Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu
wa Rais Muungano na Mazingira wamezindua kampeni ya utunzaji mazingira kwa
kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania.
Akizindua kampeni hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu aliipongeza
Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa mikakati ya kusaidia jitihada za Serikali katika
kutunza na kuboresha mazingira kupitia kampeni hiyo ya Pendezesha Tanzania
ambayo inahamasisha umuhimu wa upandaji miti katika kutunza mazingira.
Waziri Zungu amesema kampeni ya Pendezesha Tanzania imekuja wakati muafaka
kwani inaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kupanda miti Milioni Moja na
Laki Tano kwa kila Halmashauri kwa mwaka ili kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa
Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.
“Niipongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuwahamasisha
watanzania kutunza mazingira yao yaliyowazunguuka. Niwaahidi Serikali itaendelea
kuunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuboresha na kuyatunza
mazingira yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri Zungu huku
akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano Benki ya CRDB katika kuweka kipaumbele
suala la utunzaji wa mazingira.
Katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya
Goba, Waziri Zungu aliiteua Benki ya CRDB kuwa balozi wa mazingira. “Benki ya
CRDB mmeonyesha kujitoa sana katika kuhamasisha watanzania kutunza
mazingira. Kuanzia leo hii nimewatea rasmi kuwa mabalozi wetu wa mazingira.
Naomba Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki uhakikishe wanapata cheti cha
ubalozi ili waendelee kuwatumikia watanzania kwa kujitoa Zaidi,” alisema Waziri
Zungu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge aliishukuru Benki ya
CRDB kwa kuzindua kampeni ya Pendezesha Tanzania katika mkoa wa Dar es
Salaam. Kunenge aliwataka wananchi wa mkoa huo kupanda mti mmoja kila mtu
katika makazi yao kama sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo. “Asanteni sana Benki
ya CRDB kwa kutupa heshima wakazi wa Dar es Salaam ya kutupendezeshea jiji
letu. Niwaahidi kuwa tutashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema
Kunenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela
alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya benki hiyo kusaidia
shughuli za maendeleo katika jamii ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida kila
mwaka kusaidia nyanja za elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
“Lengo la kuzindua kampeni hii ni kuendelea kuihamasisha jamii kuona jukumu la
kupanda miti ni la jamii nzima. Tumeanza kwa kupanda miti 2000 katika shule zote
za msingi na za sekondari zilizo katika Kata ya Goba kwa lengo la kuzifanya shule
hizi kuwa na mazingira bora na rafiki kwa watoto kusoma,” alisema Nsekela.
Kampeni ya Pendezesha Tanzania inatarajiwa kufanyika nchi nzima ili kusaidia
kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupanda na kutunza miti katika kukabiliana
na mabadiliko ya tabia nchi. “Tumeanza Dar es Salaam katika shule hizi zilizopo
katika kata ya Goba, lakini lengo letu ni kufika katika wilaya na vijiji vyote Tanzania,”
aliongezea Nsekela.
Sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania, Benki ya CRDB pia
imetoa msaada wa pampu za maji kwa shule za Sekondari za Fahari, Goba na
Kinzudi ili kusaidia kuboresha upatikanaji wa maji katika shule hizo.
Akizungumza juu mikakati ya biashara inayozingatia mazingira, Nsekela alisema
Benki ya CRDB imejiwekea mfumo wa biashara ambao unazingatia utunzaji wa
mazingira ikiwamo kuweka sera inayoelekeza utoaji wa mikopo kwa miradi
inayozingatia utunzaji wa mazingira, kuanzisha huduma na bidhaa za kidijitali,
pamoja na kuwekeza katika mifumo ya ufanyaji kazi inayopunguza matumizi ya
karatasi.
Afisa elimu Kata ya Goba, Edward Shilamba aliishukuru Benki ya CRDB kwa
kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti katika shule za Sekondari na Msingi kata
ya Goba. Afisa elimu huyo alimhakikishia Waziri wa Mazingira kuwa wataweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha miti hiyo inastawi kama inavyotarajiwa.
Kutokana na jitihada za kusaidia utunzaji mazingira mpaka, mwaka jana Benki ya
CRDB ilikuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuweza
kutambuliwa na kupata usahili katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshugulikia
masuala ya Tabia Nchi “United Nations Green Climate Fund (GCF)”. Kupitia
usahili huu, Benki ya CRDB sasa inaweza kushiriki katika kuwezesha miradi
mikubwa ambayo ni rafiki wa mazingira, kwa kutoa mikopo ya hadi dola za
kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.
No comments:
Post a Comment