Wataalam wa afya ya umma wamekuwa wakitoa ushauri ili kujaribu kuzuia maambukizi ya virusi hivi. |
KISA cha kwanza cha virusi vya corona Kimethibitishwa nchini Kenya. Waziri wa afya nchini humo Mutahi Kagwe amethibitisha kisa hicho katika tangazo alilolitoa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.
Bwana Mutahi amesema kwamba mtu mwenye maambikizi ya virusi vya Corona alithibitishwa kuwa ana maambukizi hayo Alhamisi usiku.
Waziri huyo amesema kwamba kisa hicho ni cha kwanza kuripotiwa nchini Kenya tangu kuzuka kwa mlipuko huo mjini Wuhan nchini China.
Kisa hicho ni cha raia wa Kenya aliyewasili nchini humo kutoka Marekani kupitia mjini London nchini Uingereza tarehe 5 mwezi Machi 2020.
Aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika maabara ya wizara ya afya nchini Kenya.
Hatahivyo waziri huyo amesema kwamba mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke yuko katika hali njema na kwamba viwango vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida.
''Tarahe 5 mwezi Machi aligunduliwa kuwa na virusi hivyo katika maabara ya serikali lakini sasa viwango vyake vya joto vimeshuka na kuwa vya kawaida anakula vizuri lakini hawezi kutolewa hadi virusi hivyo vitakapokwisha mwilini.'', amesema Waziri Kagwe.
Wakenya wametakiwa kutokua na hofu
Waziri huyo amewataka Wakenya kuwa watulivu na kuacha wasiwasi.
Amesema kwamba serikali ya Kenya kupitia wizara ya afya itaendelea kuimarisha mikakati ili kuhakikisha kwamba hakuna usambazaji wa virusi hivyo zaidi.
Kamati ya dharura ilioanzishwa ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona itaendelea kutoa muongozo ili kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Amewahakikishia Wakenya kwamba Kenya imejiandaa vilivyo kukabiliana na virusi hivyo tangu kisa cha kwanza kitangazwe nchini China, akiongezea kuwa serikali itatumia raslimali zake zote kukabiliana na janga hili..
Amesema kwamba tayari serikali imetambua maeneo yote ambayo muathiriwa alipitia kabla ya kufanyiwa vipimo.
''Mtu anapoambukizwa huhisi maumivu machache na kupona kwa urahisi lakini virusi hivyo vinaweza kuwaathiri zaidi watu wengine hususan wazee na wengine wenye magonjwa sugu''.
-BBC
No comments:
Post a Comment