WANAOFANYA MIZAHA YA CORONA KUCHUKULIWA HATUA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 22 March 2020

WANAOFANYA MIZAHA YA CORONA KUCHUKULIWA HATUA

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe katika Kikao cha Kutathmini utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe, ambapo  amesema watu wanao fanya mizaha mitandaoni kuhusu ugonjwa wa Corona hao watachukuliwa hatua.

Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Songwe wakifuatalia mada mbalimbali kuhusu tathmini ya utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe ambapo  moja ya maazimio ni kutoa elimu Zaidi kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari ya Corona.


IMEBAINIKA kuwa wapo baadhi ya watu ambao hutumia mitandao ya kijamii kutengeneza na kusambaza mizaha na taarifa za uongo juu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona huku wakiwaaminisha wengine kuwa ugonjwa huo hauwapati watu weusi.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe katika Kikao cha Kutathmini utayari wa Kupambana na Ugonjwa wa Corona Endapo utatokea Mkoani Songwe, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema watu hao watachukuliwa hatua kali.

Palingo amesema mizaha hiyo inadhoofisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Corona na kuwafanya wananchi wengine kutotilia maanani maelekezo ya wataalamu wa Afya ya kuchukua hatua za tahadhari kwakuwa mapambano hayo ni vita ambayo inajumuisha jamii nzima.

Amesema kuwa licha ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kutangaza kuwachukulia hatua kali wote wanao sambaza mizaha na taarifa za uongo kuhusu Ugonjwa wa Corona, Uongozi wa Mkoa wa Songwe na Wilaya zote pia hauta wavumilia wote watakaofanya vitendo hivyo Mkoani hapa.

Palingo ameongeza kuwa wazazi na walezi wote wahakikishe wana waangalia watoto wote wasizagae mitaani, sokoni, minadani na katika mikusanyiko ya masomo ya ziada (Tuisheni) kwani serikali imefunga shule ili kuchukua tahadhari ya kuwakinga wanafunzi dhidi ya Ugonjwa wa Corona.

Amesema serikali inaendelea kusisitiza Sehemu ambazo lazima mikusanyiko iwepo kama katika nyumba za ibada na katika ofisi mbalimba, maji ya kunawa na sabuni yawepo na pia hatua zote muhimu za tahadhari zichukuliwe.

Aidha Palingo amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuacha masuala ya mila yanayoweza kuwawaweka katika hatari ya kuambukizana ugonjwa wa Corona hususani mila ya kusalimiana kwa kushikana mikono.

Amesema waanchi wanapaswa kuelewe kuwa wasisubiri ifikie hatua ya kutibu wagonjwa wa corona bali wazuie Kwanza kwa kuchukua tahadhari ya kujikinga kwani ikifikia hatua ya kutibu watu wengi wanaweza kupoteza maisha.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamadi Nyembea amesema Mkoa wa Songwe unatoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa wananchi kwa ngazi zote kwani ni njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa huo.

Dkt Nyembea amesema Kamati za Afya za Wilaya hadi ngazi ya Kata zitahakikisha zinafikisha elimu ya kujikinga na Corona kwa wananchi pia maafisa wengine wa Serikali nao washiriki kuwaelimisha wananchi.

Sauli Ndambo Mkazi wa Ilembo Wilaya ya Mbozi ameishukuru serikali kwa kuchukua tahadhari na kufunga shule ili watoto wawe salama huku akiwataka wanao fanya mizaha kuacha mara moja kwani ugonjwa huo hauna mzaha na unaua.

Laurent Mwasile Mkazi wa Vwawa Wilaya ya Mbozi amewasihi vijana kuchukua tahadhari na kuacha mila ya kusalimiana kwa mikono na endapo watamuona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo watoe taarifa katika vituo vya Afya.

No comments:

Post a Comment