UFAFANUZI WA TCRA JUU YA UMILIKI WA LAINI ZA SIMU ZAIDI YA MOJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 2 July 2020

UFAFANUZI WA TCRA JUU YA UMILIKI WA LAINI ZA SIMU ZAIDI YA MOJA


UFAFANUZI JUU YA UTEKELEZAJI WA ZOEZI LA KURASIMISHA UMILIKI
WA LAINI ZA SIMU ZAIDI YA MOJA KATIKA MTANDAO MMOJA

1.0 UTANGULIZI

Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Usajili wa Laini za Simu) za mwaka 2020, yaani “The Electronic and Postal Communications (SIM Card Registration) Regulations, 2020”, zimeainisha katika Kanuni ya 18 kuwa:-
18 (1) Mtu anayehitaji kumiliki na kutumia laini ya simu ataruhusiwa kusajili:-

(a) Kama ni mtu binafsi

i. Idadi ya laini moja kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe mfupi pamoja na
matumizi ya data;

ii. Idadi ya laini zisizozidi nne kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na mashine; na

(b) Kama ni Kampuni au Taasisi

i. Idadi ya laini zisizozidi thelathini kwa kila mtoa huduma za
mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe
mfupi pamoja na matumizi ya data;

ii. Idadi ya laini zisizozidi hamsini kwa kila mtoa huduma za
mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na
mashine.

(2) Laini zilizosajiliwa kwa matumizi yaliyoainishwa kwenye Kanuni 18 (1) (a) hazipaswi kutumiwa kwa kubadilishana (interchangebly).

(3) Bila kujali Kanuni ya 18 (1), Mtu binafsi, Kampuni au Taasisi inaweza kuruhusiwa kusajili na kumiliki laini zaidi ya zilizoainishwa kwa kuomba na kupata idhini kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (4) Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya Kanuni hizi, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kuutaarifu umma kwamba zoezi la kuomba idhini ya umiliki wa laini za simu zaidi ya moja katika mtandao mmoja linaendelea. Tunawashauri wamiliki wa laini za mawasiliano ya simu kuendelea kuhakiki usajili wa laini zao zote wanazomiliki.

2.0 KUTHIBITISHA IDADI YA LAINI ZILIZOSAJILIWA KUTUMIA KITAMBULISHO CHA TAIFA (NIDA)

2.1 Kila mmiliki wa laini ya simu anatakiwa kupiga namba *106# na kuangalia usajili wa laini anazomiliki na endapo atakuta namba
ambayo haitambui na imesajiliwa kwa kutumia namba ya
kitambulisho chake cha Taifa anashauriwa kuwasiliana na mtoa
huduma wake ili azifunge mara moja kuepusha matumizi mabaya na kumsababishia usumbufu usiokuwa wa lazima utakaojitokeza.

2.2 Kwa wale ambao kwa sasa wanamiliki laini zaidi ya moja katika mtandao mmoja, mwisho wa kuhakiki laini zao itakuwa tarehe 31 Julai 2020.

2.3 Utaratibu wa kuomba idhini ya kumiliki laini mpya za ziada katika mtandao mmoja unaendelea na mteja anaweza kupata huduma hii kupitia kwa wakala au kwenye ofisi za watoa huduma ambapo kwa kutumia njia za kielektroniki mtoa huduma atawasilisha maombi ya mteja wake TCRA kwa idhini ya kusajili na kumiliki laini za ziada; mteja atapokea majibu ya maombi yake ndani ya takribani dakika tano.

3.0 URASIMISHAJI WA LAINI ULIZOTHIBITISHA

3.1 Urasimishaji wa laini za ziada kwa sasa unaweza kufanyika kwa wakala au kwenye ofisi za watoa huduma ambapo kwa kutumia njia za kielektroniki ambapo mtoa huduma atawasilisha maombi yake ya idhini ya kurasimisha laini za ziada TCRA na kupokea majibu ndani ya takribani dakika tano; au

3.2 Kwa kupitia namba *106# ambapo wewe mwenyewe utaweza
kuomba idhini ya kurasimisha kutoka TCRA kupitia simu yako.
Huduma hii ya kurasimisha kwa njia ya simu yako itaanza kutumika rasmi Agosti 1, 2020.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Jengo la Mawasiliano, Kitalu Na. 20 Barabara ya Sam Nujoma,
S. L.P 474, 14414 DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment