VIZIMIA MOTO, FIRE EXTINGUISHER |
JE, NI KOSA KUTOKUWA NA KIZIMIA MOTO (FIRE EXTINGUISHER) KWENYE MAGARI YASIYO YA ABIRIA?
KWA mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Tanzania sura ya 168, jibu ni HAPANA
Sasa tuangalie kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kanuni zake mbalimbali.
Hapa pia jibu ninalotanguliza ni HAPANA, na nitajenga hoja zenye sababu (reasoned arguments). Lakini kwa kusema HAPANA, sisemi sio muhimu wala kwamba hakihitajiki. Ila nasema HAPANA kwa kuzingatia kanuni za jumla za sheria (general principles of law) kwamba mtu hawezi kuadhibiwa ikiwa hakuna sheria mahsusi aliyoivunja. Na hapa tunazungumzia kosa, kwa maana ya kutotimiza matakwa ya sheria na hivyo kustahili adhabu.
Hoja zenye Sababu ya Kuafiki jibu la HAPANA
Hakuna kanuni yoyote katika Kanuni ya Ukaguzi na vyeti, ya 2008 yaani THE FIRE AND RESCUE FORCE (SAFETY INSPECTIONS AND CERTIFICATES) wala marekebisho yake ya mwaka 2012, yaani THE FIRE AND RESCUE FORCE (SAFETY INSPECTIONS AND CERTIFICATES) AMENDMENT REGULATIONS,2012, wala sharia mama inayoanzisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inayoweka bayana kwamba kutokuwepo na kizimia moto kwenye gari ni kosa la kutozwa faini au kifungo.
Kinachotamkwa na kanuni ya 5(1) ni hitaji la gari kukaguliwa usalama wake dhidi ya majanga ya moto, wakati kanuni ya 5(2) inahusu adhabu kwa kutokagulisha gari. Aidha, kanuni ya 6(1) ikisomwa pamoja na kanuni ya 6(3)(b) inataka mmiliki au mwendeshaji wa gari la abiria ndiye awe na kifaa cha kuzimia moto na kukidhi vigezo wakati anasubiri kupewa cheti.
Aidha, kanuni ya 16 haiwezi kutumika hadi pale itakapotokea kuna kipengele kinaweka hitaji la kuwa na kifaa Fulani au kinatamka jambo Fulani kuwa kosa, lakini kipengele hicho cha sharia hakitaji adhabu. Hapo sasa kanuni ya 16 inaweza kutumika.
Hata hivyo, ili upewe cheti cha usalama wa gari dhidi ya majanga ya moto (Fire Safety Certificate) afisa wa zimamoto lazima akague na kujihakikishia yafuatayo:
(a) Milango ya dharula kama ipo na inafanya kazi
(b) Vizuia moto (Fire retardants) kama zipo na zinafanya kazi. Fire retardants hizi ni pamoja na kapeti za gari, paa la gari kwa ndani, na kizimia moto (fire extinguisher)
(c) Mfumowa umeme kama upo vizuri
(d) Mfumo wa mafuta wa gari kama upo vizuri
(e) Abaini iwapo mwenye gari ana elimu ya kuhusu moto
Na hakuna popote, kwenye fomu ya ukaguzi wala kwenye kanuni ya 5(1) inayompa mamlaka afisa za Zimamoto kukagua chombo cha moto, panapoonesha kuwa kutokuwa na kizimia moto ni kosa.
Kosa pekee linalosemwa ni “ kutopelekwa gari kukagulishwa”. Utaniuliza swali, sasa katika ukaguzi wa vipengele (a) hadi € hao akikuta mfano mfumo wa umeme ni mbovu sio kosa? Jibu ni sio kosa, bali madhara yake ni kunyimwa Fire Safety certificate. Atakuekeza ukarekebishe ndipo uje upewe. Hivyo ieleweka kwamba kisheria kutopeleka gari kukaguliwa sio sawa na kutokuwa na kimojawapo kinachojitajika katika ukaguzi.
Ni imani yangu makala hii ndefu itakuwa imekuongezea maarifa na kuweza kutenda kwa weledi zaidi au kutii sheria bila shuruti kwa hiyari zaidi. Hata hivyo, natoa mwito kwa wenye magari kuendelea kuwa na fire extinguisher tusisubiri hadi sheria, kwani ni kifaa muhimu kwa maokozi, japokuwa sio kosa kuwa nacho.
RSAadmin1
RSA Tanzania
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu sote.
No comments:
Post a Comment