NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kuwa mbegu bora za mazao ziuzwe kwa bei nafuu ili wakulima wamudu gharama na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Alitoa agizo hilo wakati wa mkutano wa ufunguzi wa mafunzo ya wakulima kuhusu udhibiti wa Sumukuvu katika kijiji cha Engusero Wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara. Mafunzo yanayoratibiwa na mradi wa kudhibiti sumukuvu (TANIPAC) chini ya wizara Kilimo.
Katika uzinduzi huo, Naibu Waziri Bashe alipokea malalamiko ya wakulima wa zao la mahindi na alizeti kuhusu bei kubwa ya mbegu. Malalamiko hayo yalitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bw. Tamimu Kambona
Kambona alidai kuwa wakulima wa Kiteto wananunua kilo moja ya mbegu ya mahindi kwa shilingi 8000 na alizeti shilingi 35,000 hali inayofanya washindwe kumudu gharama na wakati mazao hayo yanalimwa kwa wingi Kiteto hivyo kuiomba wizara ya Kilimo ianzishe kituo cha uzalishaji mbegu bora Kiteto.
“Changamoto yetu Kiteto ni upatikanaji wa mbegu za mahindi na alizeti. Kilo mboja ya mbegu ya alizeti inauzwa shilingi 35,000 wakati mkulima anauza kilo moja ya alizeti shingi 1,700 wakati wa mavuno na mbegu ya mahindi sasa inauzwa shilingi 8,000 wakati sasa mahindi hapa tunauza kwa bei shilingi 400-500 kwa kilo” alisema Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
Akijibu malalamiko hayo, Naibu Waziri Bashe aliwasiliana kwa simu katikati ya mkutano huo na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya mbegu (ASA) Dkt.Sophia Kashenge na kumwelekeza kuwa kuanzia msimu ujao wa kilimo ASA wafungue Kituo cha kuzalisha mbegu bora Wilaya ya Kiteto.
Aidha Bashe aliagiza ASA wauze mbegu za mahindi kwa bei ya Tsh 2,750 kwa kilo badala ya Tsh 8,000 na kwa alizeti wauze Tsh 6,000 kwa kilo badala ya Tsh 35,000. Kampuni hiyo ya umma kupitia Mtendaji Mkuu wake ilikubali maelekezo hayo kuwa itayatekeleza ili wakulima waweze kupata mbegu bora kwa gharama nafuu.
Katika hatua nyingine Bashe alimwelekeza Mtendaji Mkuu wa NFRA Milton Luppa kwenda Kiteto kuanzia wiki ijayo ili waanze kununua mahindi kwa wakulima ambao sasa wanauza kwa bei ndogo ya Tsh.500 kwa kilo hivyo kuwa na malalamiko.
“Kuanzia wiki ijayo NFRA watafika Kiteto kuanza kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya kuanzia Tsh.600 kwa kilo ili gunia moja la kilo 100 liuzwe kwa shilingi 60,000 badala ya sasa Tsh. 500,000,” alisisitiza Bashe.
Bashe alisema kwa mujibu wa taarifa ya za halmashauri ya wilaya ya Kiteto katika msimu huu wa Kilimo inatarajia kuzalisha tani 270,000 za mahindi kutoka tani 160,000 za mwaka 2019/20 hivyo uwepo wa mradi wa udhibiti sumukuvu utaweza kusaidia uhifadhi bora wa mahindi ili yasiharibiwe na fangasi wa sumukuvu kwa njia ya utoaji elimu na ujenzi wa maghala bora.
Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa uamuzi huo umelenga kuwasaidia wakulima kunufaika na jasho lao kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuwa Wizara ya Kilimo ihakikishe kero na vikwazo kwa wakulima zinatatuliwa haraka.
“Sisi kama serikali tumelenga kuwalinda wakulima kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika wa masoko kwa mazao yao pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeelekeza serikali kuhakikisha inapunguza gharama za uzalishaji mazao kwa wakulima nchini” alisisitiza Naibu Waziri Bashe
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kiteto Emanuel Papian aliishukuru serikali kwa niaba ya wakulima kwa uamuzi wake wa kufungua kituo cha uzalishaji mbegu kwenye wilaya ya Kiteto hali itakayosaidia upatikanaji mbegu kwa gharama nafuu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Engusero Robert Mtyamburi alisema wananchi wa Kiteto wamefurahishwa na uamuzi wa serikali kuelekeza mbegu kuuzwa kwa gharama ya chini hali itakayokuza uzalishaji mazao ya mahindi na alizeti.
Mwenyekiti huyo aliongeza kusema Kiteto ni wilaya muhimu kwa Kilimo kwani eneo lake lote linafaa kwa uzalishaji mazao hivyo ameiomba serikali itazame suala la upatikanaji mbolea na viuadudu kwa bei nafuu zaidi ili wakulima wapate uchumi mzuri na kuepuka kuibiwa na walanguzi.
No comments:
Post a Comment