WANANCHI MAHEMBE WASHIRIKI UJENZI WA HOSPITALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 7 July 2020

WANANCHI MAHEMBE WASHIRIKI UJENZI WA HOSPITALI

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Simon Chacha akichimba Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma inayojengwa kwenye Kata ya Mahembe.

Wakazi wa Kata ya Mahembe wakishiriki kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.

Mwandishi Wetu, Kigoma

SERIKALI imeanza Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ili kukabiliana na changamoto ya wananchi wa Wilaya hiyo ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za Afya.

Katika kuhakikisha matokeo chanya, Wananchi wa Kata ya Mahembe inapojengwa Hospitali hiyo, wamejitokeza kuchangia nguvu zao katika shughuli ya Uchimbaji wa Msingi  wa Jengo ambalo baada ya kukamilika kwake litawaondolea adha ya kutembea takribani Kilometa nane kufuata huduma za Afya.

Akizungumza wakati wa kuanza kwa ujenzi wa Msingi wa Hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. SIMON CHACHA  amesema mradi huo utagharimu shilingi  bilioni moja na milioni mia tano hadi kukamilika kwake.

Dkt. Chacha amesema ujenzi wa Hospitali hiyo umepangwa kukamilika  mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti,  baadhi ya wakazi wa Mahembe wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea maendeleo hatua ambayo haikuwahi kufikiwa kwa miaka mingi iliyopita.

"Muda tuliokuwa tukiutumia kwenda umbali mrefu kutafuta tiba au kupeleka huduma mbali, tutautumia kuendeleza shughuli zetu za kiuchumi" walisema. 

Aidha, wameipongeza Serikali kwa kufikia Uchumi wa kati kabla ya muda uliopangwa huku wakionesha matumaini makubwa ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Pendo Mangalia amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma katika maeneo ya karibu na kuwaondoa na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.

Amesema wananchi wamehamasika na kuchangia nguvu zao kuhakikisha maendeleo yanapatikana. Kukamilika kwa  ujenzi wa hospitalii hiyo katika eneo la Mahembe kunafanya kuwa na Hospitali Tano za Wilaya Mkoani Kigoma.  

No comments:

Post a Comment