Watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutoka mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Waziri huyo na watendaji hao jijini Dodoma.
WAZIRI WA UJENZI, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amewaagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuhakikisha kuwa magari yote ya Serikali yanayotengenezwa katika karakana zao hayaibui matatizo na kuzua malamiko kwa mshitiri mara baada ya kutengenezwa.
Kamwelwe ametaja malalamiko hayo kuwa ni TEMESA kutotengeneza magari kwa umakini pamoja na gharama za matengenezo kuwa kubwa ukilinganisha na watoaji wengine wa huduma za matengenezo na ufundi wa mitambo.
Kamwelwe ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati alipokutana na watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na kusisitiza kuwa agizo hilo litatekelezwa kuanzia kesho Tarehe 13 Machi 2020, ambapo amefafanua kuwa Wizara na Taasisi za Serikali ambazo zitaleta malalamiko hayo kwa Meneja ambaye hakutekeleza majukumu yake ipasavyo, Waziri huyo atachukua hatua kali ikiwemo kumfukuza.
“Tutahakikisha kuwa tunakusimamisha kazi na kuunda kamati itakayochunguza malalamiko yaliyowasilishwa, endapo itabainika umehusika kwa namna moja ama nyingine, hatua itakayofuata ni kufukuzwa”, amesema Kamwelwe.
Aidha, Kamwelwe amewataka TEMESA kuhakikisha kuwa wanatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia zinazokuwa kwa kasi hususani katika mitambo na magari yanayoagizwa na Serikali.
Kuhusu suala la vipuri Kamwelwe amesistiza kuwa wahakikishe vipuri hivyo vina ubora wa kutosha na vinanunuliwa katika manunzi ya pamoja kwa mtengenezaji na endapo itatokea dharura manunuzi hayo yanaweza kufanyika kwa wasambazaji wa jumla hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Kamwelwe amekutana na Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutoka mikoa yote nchini na kuwataka wahakikishe wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara kuu ili kuepukana na kukatika kwa mawasiliano katika barabara hizo.
Amefafanua kuwa ukaguzi huo uhusishe mifumo ya maji kwenye barabara ikiwemo madaraja, makalvati na mifereji hususani kwenye mikoa ambayo inapata mvua juu ya wastani.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya barabara ikiwemo barabara kuu, hivyo ni lazima tuilinde na kuwa makini na miundombinu hii, meneja hakikisha unakagua miundombinu hii majira yote ya mwaka na kuhakikisha unafanya ukaguzi wa kutosha na kujiridhisha kila mvua inaponyesha”, amefafanua Kamwelwe.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amemhakikishia Waziri huyo kuwa watajipanga ili kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote kwani ndio njia kuu ya usafiri na usafirishaji na hivyo kukuza uchumi wa Tanzania na nchi jirani.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, amesema kuwa Wakala unaendelea kununua vipuri halisi kwa wingi kutoka kwa wauzaji wa jumla na viwandani ili kupata vipuri bora na kwa bei ya soko.
Ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2019 Wakala umetengeneza magari yanayofikia 12,376 ikilinganishwa na magari 10,263 yaliyotengenezwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2018 sawa na ongezeko la asilimia 21 ikiwa ni manufaa ya kutekeleza agizo la Mhe. Waziri la kusitisha kupeleka magari katika karakana binafsi kama hapo mwanzo.
Waziri Kamwelwe amekutana na kufanya kikao na watendaji hao kutoka TANROADS na TEMESA kutoka mikoa yote ikiwa ni kukumbushana kuhusu utendaji wa kazi zao kwa weledi na ufanisi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawsiliano
No comments:
Post a Comment