Na OWM, DAR ES SALAAM
OFISI ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji imekutana na wadau wa uwekezaji wa sekta Binafsi kwa lengo la kuijadili rasimu ya taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996. Wadau hao kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Baada ya kupokea rasimu ya taarifa hiyo,wameridhishwa kwa jinsi serikali imekuwa ikiishirikisha sekta binafsi katika masuala ya uwekezaji nchini.
Akiongea wakati wa kufungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Uwekezaji) Dorothy Mwaluko, Mkurugenzi Idara ya Mipango na Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, Packshard Mkongwa amewahakikishia wadau wa Sekta Binafsi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kukuza uwekezaji na biashara nchini.
“Serikali imekuwa ikitekeleza sera za mageuzi ya uchumi kuanzia miaka ya 1980 kwa lengo la kuimarisha na kuiwezesha sekta binafsi kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi. Ili kutimiza azma hii, Serikali imekuwa ikitunga Sera na Sheria kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya kukuza uwekezaji na biashara nchini. Kwa mantiki hii tunakutana na nyie sekta binafsi ili muweze kutoa maoni yenu kuhusu rasimu ya taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996” Amesisitiza Mkongwa.
Ameongeza kuwa ili kuiwezesha Sekta Binafsi kuwa yenye nguvu na ushindani nchini amewataka wadau hao kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwenye nyanja za Uratibu wa Masuala ya Uwekezaji, Utangazaji wa Fursa za Uwekezaji na Uwezeshaji Uwekezaji. Moja ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Sera hiyo ni pamoja na Tanzania kufikia lengo la kuwa na Uchumi wa kipato cha Kati, Ukuaji wa Uchumi usioteteleka na kudhibiti mfumuko wa bei.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Zachy Mbenna akielezea maoni ya wadau na amefafanua kuwa mkutano huo wa kuijadili rasimu ya taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 ni muendelezo wa juhudi za serikali katika kuweka mazingira bora na wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini.
“Sisi wadau wa sekta Binafsi tungependa Sera ya Taifa ya Uwekezaji iwe kwenye mtazamo wa Kuhamasisha uwekezaji, kwa maneno, utekelezaji wake pamoja na sheria zinazo husiana na masuala ya uwekezaji zioneshe zinalenga kuhamasisha uwekezaji wa hapa nchini, kikanda na kimataifa. Sawa tunatengeneza Sera ya Uwekezaji ya Tanzania lakini lazima iwe imezingatia masuala yanayohusu uwekezaji ya kikanda na kimataifa” Ameeleza Mbenna.
Mtaalamu wa Utafiti wa masuala ya sheria ya uwekezaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Saudin Mwakaje akisisitiza umuhimu wa wadau wa Sekta Binafsi kuijadili rasimu ya taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sera hiyo 21 Septemba 2020, Dar es Salaam, mkutano huo umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya maendeleo ya Sekta Binafsi kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Aidha, ameeleza kuwa Sera ya Uwekezaji haina budi kuangalia namna ya kutoa mwongozo wa kuwafanya wawekezaji wa ndani na nje wanao wekeza nchini juu ya namna wanaweza kuhimili majanga endapo yanatokea na kuweza kuathiri shughuli za uwekezaji. Mfano mzuri wa ugonjwa wa homa ya COVID-19 ulivyo athiri shughuli zao za uwekezaji. Amesisitiza pia kuwa ni vyema kuwa sera ikazingatia kuwa inawezesha kutumika kuchagiza maendeleo ya ukuaji wa uchumi nchini.
Mbenna amefafanua kuwa wangependa sheria za kisekta kwenye masuala ya uwekezaji na Biashara ioneshe namna zinavyounga mkono sheria mama ya uwekezaji. Pia tusiruhusu jitihada zinazo kinzana katika kuendeleza uwekezaji bali ziwe na uwiano mzuri, vile vile amesema katika uwiano huo, Sera za Zanzibar na Tanzania bara hazina budi kuzingatia hilo. Pia amebainisha kuwa Sera ni vyema itambue makundi yanayoibuka kama vijana yanaweza kuchukua nafasi katika masula ya uwekezaji.
Sera ya Taifa ya Uwekezaji imebainisha malengo mahsusi sita (6) na malengo nane (8) ya kisekta. Baadhi ya malengo hayo ni kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa kwa ajili ya mauzo ya nje; Kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi; Kuhimiza na kuvutia matumizi ya teknolojia za kisasa katika uwekezaji; Kuweka mfumo mzuri na wa wazi wa kisheria; na kuondoa urasimu katika taratibu za upatikanaji wa vibali vya uwekezaji.
Mkutano huo uliowashirikisha wadau wa sekta binafsi ni wa pili baada ya ule wa kwanza uliofanyika tarehe 11 Septemba, 2020 jijini Dodoma ambao ulihusisha wadau wa sekta ya umma kwa maana ya Wizara na Taasisi za Serikali. Mkutano huo umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
No comments:
Post a Comment