Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
|
Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa imetenga Sh. bilioni 600 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya Watumishi wa umma kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni moja ya mkakati wa kuleta nidhamu na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bumbwini, Mhe. Muhammed Amour Muhammed, aliyetaka kujua ni lini Serikali italipa madeni ya Watumishi wa umma kutokana na madeni hayo kuongezeka.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imetenga jumla ya Sh. bilioni 600 ambazo zimeidhinishwa na Bunge ili kugharamia malipo ya madeni mbalimbali ikijumuisha madeni ya Watumishi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 jumla ya shilingi bilioni 364.7 zimelipwa kama madai ya Watumishi, Wazabuni na Wakandarasi ambapo kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 97.6 zimelipwa kama madeni ya Watumishi pekee”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2019/2020 jumla ya Sh. bilioni 375.7 zilitolewa kugharamia madeni mbalimbali, kati ya fedha hizo Sh. bilioni 113.8 zilitumika kulipa madeni ya mshahara na Sh. bilioni 261.9 madeni yasiyo ya mshahara.
Dkt. Kijaji alibainisha kuwa, kutokana na changamoto ya uwepo wa madeni hewa Serikali ilizuia ulipaji wa madeni kabla ya kuhakikiwa lengo likiwa ni kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha kutokana na takwimu hizo, Serikali inajisikia fahari na inahitaji kupongezwa kutokana na juhudi mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha madeni yote ya Watumishi yanalipwa kwa wakati ikithibitika yana uhalali.
No comments:
Post a Comment