SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA MAJINI-WAZIRI MKUU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 7 July 2020

SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA MAJINI-WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Mtwara Julai 7, 2020. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na katikati ni Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  Julai  7, 2020 amekagua  kazi ya upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Mtwara. Pichani ni   kazi za upanuzi na uboreshaji wa bandari hiyo.

Eneo la bandari ya Mtwara linalopanuliwa  katika maboresho yanayofanywa na serikali ili kukuza uwezo wa bandari hiyo. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua upanuzi huo Julai 7, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema malengo ya Serikali ni kuimarisha usafiri kwenye maziwa yote na bahari ili kuwawezesha Watanzania wafanye biashara na mataifa ya nje.

“Malengo yetu ni kuruhusu mataifa ya nje yafanye biashara na Tanzania na  kuruhusu Watanzania wasafiri kwenda hukohuko kuona na kujifunza ili warudi hapa na taaluma mpya. Utaratibu huo pia utawezesha kutengeneza mzunguko mzuri wa kifedha kwa wananchi,” amesema.

Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Klabu ya Bandari mjini Mtwara Julai 7, 2020)Waziri Mkuu amesema  kabla ya kukagua ujenzi wa gati namba 2 katika bandari ya Mtwara juzi alitembelea miradi ya ujenzi wa bandari za Karema (Katavi), Kabwe na Kasanga (Rukwa) katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

“Nimetoka Ziwa Tanganyika ambako tunapakana na Burundi, Rwanda, Zambia na Congo na Serikali kwenye mkakati huu tumeingiza fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa bandari zetu. Tumeimarisha bandari ya Kigoma pale Kibirizi, kazi imekamilika na sasa tunajenga eneo la kuweka makontena.”

Amesema katika Ziwa Victoria kuna meli iliyokuwa inakarabatiwa na imeanza majaribio ya kwenda Kagera na nyingine inaendelea kujengwa ili kuruhusu wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa wafanye biashara zao kwa urahisi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka vijana wanaopata ajira kwenye miradi mikubwa inayogharimiwa na Serikali watumie fursa hiyo kupata utaalamu utakaowawezesha kuajiriwa maeneo mengine hata baada ya miradi ya sasa kukamilika

Akizungumza na vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi kwenye mradi wa gati jipya katika bandari ya Mtwara leo mchana, Waziri Mkuu amewataka vijana wote wanaofanya kazi kwenye miradi mbalimbali nchini hasa ile mikubwa na ya kimkakati wawe waaminifu ili kujenga taswira nzuri  ya nguvukazi ya vijana wa Kitanzania wanapohitaji kuajiriwa hasa na makampuni ya nje ya nchi.

“Kuweni mabalozi wazuri wa vijana wenzenu kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu wa hali ya juu ili mkimaliza miradi ya sasa, mpate ajira tena kwenye miradi mingine. Bado Serikali yetu inakusudia kuanzisha miradi mingine mingi  na matarajio ni kuwa vijana wa Kitanzania watanufaika kwa kupata ajira katika miradi hiyo.”
  
Awali, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara alimweleza Waziri Mkuu kuwa kazi ya ujenzi wa gati namba 2 katika bandari ya Mtwara unafanywa na kampuni ya MS China Railway Construction Enginereering Group Company Limited (CRMBEG) kwa gharama ya sh. 157,801,598,519.92.00

Amesema ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi Mei 27, 2017 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai, 2020 ukisimamiwa na Mhandisi Mwelekezi, Inros Lackner kutoka Ujerumani.

Mhandisi Kijavara alisema kuwa  mradi huo umefikia  asilimia 75 ya utekelezaji wake na jumla ya sh. bilioni 74.84 zimelipwa kwa mkandarasi sawa na asilimia 48.

Akizungumzia ushiriki wa wazawa katika ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Kijava alisema kuwa mkandarasi huyo ameajiri wazawa 308 sawa na asilimia 87.5 ya wafanyakazi wote. Alisema wafanyakazi hao wameajiriwa katika  kada mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliafuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara.

No comments:

Post a Comment