Na Allawi Kaboyo, Biharamulo
WANAFUNZI zaidi ya elfu 15 wanatarajiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Wilaya Biharamulo huku upungufu wa vyumba vya madarasa katika halmashauri hiyo ukiwa ni vyumba 64 hali inayoweza kusababisha kuwepo kwa mrundikano wa wananfunzi kwenye vyumba vya madarasa vilivyopo.
Taarifa hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Waziri za Kombo Desemba 1, mwaka huu kwenye hafla ya kupokea mchango wa wadau wa maendeleo iliyofanyika katika ofisi za mkurugenzi na kuhudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo, amesema kuwa Biharamulo inachangamoto kubwa kwenye miundombinu ya shule hasa upande wa sekondari.
Amesema kuwa halmashauri hiyo inazo shule za sekondari 20 za serikali ambazo wanafunzi hao waliofahulu elimu ya msingi wanatakiwa kupokelewa na kuongeza kuwa idadi ya wananfunzi wanaoondoka kwa maana ya kidato cha nne ni wachache ukilinganisha na wanaoingia kwa kidato cha kwanza hali inayopelekea kuwepo kwa mapungufu hayo.
Kwaupande wake mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi Mhe. Eng. Ezra Chiwelesa ambaye amekebidhi mifuko 200 ya saruji katika kuwezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa amesema kuwa, mchango huo ni wa awali kadiri muda unavyozidi kwenda ataweza kuleta michango mingi zaidi kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali.
Amesema kuwa Biharamulo itaweza kujengwa na wananbiharamulo wenyewe ambapo ametoa wito kwa jamii nzima kuliona hili kuwa ni la kwao na kuweza kushiriki kikamilifu huku akimtaka mwenyekiti mteule wa halmashauri kuwahimiza madiwani wake kuwahusisha wananchi kwenye hili ili mwakani watoto wanapoanza shule changamoto hiyo iwe imekwisha.
“Nilipokea barua kutoka kwa mkurugenzi ikiniomba kuchangia kama mdau lakini kama kiongozi, namimi kwa kuliona tatizo hili kwa umuhimu wake maana nimepita kwenye maeneo yote ya wilaya hii nimejionea hali ilivyo, ndio maana nimeamua kwa haraka kuleta hii saruji ili iweze kusaidia maana januari watoto wanatakiwa kuanza masomo.” Amesema Mhe. Chiwelesa.
Hajat Faidha Kainamula ni mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa wanawake Tanzania mkoa wa Kagera {UWT} yeye kama mdau wa maendeleo amekabidhi mifuko 100 ya saruji ambapo mifuko 50 ni kutoka kwenye kampuni yake ya SAMUDI INVESTMENT na mifuko mingine 50 ni kutoka UWT, ambaye amewataka wakina mama katika maeneo yao kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha wanawezesha ujenzi wa madarasa hayo.
Bi Kainamula ameongeza kuwa amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa miaka mingi hivyo anajua changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu ambapo ametoa wito kwa wanannchi wote wa Biharamulo kuhakikisha wananchangia madarasa hayo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo mkuu wa wilaya Biharamulo Kanal Mathias Kahabi amewashukuru wadau hao kwa mchango wao mkubwa katika halmashauri hiyo huku akimsifu mhe. Mbunge kwa namna alivyoanza kutekeleza ahadi zake kwa kipindi kifupi na kwa haraka tofauti na watu walivyodhani.
Kahabi amesema kuwa wilaya hiyo imekuwa ikishindwa kwenda mbele kutokana na kuwepo kwa wapigaji wengi na sasa hali hiyo imeanza kupotea kutokana na uwepo wa viongozi mathubuti na kuwataka watumishi kutojisahau katika utumishi wao na badala yake wajikite katika kutatua kero za wananchi.
Amesema kuwa msaada huo umekuwa chachu kubwa ya maendeleo na mfano mkubwa wa kuigwa kwa wadau wengine maana tayari mbunge kaonyesha njia hivyo na wadau wengine wanatakiwa kufata nyayo hizo ili kuweza kuibadirisha Biharamulo na kuweza kuendana na kasi iliyopo ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment