Ubovu wa tairi barabarani. |
KWA NINI KATIKA “NOTIFICATION” UBOVU WA TAIRI LIMEORODHESHWA KUWA KOSA TOFAUTI NA UBOVU WA GARI?
Uhalali wake ukoje ikiwa tairi ni sehemu ya mfumo wa gari?
Kwamba inatokea gari inapokaguliwa ikakutwa, kwa mfano bodi ni chakavu, breki hazifanyi kazi vizuri, mikanda mibovu, tairi chakavu. Basi hapa askari anaandika makosa mawili: 1. Ubovu wa gari kinyume na kif.39(1)(a) &(b)2,3; 2. Tairi mbovu kinyume na Kanuni 30(1). Mkosaji anatakiw akulipa shilingi 60,000. Je ni sahihi kwa mujibu wa sheria? Je sheria inasemaje?
KIFUNGU CHA 39(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani Tanzania (RTA) kinaorodhesha sehemu kuu za mfummo wa gari au ukipenda ita mifumo mikuu ya gari. Kifungu kinaitaja mifumo hiyo kuwa ni: 1.Chesesi; 2. Injini; 3.Mfumo wa gia; 4. Mfumo wa breki; 5. Bodi au sehemu za bodi; 6. Tairi na taa.
Kifungu hiki kinataka gari au tela na sehemu zake hizi na vifaa vyake vinavyounda sehemu hizo:
(a) Kuwa katika hali nzuri na vinafanya kazi vizuri, na vipo katika hali ambayo uendeshaji wa gari barabarani mchana au usiku, hauwezi kuwa hatari kwa watu wanaosafiri na gari au tela hilo au kwa watumiaji wengine wa barabara;
(b) Vinazingatia matakwa yote na maelekezo kadiri yalivyo kwenye kanuni
Na kwamba ikiwa gari limeshindwa kukidhi masharti na vigezo vya kifungu cha 39 hapo juu basi gari husika ni bovu na mhusika, akitiwa hatiani mahakamani, atatakiwa kulipa faini ya shilingi 50,000 kama ilivyoainishwa katika Kif.39(5) cha RTA. Hii ni sharia mama. Sheria mama hutafsiriwa na kanuni ili kurahisisha utekelezaji.
SASA TWENDE KWENYE KANUNI.
Sehemu ya VI ya Kanuni za Trafiki (The Traffic Regulations) inasomeka: Conditions as to the Use and Construction of Vehicles. Kwa lugha nyepesi ni masharti ya kutumia na kuunda gari.
Kanuni ya 30 (1) ya Kanuni hizi ina maneno ya pembezoni (marginal notes) yaliyoandikwa Conditions as to the use of motor vehicles. Yaani masharti ya kutumia magari. Kanuni inasema ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia au kuruhusu gari litumike barabarani au kuendesha gari barabarani isiyokuwa kama masharti yaliyoainishwa kwenye kanuni hii yamezingatiwa. Kanuni ina vipengele a;b;c;d;e;f;g; hadi m.
Kipengele (g) kinahusu aina ya matari yanayopaswa kutumika na kwa mujibu wa kipengele hiki matairi yanayopaswa kutumi ni “pneutmatic tyres”. Na kipengele (h) kinapiga marufuku matumizi ya tari za chuma barabarani bila idhini ya mamlaka.
Kipengele (i) kinahusu utunzaji wa matairi. Kwa mujibu wa kipengele hiki ‘tairi zinazotumika kwenye gari kwa wakati wote wakati gari ikiwa inatembea zitakuwa zimetunzwa katika hali ya kutokuwa na ubovu wa aina yeyote (any defect) unaoweza kusababisha madhara kwenye uso wa barabara au kwa watu waliomo juu au ndani ya gari au kwa watumiaji wengine wa barabara”.
Kipengele (j) kinahusu kipenyo (diamter) cha tairi la gari. Kipengele hiki kinaweka masharti kwamba kipenyo cha tairi la gari ambalo uzito wake unazidi uzito wa 200 hautakuwa pungufu ya inchi 26.
Baada ya hapo hakuna kipengele kingine chochote kinachohusu matairi.
SASA MASWALI YA KUJIULIZA BADO YANABAKI
1. Je, Kuna utofauti wowote wa kilichoandikwa kwenye sheria mama kifungu cha 39(1)(a) na (b) na kile kilichoandikw akwenye Kanuni ya 30(1)(i)? Ili tuseme kwamba ubovu wa tairi ni kosa tofauti?
2. Sheria ya tafsiri za Sheria (The Interpretation Act) inasema kunapotokea utata au ukinzano kati ya sheria Mama (Parent Act) kama ilivyo Road Traffic Act na kanuni (by-law) iliyotungwa chini ya sheria hiyo, basi kilichoandikwa kwenye sheria mama ndicho kinakuwa na nguvu (prevails); Je, bado tunaona ipo sababu ya kusema tairi sio sehemu ya mfumo wa gari na hivyo kuwa kosa tofauti wakati sheria mama inaliorodhesha kuwa kosa moja chini ya kifungu cha 39(1)?
3. Kama tairi sio sehemu ya mfumo wa gari, je gari likikosa matairi hata kama kila kitu kizima kinafanya kazi, linaweza kutembea?
MSIMAMO WANGU MIMI: Ubovu wa gari unahusisha na tairi, hivyo sio kosa linalojitegemea.
Karibuni kwa mjadala
RSAadmin1
RSA Tanzania
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote.
No comments:
Post a Comment