MUFTI ATOA MAAGIZO KUHUSU UGONJWA WA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 19 March 2020

MUFTI ATOA MAAGIZO KUHUSU UGONJWA WA CORONA

Mufti Abubakar Zubairy bin Ally.

TAMKO LA BARAZA LA ULAMAA KUHUSIANA NA JANGA LA UGONJWA WA CORONA (COVID 19)

Kutokana na misingi ya Dini ya Kiislam, Barazala Ulamaa linafafanua na linaagiza waislamu kufanya Mambo yafuatayo:-

1. Muislamu yeyote atakaepatwa na maradhi haya ni haramu kwake kuhudhuria Swala ya Ijumaa na Swala za Jamaa kama ambavyo pia ni haramu kwake kuchanganyika na watu wengine kwani kufanya hivyo ni kuusambaza na kueneza ugonjwa huo kwa wenzake.

2. Mamlaka zinazohusika zikitangaza karantini kwa eneo lolote ,waislamu wa eneo hilo wanaruhusiwa na sheria ya kiislamu kutohudhuria Swala ya Ijumaa na Swala zote za Jamaa.

Kwa sababu lengo la Swala za jamaa ni kujenga umoja na pia kuleta maslahi na manufaa kwa Waumini, Ama kuhudhuria huko kunapokuwa ni sababu ya kuambukizana maradhi, basi kuhudhuria huko kunageuka kuwa Haramu, Hivyo, swala hizo za jamaa zinazuiwa kisheria mpaka hali hiyo itakapobadilika na kuthibitishwa na wataalamu wa afya.

Kama ambavyo imepokewa kuwa Bwana Mtume (S.A.W), aliwahi kuwazuia watu kuja msikitini ili wasiwaudhi wenzao kwa harufu inayotoka kwenye midomo yao kwa kula vitunguu. Na inatambulika kwamba madhara ya harufu ya vitunguu ni madogo mno ukilinganisha na madhara ya kuambukiza ugonjwa wenye kuangamiza.

3. Hivyo Baraza la Ulamaa linawataka Waislamu Wote Nchini pale amri ya karantini itakapotolewa na Mamlaka husika ,kutii na kutekeleza kwa kuwa Amri hizo zinaenda sambamba na mafunzo ya dini ya kiislamu na maamrisho yake.

4. Kutekeleza Amri hizi Kwa lengo la kuokoa nafsi zisiangamie ni Ibada kubwa na mtekelezaji wa amri na maagizo haya atalipwa thawabu zisizo na kifani. Ama Yule atakaepinga Amri hizi akasababisha watu kuambukizwa na kufa ataandikiwa Dhambi zisizo na kifani kwa mujibu wa Aya tuliyotaja hapo juu.

5. Baraza la Ulamaa linawataka waalimu wote wa Madrassa pamoja na viongozi wa Madrassa kufunga Madrassa zote kufuatia agizo la serekali kusitisha masomo kwa shule zote mpaka itakapotangazwa tena.

6. Kuacha mikusanyiko isiyo na lazima katika kipindi hiki .

7. Kuhakikisha Waumini wote wananawa mikono kwa sabuni na maji yenye kutiririka kabla ya kuingia msikitini kutekeleza Ibada.

8. Baraza la Ulamaa linawashauri waumini wote wenye uwezo kwenda Msikitini na Miswala yao.

9. Baraza pia linawashauri Waumini wenye matatizo ya kiafya na wale wenye umri mkubwa kuswali majumbani mwao kwani ugonjwa huu huambukiza kirahisi watu wenye sifa hizi zilizotajwa katika kipengele hiki. 

10. Kuhakikisha kuwa kanuni za usafi Msikitini zinakamilishwa .

11. Inashauriwa kwa kila Muumini kuchukua Udhu nyumbani kwake pale anapokusudia kwenda Msikitini.

12. Baraza linawataka Waumini kutii na kutekeleza Maagizo yote ambayo tayari yameshatolewa na Wizara ya Afya katika kupambana na kujilinda na janga hili, kama vile kuziba kinywa wakati wa kupiga chafya, kunawa mikono, kuzingatia usafi kwa kiwango cha juu, kwani yote hayo ni mafunzo ya Mtume (S.A.W) aliyoyatoa kwa waumini karne 15 zilizopita.

Mwisho Baraza la Ulamaa linawataka Maimam wote kusoma dua ya Qunuti katika swala zote za faradhi kumbembeleza Mungu atuondolee janga hili nchini na duniani kwa ujumla.
.........

Harith Nkussa
Mwandishi maalum wa mufti
18.3.2020
Jumatano saa sita na dk 5 mchana
Ofisi ya Mufti
Mtaa wa Lumumba
Dar es salaam

No comments:

Post a Comment