BIASHARA KUENDELEA TUNDUMA LICHA YA ZAMBIA KUFUNGA MPAKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 11 May 2020

BIASHARA KUENDELEA TUNDUMA LICHA YA ZAMBIA KUFUNGA MPAKA

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akizungumza na Wananchi katika eneo la Tunduma mapema leo ambapo amewataka kuendelea na shughuli za kiuchumi licha ya Zambia Kufunga Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Nakonde.

Wafanyabiashara wa Tunduma wakiendelea na shughuli mbalimbali za Kiuchumi kama serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyo waelekeza licha ya Zambia kufunga Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Nakonde.

WAFANYABIASHARA wametakiwa kuendelea na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma ambao uko katika Mpaka wa Tanzania na Zambia ikiwa tayari Nchi ya Zambia imefunga Mpaka wake wa Nakonde kuanzia leo Mei 11, 2020.

Akizungumza na Wananchi katika eneo la Tunduma mapema leo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema Tanzania haijafunga mpaka wala kufunga shughuli zozote za Kiuchumi hivyo wananchi wa Tunduma waendelee kufanya shughuli za Kiuchumi ikiwa ni pamoja na biashara.

“Sisi hatujaweka Lockdown, tuendelee na shughuli zetu, wananchi wa Tunduma mko huru chapeni kazi ila tufuate maagizo ya serikali ya kujikinga na Corona kwa kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko na kunawa kwa maji tiririka na sabuni, tufanye kazi huku tunajilinda na Corona.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

Aidha, Brig. Jen. Mwangela amewataka wananachi wa Tunduma na Mkoa wa Songwe kufuata maelekezo yaliyotolewa na Nchi ya Zambia ya kutovuka Mpaka hivyo wasiingie huko kufanya biashara bali kwa sasa biashara ziendelee upande wa Tanzania mpaka hapo mpaka utakapo funguliwa.

John Mtafya Mkazi wa Tunduma ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu shughuli za Kiuchumi kuendelea katika Mpaka wa Tunduma licha ya kuwa kufungwa kwa Mpaka upande wa Zambia kuta athiri Mahusiano ya kibiashara yaliyokuwepo.

Mtafya amesema wafanya biashara wa Tunduma wataendelea na biashara kama ilivyokuwa awali huku wakijilinda dhidi ya Ugonjwa wa Corona kama ambavyo serikali imeelekeza.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zambia Edgar Chagwa Lungu hapo jana Waziri wa Afya wa Nchi hiyo Chitalu Chilufya ametangaza uamuzi wa Kufunga Mpaka kufuatia ripoti ya wagonjwa 76 wa Corona katika Mji wa Nakonde ulio katika Mpaka wa Tanzania na Zambia.

No comments:

Post a Comment