DIWANI AOMBA CHUO KIPYA CHA UFUNDI KWA WALEMAVU MKOANI SINGIDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 6 April 2020

DIWANI AOMBA CHUO KIPYA CHA UFUNDI KWA WALEMAVU MKOANI SINGIDA

 Diwani wa Kata ya Utemini,   Baltazar Kimario.
Na Ismail Luhamb,Singida.
DIWANI  wa Kata ya Utemini Manispaa ya Singida, Baltazar Kimario, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga chuo kipya cha ufundi stadi cha kwa ajili ya watu wenyeulemavu mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari  katika kikao cha baraza la madiwani kilicho keti mwishoni mwa wiki, Kimario, alisema chuo kinachoendelea kutumika kilijengwa  miaka ya 70 hivyo miundombinu yake imechakaa inahitaji ukarabati wa mkubwa.
  Kimario alisema  chuo cha sasa kimezingirwa na maji, kitendo kinachohatarisha maisha ya wanafunzi na walimu wao.  
Akifafanua alisema kwa muda mrefu amekuwa akiilalamikia mitaro ya maji zaidi ya mitatu kuelekezwa kwenye chuo hicho inayochangia mazingira ya chuo hicho yasiwe rafiki.
“Chuo hiki kinapokea wanafunzi wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao wana ulemavu wa aina tofauti wakiwemo wenye  uoni hafifu hivyo ni muhimu mazingira ya chuo yakaboreshwa”, alisema..
“Aidha,eneo limekuwa chepechepe kutokana na kufumuka kwa chemuchemu nyingi.Mlemavu anayetumia baiskeli ya tairi tatu, fimbo/ magongo au wenye uoni hafifu mazingira ya chuo kwa sasa, sio rafiki”.
Kutokana na hali hiyo  Kimario, alisema kama kutakuwa hakuna uwezekano wa kujenga kipya kwa sasa,amependekeza mitaro iliyoelekezwa chuoni hapo itafutiwe  mkondo mwingine. 
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho, Fatuma Malenga, alisema mitaro hiyo imesababisha maji ya mvua kusambaa sehemu kubwa ya chuo na kusababisha changamoto ya kupitika. 
“Kuna darasa maji yanatoka chini ya sakafu baadhi ya majengo misingi yake maji yametuama kwa muda mrefu na kwa miaka kadhaa nimekuwa nikiilalamikia mitaro hii, lakini ufumbuzi wa tatizo hili kuondoa au kuichepusha  mitaro  bado haujapatikana”. alisema Malenga.
Mwanafunzi  wa fani ya uselemala,  Jackson Nyamhanga, ametumia fursa hiyo kuiomba serikali iboreshe mazingira ya chuo hicho kikongwe ili kiwe kimbilio kwa walemavu kupata haki yao ya elimu. 
Mwanafunzi huyo kutoka mkoani Geita, amesema endapo chuo kitafunguliwa na maji yakaendelea kusambaa chuoni hapo itawawia  vigumu  kuendelea na masomo kutokana na vyoo kujaa maji. 
Wakati huo huo,  Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)  Manispaa ya Singida, Mhandisi  Lambert Bayona, alisema kwa ujumla chuo hicho kimejengwa kwenye eneo la maji lenye chemuchemu.
“Hii mitaro inayolalamikiwa inapitisha maji yanayotoka kwenye chemuchemu za sehemu mbalimbali katika eneo la Sabasaba. Maeneo hayo yapo juu au kwenye mwinuko. Chuo chenyewe kipo chini. Kwa hiyo sio kweli mitaro imeelekezwa chuoni, maji yanafuata  mkondo wake ”, alisema  Bayona. 
Hata hivyo, Bayona, ameahidi kutatua changamoto hiyo.

No comments:

Post a Comment