NMB WASAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO PAWAGA. - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 6 April 2020

NMB WASAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO PAWAGA.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela wakipokea msaada kwa Meneja wa Benk ya NMB tawi la Iringa huku wakiwa na Tahadhari ya kujikinga na virusi vya Corona

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya akikabidhiwa msaada na kiongozi wa wauzaji wa vipuri vya magari mjini Iringa (Famari Stores).

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akipeleka sehemu ya kuhifadhi msaada huo.

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
 
SERIKALI ya wilaya ya Iringa imepokea msaada wa chakula na sabuni kutoka kwa wauzaji wa vipuri vya magari mjini Iringa (Famari Stores) na Benki ya NMB kwa lengo la kuziwezesha baadhi ya kaya zilizokumbwa na mafuriko katika kitongoji cha Mbingama kijijini Isele, tarafa ya Pawaga wilayani Iringa kukabiliana na changamoto ya bidhaa hizo.

Msaada huo unaohusisha unga na maharage ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela na wawakilishi wa taasisi hizo kwa nyakati tofauti mjini Iringa jana.

Akishukuru kwa msaada huo, Kasesela alisema; “unasafirishwa leo leo hadi kwa wahanga hao ili ukafanye kazi iliyokudiwa. Mahitaji ya vyakula na vitu vingine vya kibinadamu kwa wahanga wale ni makubwa na ya haraka.”

Kasesela alisema mafuriko yaliyotokea hivikaribuni katika kitongoji hicho yamesebabisha kaya 218 zenye jumla ya watu 801 kuachwa bila makazi huku akiba yao ya vyakula, fedha, nguo na vifaa vyao vingine vikisombwa baada ya nyumba zao kubomoka.

“Mahitaji ya kibinadamu kwa wahanga hawa ni makubwa, tunaendelea kupokea misaada kutoka kwa wasamalia wema popote pale walipo na niishukuru kampuni ya Famari Stores na benki ya NMB kwa kusikia na kujitoa kuwasaidia wahanga hao,” alisema.

Wakati taarifa ya mwakilishi wa kampuni ya Famari Stores, Clement Kayage inaonesha msaada wao wa unga na sabuni una thamani ya zaidi ya Sh Milioni 1.5; meneja wa benki ya NMB tawi la Mkwawa, Komari Kiwia alisema msaada wao wa unga na maharage una thamani ya Sh Milioni 2.

Akikabidhi msaada huo, Kayage alisema; “Baada ya kupata taarifa za hali iliyowakuta wahanga hao, kampuni yetu iliguswa na kwa kuanzia tumetoa msaada wa unga na sabuni wenye thamani hiyo na tutakapopata nafasi tena basi tutaangalia chakusaidia.”

Naye meneja wa NMB alisema; “sisi kama taasisi tunayofanya kazi na jamii ya mkoa wa Iringa tumetoa unga na maharage, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh Milioni mbili kama mchango wetu unaolenga kuwafariji wahanga hao.”

Akiziomba taasisi zingine kujitokeza kuzisaidia kaya hizo Kasesela alisema serikali imeamua kuwaondoa moja kwa moja wahanga hao katika kitongoji hicho kwa kuwa rekodi zinaoneshwa kimekuwa kikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara.

“Kwahiyo kaya zote zimeondolewa katika kitongoji hicho cha Mbingama-hivyo hawataruhusiwa kurudi tena pale na serikali imekwishawapa maeneo mengine ndani ya  kijiji cha Isele kwa ajili ya kujenga makazi yao mapya,” alisema.

Alisema kuhamishwa kwa wananchi hao kumeongeza mahitaji yao vikiwemo vifaa vya ujenzi wa nyumba, vyakula, nguo na mahitaji mengine ya msingi ya binadamu.

“Msaada wa Famari Stores na NMB umekuja baada ya hivikaribuni kupokea msaada wa unga na nguzo za ujenzi kutoka kampuni ya Qwihaya General Enterprises ya mjini Mafinga,” alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya aliwataja wengine waliotoa msaada kwa wahanga hao kuwa ni pamoja na world vision, msalaba mwekundu na taasisi mbalimbali za dini.

“Lakini na sisi kama halmashauri tumefanya juhudi kwa kupeleka unga, maharage, mafuta na maturubai kwa ajili ya kuwasitiri wahanga hao,” alisema.

Masunya alisema halmashauri yake pia imewapeleka wataalamu wa afya ili kuwasaidia wahanga hao kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa corona unaooendelea kusambaa sehemu mbalimbali dunia.

No comments:

Post a Comment