COVID 19 ILIVYO WAATHIRI WAFANYABIASHARA SEKTA ISIYO RASMI HASA WANAWAKE NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 4 June 2020

COVID 19 ILIVYO WAATHIRI WAFANYABIASHARA SEKTA ISIYO RASMI HASA WANAWAKE NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa, Taasisi  isiyo ya Kiserikali ya Equality for Growth (EfG), Jane Magigita (katikati) akizunguma na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu ugonjwa wa Corona ulivyo waathiri wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi hasa wanawake. Kulia ni Mwenyekiti wa muda wa Kitaifa wa Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake Masokoni hapa nchini,  Betty Mtewele na Mwezeshaji wa Sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma ambaye ni Mfanyabiashara wa Tabata Muslim

 Afisa mradi wa EfG, Susan Sitta (katikati) akizungumza katika mkutano huo.

Mkutano ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale

TAASISI  isiyo ya kiserikali ya Equality for Growth (EfG) imesema wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi hasa wanawake, wachuuzi wa sokoni ni miongoni mwa watu walio pata athari za ugonjwa wa COVID 19 . 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Jane Magigita alisema wafanyabiashara hao kutoka katika sekta hiyo ni miongoni mwa watu walioathiriwa na Covid-19.

" Katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa COVID 19 tulitumia nafasi hii kukusanya maoni ya wanawake kupitia “Vitendawili vya Corona- Simulizi za wanawake sokoni” ambazo zimetuwezesha kuibua changamoto zinazowapata wanawake wafanyabiashara zikiwemo kupungua kwa wateja, kushuka kwa mapato ya biashara, kushindwa kumudu gharama za barakoa na vitakasa mikono na mazingira kutoruhusu kukaa umbali unaotakiwa katika kujikinga kutokana na miundombinu masokoni." alisema Magigita.

Alisema Covid 19 imekua na madhara makubwa katika ajira hasa katika sekta isiyo rasmi hivyo kupelekea kuyumba na kuwa ajira imeathirika kutokana na kupunguzwa kwa masaa ya kufanya kazi, kufanyia kazi nyumbani na hitaji la kupunguza gharama za uendeshaji. 

Alisema ripoti iliyotolewa na UNDP Tanzania, Economic and Social Research Foundation (ESRF) imeonyesha madhara ya COVID 19 katika makusanyo ya kodi, kuongezeka umaskini na utofauti wa kipato kwa Tanzania. 

Aliongeza kuwa ripoti hiyo imekisia madhara makubwa katika sekta ya hoteli na utalii, uuzaji wa mazao nje ya nchi, usafirishaji na sekta ya fedha pia. Bila kuwa na hatua madhubuti za kukabiliana na COVID 19 itapelekea ugumu kuyafikia malengo endelevu ya dunia (SDGs).

Aidha ripoti nyinginezo nchini zimeonyesha maeneo ambayo yameadhirika sana na COVID 19 ni pamoja na kupungua kwa idadi ya watalii, mapato ya usafiri wa ndege, kufungwa kwa biashara karibu na mashule pamoja na vyuo, biashara za kimataifa, ukwasi wa kifedha, matumizi makubwa kwenye afya, elimu na wingi wa sintofahamu katika biashara. 

Alisema sekta hiyo inaajiri watu wengi zaidi kwani inatoa ajira kwa takribani asilimia 90% ya Watanzania na kuwa takwimu zinaonesha katika sekta isiyo rasmi wanawake ni 74% ya nguvu kazi nchini; 15% ya wanawake pia wamiliki wa biashara; 54% ni wajasiriamali wadogo na wa kati na kuwa wako katika nyanja mbalimbali za uzalishaji na mnyororo wa thamani ikiwemo kilimo, huduma na biashara.

Alisema EfG imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na jamii na kwa kushirikiana na Serikali, katika kuwawezesha wanawake wa sekta isiyo rasmi kuwa na sauti ya pamoja na kuweza kusimamia haki zao za kibiashara na kiuchumi kwa kupinga ukatili pamoja na vikwazo vya kijinsia. 

"Tumewafikia wanawake kwa kutoa mafunzo ya biashara, uwekezaji, ugawanyaji wa mapato, kuweka akiba na sera za ujasiriamali. Pia kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi na kushiriki katika nafasi na vyombo vya maamuzi." alisema Magigita.

Magigita alitaja baadhi ya mapendekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa na wadau mbalimbali kuhusu maendeleo katika majanga ya namna hiyo ni Taasisi za fedha ziangalie namna bora ya kupunguza makali ya marejesho kwa wafanyabiashara wadogo na walio katika sekta isiyo rasmi. Kipaumbele kitolewe kwa wanawake, watu wenye ulemavu, na vijana.

Mapendekezo mengine ni Taasisi za mbalimbali za fedha zinazotoa mikopo midogo ambazo hazisimamiwi moja kwa moja na Benki Kuu kama vikundi vya VICOBA, SACCOS na wakopeshaji binafsi kufikiria namna ya kupunguza riba kubwa zinazotozwa kwa wafanyabiashara wadogo.

Elimu ya Ujasiriamali na usimamizi wa fedha itolewe na taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini  kwa wafanyabiashara ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambao tayari wameathirika na COVID 19.

Kwa kuwa wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi wengi wao hutumia simu kama benki, tunashauri wanaotoa huduma za kibenki kupitia mitandao kupunguza gharama za kutuma na kupokea pesa kutumia mitandao ya simu, na kiwango cha kutuma pesa kiongezwe. 

Halmashauri zote nchini ziendelee kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10% ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya miradi na biashara, ambazo zinachangia kumuinua mwanamke kiuchumi.

Benki Kuu imedhamiria kuziwezesha taasisi za kifedha kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha (ukwasi), ili zitoe mikopo yenye riba nafuu kwa wananchi. Kwa kufanya hivyo watanzania walio wengi wataweza kukopa kwa riba nafuu hivyo kuboresha shughuli zao za kuichumi.

Magigita alisema wanatumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wa sekta isiyo rasmi waliochukua mikopo kutoka taasisi za fedha na wameshindwa kuzitumia hizo fedha kutokana na wateja waliokuwa wanatarajia kuwafikia hawapo tena kutokana na COVID 19, wasizitumie hizo fedha kwa shughuli mbadala. Wazirudishe kwa mkopeshaji na wajadiliane kuhusu punguzo la riba.

Biashara zisibadili matumizi ya fedha wakati huu wa COVID 19, ikibidi kufanya hivyo basi watafute ushauri kutoka kwa wataalamu au kwa walio wakopesha/waliowapa fedha.

Wafanyabishara wawe makini sana katika kutafuta vyanzo vya mitaji katika wakati huu ili wasije wakaingia katika mitego ya wakopeshaji wenye riba na masharti yasiyostahimilika. 

Kuchangamkia fursa ama unafuu unaotolewa na serikali pamoja na taasisi nyingine wakati huu wa COVID 19 kukuza biashara zao. 

Maoni ya wanawake wafanyabiashara sekta isiyo rasmi masokoni wakitoa maoni yao kuhusu shughuli zao za kiuchumi kuathiriwa na ugonjwa huo wamesema kutokana na mapato kupungua sana katika biashara zetu kwani na watu hawatembelei masokoni na kukaa nyumbani zaidi. Hii imetokana na kupungua kwa wateja ikiwemo katika mahoteli ambao ndio watumiaji wakubwa wa mbogamboga na matunda tunayouza sokoni.

Kuwepo kwa miundo mbinu inayoweza kuimiri majanga, kwani wanawake wengi waliamua kusimama biashara kwa kuhofia maambukizi ya COVID 19.

Changamoto ya kushindwa kulipa mikopo kutokana na kipato duni, tunaomba taasisi za fedha zilizotupa mikopo, ambazo kwa sasa zinapata unafuu kutoka Benki Kuu zitufikirie zaidi wanawake wa sekta isiyo rasmi.

Sekta isiyo rasmi tunaomba tufanyiwe tathmini ya athari za COVID 19 na kuchukua hatua ili kuwezeshwa kwa kupewa mikopo yenye riba nafuu kama walivyopewa Sekta rasmi nchini. 

Wanawake hao wameipongeza serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa jitihada kubwa na za kimkakati kuunusuru uchumi hususani wakati wa janga la COVID 19. Sanjari na pongezi zetu tumeamua kama shirika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha athari za COVID 19 zinapunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa wafanyabiashara wadogo hususani wanawake nchini. 

"Kama alivyosema Raisi wetu Dkt. John Magufuli hivi virusi vinaweza kuwa kama majanga mengine na tukalazimika kuishi navyo katika maisha yetu yote, hivyo sera dhabiti zinahitajika kuwasaidia watu wanaoendesha shughuli zao katika sekta isiyo rasmi waweze kujikwamua. Tunaamini kwa kushirikiana, nchi yetu itaendelea kuishinda vita dhidi ya COVID 19, na uchumi wetu kuendelea kuimarika." alisema Mwenyekiti wa muda wa Kitaifa wa Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake masokoni hapa nchini,  Betty Mtewele. 


No comments:

Post a Comment