REPSSI NA SERIKALI YA KIBITI WAPITA MITAANI KUTOA ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 6 April 2020

REPSSI NA SERIKALI YA KIBITI WAPITA MITAANI KUTOA ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA

 Mkurugenzi wa REPSSI Edwick Mapalala kushoto akimkabidhi mganga mkuu wa wilaya ya Kibiti Martin Mwandiki msaada wa kujikinga na virusi vya Corona.

 Maafisa wa REPSSI na serikali ya Kibiti wakiwa njiani kuwafuata wananchi waliko

Tumaini Godwin, Kibiti

SHIRIKA la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti wameamua kupita mtaa kwa mtaa kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona ‘covid 19’.

Bila kutengeneza mikusanyiko ya watu, maafisa wa REPSSI na halmashauri ya wilaya hiyo walikuwa wanatumia gari ya matangazo kutoa elimu hiyo kwa jamii ili kujkinga na ugonjwa huo.

Akizungumza katika kampeni hiyo, Mkurugenzi wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala amesema ni muhimu jamii kuchukia tahadhali kwa kufuata miongozo yote inayotolewa na wataalamu wa afya.

“Mnatakiwa kunawa maji mara kwa mara na  hakikisheni hamkai kwenye misongamano,” alisema Mapalala.

Alisema REPSSI imeamua kushirikiana na Serikali katika kuamua wanatoa elimu kwa jamii ili ijikinge na maambukizi ya ugonjwa huo unaotikisa dunia.

“Na tunasisitiza watoto watunzwe na walindwe, wasiachwe mitaani hovyo ndio maana shule zimefungwa. Kila mzazi na mlezi ahakikishe usalama wa mtoto wake,” alisisitiza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mohamed Mavura amesema wilaya hiyo imechukua tahadhari zote kupambana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Aliyaomba mashirika mengine kusaidia katika kutoa elimu na vifaa kwa wananchi ili waendelee kujikinga.

Kwa upande wake, Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kibiti, Antony Nyange amesema mkakati uliopo ni kupita katika kata zote kutoa elimu hiyo.

“Tutapita kwenye kata zote mpaka za visiwani, tunataka wananchi wapate uelewa kuhusu corona kwa sababu ugonjwa huu unahtaji tahadhari kubwa,” amesema Nyange.

No comments:

Post a Comment