Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bw. Alex Mubiru, wakipongezana (kwa tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa kutoshikana mikono) baada ya kusaini mikataba ya mkopo nafuu pamoja na msaada wa kibajeti wenye thamani ya shilingi trilioni 1.14 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma, Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Hororo/Lungalunga- |
Na Ramadhani Kissimba, Dar es Salaam
TANZANIA na Benki ya Maendeleo ya Afrka (AfDB) zimetiliana saini mikataba ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Milioni 495.59 (sawa na shilingi trilioni 1.14) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ya maendeleo ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Msalato, Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo – Hororo/Lungalunga – Malindi kwa kiwango cha lami pamoja na msaada wa kibajeti kwa ajili ya kuendeleza utawala bora na sekta binafsi.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini mikataba hiyo kwa niaba ya Serikali, Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amesema mradi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Msalato ulioko mkoani Dodoma umepata dola za Marekani milioni 271.63, mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Hororo na Lungalunga hadi Malindi umepatiwa dola milioni 168.76 huku program ya utawala bora na kuendeleza Sekta Binafsi ukipata msaada wa dola milioni 52.2.
“Mkopo huu wenye masharti nafuu umetolewa na Benki hiyo kupitia dirisha la Benki ya Maendeleo (ADB Window) kiasi cha dola milioni 198.63, kiasi cha dola za Marekani milioni 246.96 kimetoka dirisha la Mfuko wa Maendeleo wa Benki (ADF Window) na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 50 zimetoka katika Mfuko wa Serikali ya China unaosimamiwa na Benki hiyo (Africa Growing Together Fund)” alifafanua Bw. James
Alisema mkopo huo utaongeza kiasi cha fedha ambacho kimetengwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi nchini Tanzania, kutoka dola za Marekani bilioni 1.03 (takribani sh. trilioni 2.37) hadi dola za Marekani bilioni 1.47 (takribani shilingi trilioni 3.77), hivyo kuifanya sekta ya uchukuzi kunufaika kwa asilimia 70 ya misaada na mikopo yenye thamani ya Jumla ya dola za Marekani bilioni 2.1.
“Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na ujenzi wa kipande cha barabara ya Bagamoyo – Pangani kwa kiwango cha lami itasaidia Serikali kuziba pengo la miundombinu na kuchochea kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kupunguza umasikini na kuongeza utalii” alisema Bw. James
Bw. James katika hotuba yake alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kudumisha uhusiano mzuri kati ya AfDB na Serikali, uhusiano ambao umefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya uchukuzi.
Aliwatoa hofu watanzania kwamba Serikali inakopa kwa umakini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati na kuwataka wapuuze maneno ya watu wanaodai Serikali inakopa mno na kwamba Serikali inakopesheka na bado itaendelea kukopa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa AfDB Tanzania, Dkt. Alex Mubiru amesema uhusiano wa Benki na Serikali ya Tanzania ni wa muda mrefu na kupitia uhusiano huo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuchochea ukuaji wake wa uchumi na Sekta binafsi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale, amesema miradi miwili ya Ujenzi wa Barabara na Daraja la Mto Pangani utagharimu shilingi bilioni 408, na katika fedha hizo Serikali ya Tanzania itachangia kiasi cha shilingi bilioni 58.7 na itatumia shilingi bilioni 10.3 kuwalipa fidia wananchi wanaliotwaliwa ardhi yao kupisha ujenzi wa mradi huo.
Bw. Mfugale aliongeza kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao utakuwa na urefu wa kilomita 3.6 kwa kuanzia awamu ya kwanza, utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka, na utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege aina ya dreamliner 17 kwa wakati mmoja na pia inaweza kuhudumia ndege kubwa aina ya Airbus A380 ikihitaji kutua kwa dharura.
Bw. Mfugale amesema kuwa mradi huo utagharimu jumla ya Shilingi bilioni 757.78 na kati ya hizo Serikali ya Tanzania itachangia kiasi cha shilingi bilioni 133.3, ambapo wananchi watakaopisha ujenzi wa uwanja huo watalipwa fidia ya takribani shilingi bilioni 15.42.
Naye katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Elius Mwakalinga ameahidi kuwa fedha zilizotolewa zitatumika kwa mujibu wa matumizi yaliyopangwa na kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za ajira zitakazotolewa wakati wa ujenzi wa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment