WAHADHIRI 21 WAPATIWA MAFUNZO YA STADI ZA KUFUNDISHIA KISWAHILI KWA WAGENI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 12 March 2020

WAHADHIRI 21 WAPATIWA MAFUNZO YA STADI ZA KUFUNDISHIA KISWAHILI KWA WAGENI

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe akisisitiza  kuwasilisha orodha ya majina ya wataalamu wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa Waziri wa Mambo ya nje kwa lengo la kusambazwa katika balozi mbalimbali Tanzania nje ya nchi leo Jijini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya kuimarisha stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa wahadhiri wa chuo kikuu cha Dodoma yaliyoratibiwa na Baraza la Kiswahili Tanzania.


Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Tanzania Consolata Mushi akitoa taarifa kwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe kuwa taasisi yake tayari imekwisha sajili jumla ya wahitimu 1224 katika kanzidata ya wataalamu wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wageni,leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa wahadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Dodoma.


Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof.Justine Ntalikwa akimweleza Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe leo Jijini Dodoma kuwa jumla ya wahadhiri ishirini na moja wanaofundisha lugha ya Kiswahili katika chuo hicho wanashiriki mafunzo hayo kwa ya stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni yatakayofanyika chuoni hapo kwa siku nne.


Na Shamimu Nyaki- WHUSM, Dodoma

WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amesisitiza  kuwasilisha orodha ya majina ya wataalamu wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  kwa lengo la kusambazwa katika balozi.

Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya Stadi za kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni ambayo yanatolewa kwa wahadhiri 21 wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mheshimiwa Mwakyembe alisema kuwa  fursa za kufundisha  lugha ya Kiswahili duniani ni nyingi, hivyo watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hizo katika kujiongezea kipato pamoja na kukuza lugha hiyo.

“Serikali iliona uhitaji wa waalimu wakufundisha lugha ya Kiswahili nje ya nchi ,hivyo iliamua kuanzisha kanzidata ya wataalamu hao ambao kwa sasa wamefikia 1,224 na nchi mbalimbali zimeanza kutuma maombi ya uhitaji wa wataalam hao” alisema Mhe.Makyembe.

Dkt.Mwakyembe ameongeza kuwa orodha ya majina ya wataalam wa lugha hiyo itawasilishwa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi za Tanzania nje ya nchi kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa wataalamu hao.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Bibi. Consolatha Mushi alisema   kuwa mafunzo hayo hutolewa kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu katika taaluma ya lugha ya Kiswahili kuanzia Shahada ya kwanza hadi Uzamivu.

“Mafunzo haya yanatolewa na BAKITA ikiwa ni kutekeleza agizo   ulilolitoa wewe Mhe.Waziri Agosti mwaka 2018 wakati ulipotembelea Baraza letu na kubaini kuwa hakuna takwimu halisi za wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini hivyo Baraza limetekeleza agizo hilo” alisema Bibi.Consolatha.

Ameongeza kuwa hadi sasa mafunzo yameshatolewa kwa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya,  Tanga  Mwanza na Arusha lengo kiwa ni kuwaanda  waalimu wa Kiswahili kunufaika na  fursa mbalimbali za Kiswahili zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.

Naye, Dkt.Samweli Mgaya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Idara Kuu ya  Kiswahili, alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wataalamu hao kueneza lugha adhimu na aushi ya kiswahili kwa namna ambavyo inatakiwa hasa matumizi sahihi ya lugha hiyo.

Mafunzo haya yameanza kutolewa machi 9 hadi machi 13,2020 kwa ushirikiano Ndaki ya Insia na Elimu na Jamii pamoja na Idara ya Kiswahili, ikiwa ni awamu ya pili kutolewa hapa Jijini Dodoma baada ya awamu ya kwanza kufanyika mwezi Oktoba, 2018.

No comments:

Post a Comment