Na Allawi Kaboyo, Missenyi
WAKATI Tanzania ikielekea katika uchaguzio mkuu mwezi octoba mwaka huu utakaohusisha kuwachagua madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania huku zoezi hilo likitanguliwa na kampeni kwa wagombea wakinadi sera na ilani za vyama vyao, wananchi wameaswa kutokukubali kutumika na wanansiasa na kupelekea kuwepo uvunjifu wa Amani.
Wito huo umetolewa na Rais wa shirika la elimu ya Amani Tanzania Wilison George wakati wa ziara yake julai 01, mwaka huu mkoani Kagera iliyolenga kulitambulisha shirika hilo kwa viongozi wa mkoa huo pamoja na wananchi alisema shirika hilo limesajiliwa na serikali kwa ajili ya kutoa elimu ya Amani nchini.
Alisema kuwa Amani iliyopo Tanzania nchi nyingi zinaililia lakini inakuwa ngumu kwao kuipata na kusisitiza kuwa watanzania wenyewe ndio wenye jukumu kubwa la kuilinda Amani na kumuona anayetaka kuivuruga Amani yao kama adui mkubwa namba moja.
Rais huyo aliyeambatana na viongozi wengine wa shirika ngazi ya Taifa, mkoa na wilaya wamefika katika ofisi za mkuu wa wilaya Missenyi na kumwambia mkuu huyo lengo la wao kufika hapo ni kulitambulisha shirika na kuomba ushirikiano wa serikali ngazi zote ili kuboresha huduma hiyo ya elimu kwa wananchi.
“Mhe. Mkuu wa wilaya dhumuni kubwa la shirika hili ni Amani, sisi ni walinzi wa Amani tunalinda Amani kwa kutoa elimu ya Amani, na tangu tumeanza kufanyakazi tumeanza na vyama vya siasa ambavyo mpaka sasa migogoro yaoi imeisha na huwezi kuwa mlinzi wa Amani alafu wewe mwenyewe ukawa sababu ya kuvunjika kwa Amani.” Alisema Rais George.
Rais Wilison alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa elimu ya Amani nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya Amani na kutambua gharama ya kuipata Amani pale inapotoweka ambapo pia alieleza kuwa mpaka sasa wamesambaa kwenye mikoa zaidi ya 22 nchi nzima.
Aliongeza kuwa wakati Tanzania inaelekea katika zoezi la uchaguzi wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wananchi kufanya vitendo vya uvunjifu wa Amani ambapo amewataka watanzania kutokubali kutumika na wanasiasa wenye nia ovu ya kuvunja Amani suala ambalo linaweza kuwapelekea wao kuumia pale vyombo vya ulinzi na usalama vitakapoamua kuikabili hali ile.
“Utofauti wetu na mashirika mengine ni kwamba sisi tunafanya kazi na vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini na hao ndio wenzetu tunaofanya nao kazi, kwahiyo tunapata ushirikiano mkubwa kutoka kwenye vyombo hivyo na lengo letu tunahitaji tuwafikie watanzania wote waelewe umuhimu wa Amani, tunatamani siku moja polisi akae kituoni siku nzima asipatikane mwalifu, tunataka kwenye magereza yetu watu wanapungua hadi kuisha kabisa kwa kutojishughulisha na uhalifu.” Alidadavua Rais huyo.
Kwaupande wake Mkuu wa Wilaya Missenyi Kanal Denisi Mwila alilishukuru shirika hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhubiri Amani ambapo aliahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi hao wakati wowote watakapohitaji uwepo wake.
Kanali Denis alisema kuwa uwepo shirika hilo hapa nchini kutawasaidia viongozi hao katika kupambana na uhalifu kwakuwa wananchi watakuwa na uelewa mkubwa wa vitu vinavyosababisha kuwepo uvunjifu wa Amani na kulitaka shirika hilo kujenga matawi kwenye vijiji ambako ndiko kuna watu wengi, hasa katika wilaya yake ambayo ipo mpakani ambapo pia alitoa historia kubwa ya mashujaa waliomwaga damu kwaajili ya Tanzania na Kagera na kuwafanya sasa wanankagera wanaishi bila kubugudhiwa.
“Wilaya yetu hii ya Missenyi ni wilaya ambayo ipo mpakani ikipakana nan chi jirani ya Uganda kwa maeneo mbalimbali, changamoto ambayo ilikuwa kubwa katika wilaya hii ni pamoja na wimbi la uhamiaji haramu, uingizwaji holela wa mifugo kutoka nje ya nchi ambapo tumeweza kuthibiti hali hiyo kwa nguvu kubwa, kwa mantiki hiyo nalishukuru shirika hili kufika hapa kwetu ninaimaani litatusaidia kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu suala zima la kuilinda Amani mkizingatia sisi huku tupo mipakani hivyo suala la kutoa elimu ya amni ni suala muhimu sana.” Alisema Kanali Mwila.
Sambamba na ziara hiyo shirika hilo pia lilitoa msaada wa vifaa kinga vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona katika shule ya secondary Bunazi iliyopo wilayani Missenyi ambapo walitoa sabuni za kuanawia mikono, vitakasa mikono pamoja vifaa vya kuwekea maji ya kunawa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na ugonjwa huu hasa kwa watoto wa shule ambao kwasasa wameanza masomo baada ya kukaa nyumbani kwa miezi kadhaa.
Akiongea mara baada ya kupokea vifaa hivyo Kaimu Mganga Mkuu Bi. Justina Mugabe amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambapo amesema kuwa msaada huo utaweza kuwasaidi wanafunzi kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 na kuyata mashirika mengine kuliiga shirika hili kwa kuendelea kuwapa misaada hiyo maana licha ya ugonjwa kupungua hapa nchini lakini bado wanahitaji kuendelea kujikinga.
Ziara hiyo iliendelea wilayani Missenyi hadi katika mpaka wa Tanzania na Uganda Mutukula ambapo shirika hilo liliweza kujitambulisha kwenye kituo cha pamoja cha forodha kilichopo mpakani hapo ambapo viongozi wa taasisi zilizopo kituoni hapo walielezwa uwepo wa shirika hilo na kuomba kutoa ushirikiano pale watakapoanza kutoa elimu kwao na wateja wao.
Akiongea kwaniaba ya wakuu wa taasisi nyingine, Kaimu Afisa Mfawidhi Kastamu Mutukula, Bw. Zawadi Mlingwa alisema kuwa ili nchi iwe na maendeleo lazima wananchi walipe kodi na kutokana na kwamba shirika linajihusisha na utoaji wa elimu ya Amani ambapo ameeleza kuwa wataweza kukusanya kodi endapo Amani itaendelea kutawala na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi hapo pale watakapoanza shuguliza za kuwaelimsha wananchi.
“Sisi hapo tupo kwaajili ya kumsaidia Mhe. Rasi Magufuli kukusanya kodi hivyo suala la Amani ni nguzo kubwa na muhimu sana kwetu ukizingatia tupo mpakani, nchi ikiwa na mani kodi italipwa na wananchi watapata maendeleo hivyo sisi kama wadau na taasisi nyingine ambazo tunatoa huduma hapa katika kituo hiki cha pamoja tutatoa ushirikiano mkubwa wa kuhakikisha elimu hii inawafikia watu wengi na hapa hatuwahudumii watanznia peke yao tunakutana na watu wengi sana hivyo Amani ni muhimu sana kwetu.” Alisema Bw. Zawadi.
Shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2018 likiwa na muasisi mmoja nna baadae wanachama 14, mpaka sasa lina wanachama Zaidi ya laki sita nchi nzima ambapo linatoa wito kwa watanzania kujiunga kwenye shirika hilo na kueleza kuwa mpaka sasa limeanza kusambaa katika nchi za Afrika mashariki na Kati na lengo lao ni kuzifikia nchi zote za Afrika na dunia kwa ujumla.
Aidha shirika limetoa utaratibu wa kujiunga nalo kuwa anaruhusiwa mtu yeyote kujiunga kwa kujaza fomu ambayo ataipata kwa shilingi elfu 2000/= na kulipia ada ya shilingi elfu sita ambapo atapatiwa kadi ya uanachama pamoja na kitambulisho na kuanza kupewa mafunzo ya ulinzi wa Amani.
No comments:
Post a Comment