NBTS MTWARA YAFIKIA ASILIMIA 94 UKUSANYAJI DAMU SALAMA KWA WIKI MBILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 11 June 2020

NBTS MTWARA YAFIKIA ASILIMIA 94 UKUSANYAJI DAMU SALAMA KWA WIKI MBILI


Afisa Viwango na Ubora NBTS Kanda ya Kusini, Charles Mwiyumo akionesha jinsi wanavyolebo mazao ya damu baada ya mfumo kuthibitisha ni salama.

Na WAMJW, Mtwara

MPANGO wa Taifa wa damu Salama (NBTS), Kanda ya kusini, umefikia asilimia zaidi ya 94 ya ukusanyaji wa damu salama  sawa na chupa 374 katika wiki ya kuadhimisha siku ya wachangia damu duniani. 

Hayo yamesemwa leo na Meneja wa mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Kusini iliyopo mtwara Dkt. Pendael Sifuel  wakati akizungumza kuhusu wiki ya maadhimisho hayo ambayo duniani hufanyika Juni 14 kila mwaka.

“Kanda yetu tulikuwa na  lengo la  kukusanya chupa 400 kwa wiki mbili za uhamasishaji na tayari tumekusanya chupa 374  sawa na asilimia 94, hii ni kutokana na lengo la kukusanya chupa 45 hadi 50 kwa siku, hadi siku tano zilizobaki tutaweza kufikia malengo na hata kuvuka”. Amesema.

Dkt. Sifuel amesema kwamba kanda yake imeweka mkakati wa kukusanya damu kutoka vijijini kutokana na eneo la mikoa husika ni dogo na halina vyuo vingi  hivyo wamepeleka elimu zaidi ya uchangiaji damu kwa wananchi waliopo vijijini.

“Tumewekeza sana vijijini kwani wanaopata huduma hiyo ni wananchi wenyewe na kama mnavyojua kanda yetu ina mikoa mitatu tu,hivyo kila anayefika kituo cha kutolea huduma za afya na kuongezewa damu anavyorudi nyumbani anaenda kuwa  balozi hivyo *_atatoe_* elimu kwani mgonjwa hupewa damu bila kuleta ndugu kuchangia”.

Kwa upande wa utoaji wa majibu meneja huyo amesema kuwa maabara yake tangu mwaka jana wizara ya afya kuwapatiwa mashine za kisasa za uchunguzi wa sampuli za damu umewawezesha kutoa majibu ya damu kutoka siku tatu hadi siku moja.

“Kuna wakati tunapata dharura wa uhitaji wa damu salama kwa haraka kutoka kwenye halmashauri hivyo mashine hizi zinatuwezesha kutoa majibu ndani ya saa tatu tangu kupata taarifa ya dharura na kurudisha majibu haraka kama damu tuliyopokea ni salama au la”.

Dkt. Sifuel alisema mashine hizo za kisasa  zina uwezo wa kupima sampuli zaidi ya 100 ndani ya saa moja  na ina uwezo wa kupima magonjwa kama UKIMWI, Homa ya Ini B na C pamoja na Kaswende.Mpango wa Taifa wa Damu salama kanda ya kusini inahudumia mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

No comments:

Post a Comment