Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar imefanikiwa kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii kutokana na jitihada na uwezo wa Viongozi na wananchi wake.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi kwa mwaka 2019/2020 na Mpango kazi wa mwaka 2020/2021.
Alisema maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliopatikana katika sekta mbali mbali, ikiwemo miundombinu na Usafirishaji, upandishaji wa mishahara mara tano katika kipindi cha Uongozi wake (miaka kumi), ongezeko la Pencheni na mambo mengine kadhaa yanatokana na juhudi za Serikali.
Alisema mafanikio hayo yamewezesha kupungua kwa utegemezi wa Bajeti ya serikali kwa asilimia tano hivi sasa.
Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Ofisi hiyo kuandaa utaratibu wa kuwa na mipango ya mafunzo kwa watumishi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya Wizara husika na Serikali kwa ujumla na kubainisha kuwa hiyo ndio kazi ya Utumishi wa Umma.
Aliwakumbusha viongozi na watendaji hao kuwa Ofisi hiyo ni ya heshima, hivyo ni vyema pale wanapohitaji kuwaandikia barua watumishi kwa dhamira ya kubainisha muda wao wa kustaafu, wakazingatia lugha nzuri ikiwa hatua ya kuthamin mchango waliotowa katika kipindi kirefu cha utumishi wao.
Aidha, aliuagiza uongozi wa Ofisi hiyo kuweka kumbu kumbu za muhtasari wa ongezeko la mshahara na ulipaji wa posho katika mashirika ya serikali na kusisitiza wajibu wa Waziri kuwa ndie mwenye mamlaka ya kuidhinisha kiwango cha malipo hayo baada ya kupendekezwa na Bodi.
Alisema pamoja na mipango ya chuo Cha Utumishi wa Umma kuwa na azma ya kuendesha mafunzo ya Uongozi , kinapaswa kuwa na mwelekeo wa mbali zaidi utakaolenga kukiimarisha na kukifanyia upanuzi, kama vile ujenzi wa Hosteli kupitia mihula tofauti (robo mwaka, nusu mwaka au mwaka mzima).
Dk. Shein aliupongeza Uongozi, watendaji na wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi zao pamoja na maandalizi na uwasilishaji mzuri wa taarifa ya Utekelezaji wa mpango kazi, sambamba na kuwataka kuendelea kujitahidi katika kujenga uwezo ili kutekeleza vyema wajibu wao, akibainisha Zanzibar inahitaji kujengwa na watu wote.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana na Ofisi hiyo, kutokana na kuwepo kwa Uongozi bora, kuna dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa ni vigumu kwa mwananchi kupata ajira Serikalini hadi apate msukumo, huku taarifa zaidi zikihusisha baadhi ya watendaji kuuza ajira hizo.
Aliitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA) kuendleea kufanya kazi zake kwa umakini na weledi mkubwa ili kukabiliana na tatizo la Rushwa, akibainisha Serikali zote mbili (SMZ na SMT) zimekuwa zikipiga vita suala hilo.
Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwapongeza Vongozi, watendaji na wafanyakazi wa Ofisi hiyo kwa mashirikiano yao yaliowawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.
Alisema ni vyema Ofisi hiyo ikaendeleza utaratibu wa kutayarishaji taarifa ya utekelezaji wa Mpango kazi (bango Kitita), kwani ni nyenzo muhimu katika kutathmin mafanikio na changamoto zinazojitokeza pamoja na kubadilishana mawazo.
“Kuelekea kipindi hiki cha Uchaguzi mkuu, ni vyema kuhakikisha kunakuwepo udhibiti wa mali za Serikali , Serikali ipo na katika kipindi hiki inazuia kabisa uuzaji wa mali zake”, alisema.
Mapema, Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alimpongeza Rais Dk. Shein kwa busara na uadilifu mkubwa katika uongozi wake, hivyo kujenga uwazi wa Ofisi hiyo, na kusema pamoja na mambo mengine alifanikiwa kurekebisha mishahara ya wafanyakazi wa serikali mara kadhaa.
Alisema katika kipindi hicho Ofisi hiyo ilifanikiwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa mambo mbali mbali, ikiwemo kuratibu na kuendesha mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi 550 wa Wizara, Mashirika ya Umma pamoja na taasisi mbali mbali zinazojitegeemea.
Alisema Ofisi hiyo ilikamilisha zoezi la uhakiki wa malipo ya mshahra na Posho kwa Wizara 13 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Idara pamoja na taasisi mbali mbali.
Aidha, alisema Ofisi ilitangaza nafasi za Ajira 5,083 katika Utumishi wa Umma Unguja na Pemba pamoja na kuanzisha Wakala wa Serikali Mtandao.
Alieleza kuwa Ofisi hiyo pia ilifanya mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011 na kuanda mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, sambamba na kukamilisha utafiti kuhusu tathmin juu ya Uwajibikaji wa Watumishi wa Umma.
“Ofisi iliingiza taarifa za awali za Viongozi katika mfumo wa Kielektronik wa kusajili taarifa za mali na madeni ya Viongozi”, alisema.
Nae, Mshauri wa Rais Pemba, Dk. Maua Abeid Daftar alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuanzisha sheria ya Utawala bora,hatua iliyolifanya Taifa kuwa na amani na Utulivu, hususan katika kipindi kama hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Aliipongeza Serikali kwa kusimamia vyema upatikanaji wa ajira kwa vijana, na kutoa rai kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za haraka pale litakapojitokea tukio la kiongozi wa Serikali kuuza ajira.
No comments:
Post a Comment