Kaimu Mkuu wa Chuo cha Kilimo (MATI) Ilonga, Abdallah Gulana akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) walipotembelea chuo hicho kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro hivi karibuni.
Mratibu wa Masomo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Felix Mrisho (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) walipotembelea chuo hicho hicho kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro hivi karibuni.
Mkufunzi na Msimamizi Mkuu wa Mashamba ya chuo hicho, John Ngairo (kulia) akitoa maelezo kwa wanahabari kuhusu shamba la mpunga la chuo hicho ambalo limelimwa kisasa.
Mahindi yakivunwa katika shamba la chuo hicho.
Msimamizi wa shamba la mifugo la chuo hicho, Elias Mkweso akizungumzia ufugaji bora wa nguruwe.
Ng'ombe wanaofugwa katika chuo hicho wakiwa malishoni.
Mkufunzi Hamisi Ramadhani wa Idara ya Chakula na Lishe, akizungumzia jinsi wanavyo sindika mazao ya kilimo chuoni hapo.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Burton Nyasi akizungumzia faida ya masomo wanayopata chuoni hapo.
Mwanafunzi wa chuo hicho, Idara ya Mifugo, Keneth Komba akizungumzia ufugaji bora wa ng'ombe.
Msafara kuelekea kwenye miradi ya chuo hicho.
Shamba la migomba la chuo hicho.
Mratibu wa Masomo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Felix Mrisho (kulia), akizungumzia teknolojia ya kilimo kwa kutumia kitalu nyumba wanayoiendesha kwa kushirikiana na Shirika la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT).
Mkuu wa Idara ya Usindikaji chuoni hapo, Moses Chavala, akielezea namna wanavyotoa mafunzo ya usindikaji.
Wakufunzi wa chuo hicho, Antoneta Sunguya na Mariam Marianda wakionesha sufuria inayotumika kuchemshia nyanya kabla ya usindikaji.
Jengo la Utawala la chuo hicho.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Philbert Lutale, akiongoza moja ya vikao kazi chuoni hapo.
Baadhi ya Wakuu wa Idara wakiwa katika moja ya vikao kazi chuoni hapo.
Baadhi ya Wakuu wa Idara wakiwa katika moja ya vikao kazi chuoni hapo.
Mwanafunzi wa chuo hicho, Noves Magomelo wa Idara ya Kilimo Hai kisichotumia chemikali za viwandani cha mazao ya mbogamboga za majumbani akizungumzia kilimo hicho.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Morogoro
CHUO cha Mafunzo ya Kilimo cha ‘Mati Ilonga’ kimezidi kupanua wigo kwenye eneo la mafunzo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, na sasa kipo mbioni kuboresha mfumo wake wauzalishaji mali ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko.
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Abdalah Gulana, alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea chuo hicho, kilichopo wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro hivi karibuni.
“Shabaha yetu kwa sasa ni kuboresha‘model’ ya uzalishaji ili kwenda sawia na mahitaji yasoko. Msisitizo wetu mkubwa ukiwa ni kuanza kuzalisha kwa kuzingatia tafiti zetu kuhusu mahitaji ya soko,” alisema Gulana.
Alisema chuo hicho chenye uwezo wa kupokea zaidi ya wanafunzi 300 bado kina fursa nyingi kwa tija na mabadiliko chanya kwenye eneo la uchumi wa viwanda, huku akiomba serikali na wadau kutoa msukumo wa kipekee, hususan kwenye rasilimali fedha kukiwezesha kupanga, kuandika, kukarabati miundo mbinu na vifaa chakavu, sanjari na kuanzisha miradi mipya kwa pamoja ili kukitegemeza.
Gulana alisema kwa sasa wamejikita katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na hatima ye hatua ya usindikaji kupitia kiwanda kidogo walichonacho kabla ya kupeleka bidhaa zao sokoni, huku nguvu kazi ya uzalishaji husika ikifanywa na wanachuo kwa zaidi ya asilimia 50.
“Tunafundisha wanafunzi ambao ni maafisa ugani tarajiwa na mfumo wa hapa Mati Ilonga tunatumia zaidi vitendo kuliko na dharia, lengo letu hasa ni kuwawezesha wahitimu kutoka na teknolojia stahiki kama wataalamu kwa tija na ustawi wa taifa,” alisema.
Kaimu Mkuu huyo ambaye pia ni mtaalamu kutoka idara ya elimu na ushauri kwa wakulima chuoni hapo, aliyataka makundi mbalimbali, taasisi na mashirika ndani ya jamii kuchangamkia fursa za kozi fupi za kati ya siku 3 mpaka 7 zinazotolewa chuoni ili kupata teknolojia mpya ambayo itawezesha kuongeza tija kupitia mafunzo ya kilimo cha kisasa, na usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo.
Alisema kozi nyingine ndefu zinazofundishwa na chuo hicho ambacho kipo umbali wa takribani kilometa 100 kutoka Morogoro mjini, na kilometa 10 toka Kilosa mjini, ni pamoja na stashahada na astashahada kwenye maeneo ya Usindikaji wa mazao kilimo na lishe, Sayansi ya Mifugo, Sayansi ya Mimea, Zana za Kilimo na Mafunzo ya Wakulima na Huduma za Ugani.
Aidha, Gulana mbali ya kuipongeza serikali kwa jitihada kadhaa za uboreshaji wa vyuo vyake, aliomba changamoto kadhaa zilizopo chuoni hapo kupewa msukumo wa kipekee, ikiwemo tatizo la uhaba na uchakavu wa vitendea kazi na miundombinu muhimu ili kuleta tija na kuongeza kasi ya uwajibikaji.
Changamoto nyingine ya chuo hicho kilichofunguliwa takribani miaka 48 iliyopita na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ni pamoja na kukabiliwa na uhaba wa watumishi pamoja na rasilimali fedha katika kukiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa wakati.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kutilia mkazo uboreshaji wa kilimo kwa lengo la kupata malighafi za viwanda ambavyo kwa sasa ndio injini ya kutufikisha kwenye uchumi wa kati na kujitosheleza kwa chakula,” alisema Gulana.
Kwa upande wake, Mratibu wa Masomo na Makamu Mkuu wa Chuo, Felix Mrisho alisema chuo hicho chenye ukubwa wa eneo la ekari 595.5 sawa na hekta 237.8 ndoto yake ni kuwa taasisi bora inayotoa mafunzo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo.
Alipongeza mashirika ambayo ni wadau wa maendeleo, wakiwemo SAT na JICA huku akieleza mpango uliopo wa kuwa na kituo kikubwa cha biashara ambacho kitatambulisha na kutumika kama soko la bidhaa zote zinazozalishwa chuoni hapo.
“Tayari tumeandika andiko na tumepeleka kwenye moja ya taasisi za elimu tukiomba kusaidiwa fedha kwa ajili ya kuboresha idara nzima ya usindikaji na ujenzi wa kituo cha biashara. Baada ya tathmini pamoja na mambo mengine, chuo kiliamua kuongeza uzalishaji, kusindika kupitia kiwanda chake kidogo na kupeleka bidhaa sokoni,” alisema Mrisho.
No comments:
Post a Comment