NAIBU WAZIRI MABULA AKERWA NA MSHAURI ELEKEZI KUKWAMISHA MRADI WA HOSPITALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 9 June 2020

NAIBU WAZIRI MABULA AKERWA NA MSHAURI ELEKEZI KUKWAMISHA MRADI WA HOSPITALI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia baadhi ya vifaa vya ujenzi vilivyopo eneo la mradi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara alipotembelea mradi huo jana. Mradi huo unajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kulia ni Meneja wa NHC mkoa wa Mara Goodluck Thomas.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Msanifu wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara Msafiri Msaki kuhusiana na vifaa vya ujenzi vilivyopo eneo la mradi alipotembelea mradi huo jana ambao ujenzi wake unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa na hatua ya kusimamisha ujenzi wa miundombinu kwenye mradi wa kimkakati wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo eneo la Kwangwa Manispaa ya Musoma mkoa wa Mara uliofanywa na Mshauri Elekezi wa mradi huo Kampuni ya ARU Environment Consulting Company Ltd (ABECC) .
Hatua hiyo inafuatia Dkt Mabula kuelezwa na Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Mara Goodluck Thomas kuwa, baadhi ya kazi za mradi huo zimesimama kutokana na Mshauri Elekezi kampuni ya ABECC ambayo iko chini ya Chuo Kikuu cha Ardhi kusimamisha ujenzi wa miundombinu wakati Shirika likiwa limenunua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha kazi.
Akizungumza mjini Musoma jana alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Dkt Mabula alisema haelewi ni kitu gani kilichomsukuma Mshauri Elekeza kukwamisha ujenzi wa hospitali hiyo unaogharimu bilioni 15,082,481,832.82 huku mradi huo ukiwa ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo mhe rais John Pombe Magufuli ametoa fedha ili kukamilishwa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwenye jukumu la kuchukua hatua ya kusimamisha uendelezaji mradi wa hospitali hiyo ya Rufaa mkoa wa Mara ni mwajiri ambaye ni Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto siyo Mshauri Elekezi.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo ndiyo Mkandarasi wa Mradi limefanya kazi kubwa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ambapo tayari Shirika hilo limeshatumia pesa zake nje ya malipo kutoka kwa Mshitiri kiasi cha shilingi bilioni 1,657,755,635.25.
 ‘’Tutaangalia ni kitu gani kilichoimsukuma Mshauri Elekezi kusimamaisha ujenzi wa mradi wa kimkakati kama huu ambao mhe Rais ametoa fedha, kuna mambo yamefanyika kificho, amepata wapi mandate ya kusimamisha kazi, hili siyo jambo la kawaida’’ alisema Dkt mabula.
Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Mara Goodluck Thomas alimuelezea Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, katika utekelezaji ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara, Shirika lake linapata changamoto kadhaa ikiwemo kusimamishwa kazi ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufungia milango na Mshauri Elekezi.
‘’ Tunayo changamoto pia ya kutopata idhini ya gharama ya kazi zilizoongezwa na Mshitiri na nyingine zikiendelea kufanyika kwa maelekezo ya Mshitiri na gharama ya kazi hiyo zimefikia bilioni 2.5’’ alisema Meneja wa NHC Mara Goodluck.
Hata hivyo, alisema NHC katika kukabiliana na changamoto hizo imefanya mawasiliano na Mshauri Elekezi pamoja na Wizara ya Afya kueleza madhara yatokanayo na kusimamishwa kazi hizo  kwa barua kwenda kwa Mshauri Elekezi za tarehe 13 Mei 2020 na 3 Juni 2020 zenye kumbukumbu namba NHC/GEN/1427/27/GM na NHC/GEN/1427/28/GM.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vedasto Mathayo amesikitishwa na kusimamishwa kazi kwa baadhi ya shughuli kwenye mradi huo hasa ikizingatiwa hospitali hiyo ya Rufaa ya mkoa wa Mara inasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi kufuatia kuelezwa kuwa ujenzi wake ungekamilika hivi karibuni.
Shirika la Nyumba la Taifa lilikabidhiwa utekelezaji wa awamu nne ya ukamilishaji mradi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara tarehe 15/08/2019 na hadi sasa kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa maeneo ya nyongeza, miundombinu ya mifumo ya maji safi awamu ya kwanza kwa jengo la Bawa C, ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa asilimia 80, ujenzi wa majengo saidizi ambayo ni jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia, jengo la karakana na jengo la kuchomea taka.

No comments:

Post a Comment