Mkutano ukiendelea kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjoberg, ambapo wamekubaliana kuendelea na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo, jijini Dodoma.
SERIKALI imesema kuwa Ushirikiano mpya kati ya Tanzania na Sweden unatakiwa kujikita katika biashara na Uwekezaji kuliko ushirikiano wa misaada pekee ili kuisaidia Tanzania kuwa na uchumi endelevu na shirikishi kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Bw. Anders Sjoberg.
Dkt. Mpango alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden inabidi uwe na uhalisia kwa kuisaidia Tanzania kutoendelea na utegemezi na badala yake kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo, kwa kuwa kiwango cha sasa bado hakitoshelezi.
“Tanzania imejipanga kuondoa utegemezi kwa kuhakikisha inakuwa na uchumi wa viwanda unaotegemea malighafi za ndani na lengo hili haliwezi kufikiwa iwapo hakuna rasilimali watu yenye ujuzi, hivyo tunahitaji mafunzo na vifaa hususani kwenye elimu ya ufundi stadi ili kuweza kupata watu wenye ujuzi wa kuendesha uchumi huo wa viwanda utakaoongeza thamani ya bidhaa”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa anapozungumzia uchumi au maendeleo shirikishi haiwezekani kuacha nyuma Sekta ya Kilimo ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha malighafi za viwandani na inahusisha watanzania wengi na kueleza kuwa katika eneo hilo kuna fursa ya uwekezaji kwenye mbegu bora na dawa.
Pia kuna fursa katika Sekta ya uvuvi katika Maziwa na Bahari ambapo kwa sasa zana zinazotumika ni duni na hazikidhi mahitaji na kuiomba Sweden kuangalia uwekezaji katika maeneo hayo.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye rasilimali watu ili kupata wataalamu wabobezi ambao ujuzi wao utakuwa unabadilika kulingana na mabadiliko ya mahitaji, hasa katika Sekta za Afya, Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na zingine ambazo zinamchango mkubwa kiuchumi.
Alieleza kuwa Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa katika Sekta ya Afya hasa katika Matibabu ya ugonjwa wa moyo, hapo awali Serikali ilikua inatumia fedha nyingi kugharamia matibabu nje ya nchi lakini kwa sasa kuna Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo inatoa tiba hiyo hapa nchini, msaada unaohitajika ni kuongeza wataalam wabobezi ambao wataongeza kasi ya utoaji huduma hizo kwa wananchi.
Dkt. Mpango alisema kuwa katika uwekezaji kwenye ujuzi, Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na kusababisha ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za Sekondari na elimu ya juu, hivyo ni vema Sweden ikaangalia namna ya kuwekeza kwenye Sekta hiyo ili kuweza kupata rasilimali watu yenye ujuzi wa kutosha kukabiliana na mabadiliko yanayojitokeza Duniani.
Aidha alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya jukumu lake la kuhakikisha Sekta binafsi inaimarika na kuchangia pato la taifa kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na pia imeweka majukwaa mbalimbali ya majadiliano na wawekezaji na wafanyabiashara kuhusu masuala ya fedha jambo lililosababisha sekta hiyo kukua na kuinufaisha Serikali.
Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg, ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za maendeleo na akaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali kwa kusaidia katika miradi ya maendeleo ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji na kuhakikisha sekta binafsi inakua.
Nchi ya Sweden ilianza kushirikiana na Tanzania kuanzia miaka ya 1960 na kwa sasa Mpango Mkakati wa ushirikiano unaotekelezwa ulianza mwaka 2013 na kumalizika mwaka 2019, miradi ambayo inaendelea kutekelezwa ni pamoja na miradi ya Nishati, tafiti, elimu lakini pia msaada wa kibajeti.
No comments:
Post a Comment