa kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 5 wa mwaka 2019.


  1. Ufuatiliaji na Tathmini


  1. Kuandaa mpango kazi na mtiririko wa fedha wa utekelezaji wa bajeti kupitia mifumo ya CBMS na PlanRep;


  1. Kuandaa taarifa za utekelezaji kwa kuzingatia muundo ulioainishwa katika Sura ya Pili ya Sehemu ya Pili ya Mwongozo. Taarifa za utekelezaji za kila robo ya mwaka ziwasilishwe katika muda wa siku 30 baada ya kukamilika kwa robo ya mwaka husika. Vile vile, taarifa za utekelezaji za mwaka ziwasilishwe kabla ya tarehe 15 Oktoba kila mwaka wa fedha;


  1. Kujenga uwezo wa watumishi katika vitengo vya ufuatiliaji na tathmini na kuandaa mpango wa kurithisha watumishi wapya maarifa ili kuwa na mfumo endelevu wa ufuatiliaji;


  1. Kujenga uwezo wa wakaguzi wa ndani kufanya ukaguzi kupitia mifumo ya kielektroniki (system-based auditing) ili kuongeza ufanisi; na


  1. Kuongeza matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalam wa ndani kwenye eneo la usalama wa mifumo.


  1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu maelekezo mahsusi ya Mwongozo yanapatikana katika Sehemu ya Pili, Sura ya Kwanza na Sura ya Pili ya Kitabu cha Mwongozo.

 

  1. MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2021/22


  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) ambao ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 utakuwa ni wa kwanza katika kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya Mpango huu. Aidha, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2021/22 utajumuisha ukamilishaji wa miradi ya kipaumbele na kimkakati ambayo utekelezaji wake haukukamilika katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Maeneo ya kipaumbele pamoja na baadhi ya miradi itakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2021/22 ni kama ifuatavyo:

 

  1. Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi. Eneo hili linajumuisha miradi ambayo itajikita katika: kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kuimarisha utulivu wa uchumi; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuimarisha uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na huduma katika maeneo ya reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini, usafiri wa anga, TEHAMA, nishati, bandari na viwanja vya ndege; 


  1. Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Eneo hili linajumuisha kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa dawa kwa matumizi ya binadamu; miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana kwa wingi nchini. Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga kuboresha sekta ya utalii, huduma za fedha na bima;


  1. Kukuza Biashara: Eneo hili linajumuisha programu za kuimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimatiafa. Aidha, masoko yanayolengwa ni yale yatakayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo bidhaa zitokanazo na kilimo na viwanda;

  2. Kuchochea Maendeleo ya Watu: Eneo hili linajumuisha utekekelezaji wa miradi ambayo inajikita katika kuboresha maisha ya watu ikiwemo kuboresha elimu na mafunzo katika ngazi zote; afya na ustawi wa jamii; kinga ya jamii; huduma za maji na usafi wa mazingira; mipango miji, na nyumba na maendeleo ya makazi; na


  1. Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza ujuzi wa rasimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwemo kuwawezesha vijana kujiajiri. Vile vile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.

 

Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 utajumuisha miradi ya kielelezo inayoendelea ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa na ya haraka katika uchumi. Baadhi ya miradi hiyo ni: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge); Makaa ya Mawe - Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli kiwango cha standard gauge kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Rumakali (MW 222); Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu (Interchange) za Daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay Kaskazini; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; Kanda Maalum za Kiuchumi.

 

Kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta Binafsi katika ustawi wa kiuchumi na kijamii, Mpango utajielekeza katika kuhakikisha Sekta Binafsi nchini inashamiri. Mpango utaainisha vipaumbele vitakavyowezesha maendeleo ya Sekta Binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji. Aidha, Mpango utaainisha mikakati mbalimbali ya uwekezaji na fursa zilizopo kwa ajili ya uwekezaji kwa Sekta Binafsi.

 

 

  1. Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Maeneo ya Kipaumbele kwa mwaka 2021/22 yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Nne).

 

  1. HITIMISHO


  1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya yatawezesha uandaaji wa Mpango na Bajeti ambao utazingatiwa na Maafisa Masuuli wote wakati wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao kwa mwaka 2021/22. Kutokana na Mapendekezo haya, Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma wanaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wakati wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao kwa Mwaka 2021/22. Vile vile, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22 na kusimamia kikamilifu Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wajielekeze zaidi katika kutoa maoni, ushauri na mapendekezo  yanayohusu masuala ya Kitaifa kwa maslahi mapana ya nchi yetu ikijumuisha wananchi tunaowawakilisha. Maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge yatakuwa na mchango mkubwa katika uandaaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya nchi.


  1. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kutoa maoni na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22.


  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 


No comments:

Post a Comment