DK. SHEIN : KUNA UMUHIMU WA KUTIZAMA UPYA SHERIA ZINAZOSIMAMIA MWENENDO WA USALAMA WA CHAKULA NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 17 February 2020

DK. SHEIN : KUNA UMUHIMU WA KUTIZAMA UPYA SHERIA ZINAZOSIMAMIA MWENENDO WA USALAMA WA CHAKULA NCHINI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu wa kutizama upya sheria zinazosimamia mwenendo wa usalama wa chakula nchini, ili kuondokana na malalamiko mbali mbali ya wafanyabiashara.

Dk. Shein ametowa ufafanuzi huo leo February 17, 2020, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi ya Wizara ya Afya, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, 2019, hafla iliyofanyika Ikulu mjini hapa.

Alisema kuna umuhimu kwa Uongozi wa Wizara hiyo kuziangalia upya sheria zinazosimamia usalama wa chakula, hususan katika suala zima la ukaguzi wa bidhaa zinazotoka na kuingia nchini,      kwa kigezo cha kuwepo malalamiko kutoka kwa wafanyabaishara juu ya tozo wanayolipa kugharamia   ukaguzi huo.

Alisema wafanyabishara wamekuwa wakilalamikia gharama hizo, kwa kigezo kuwa dhima ya kuthibitisha ubora wa bidhaa  uko mikononi kwa Serikali badala ya wao kubebeshwa mzigo huo.

Alisema  pamoja na sheria zilizopo kuwa na uwiano katika nchi nne za Afrika Mashariki, kuna umuhimu wa kuzipitia upya kwa kuzingatia kuwa Serikali ndio yenye dhima katika kufanya utafiti na kupata matokeo.

Dk. Shein alieleza wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa utitiri wa taasisi za uchunguzi, jambo linaloongeza urasimu.

Alieleza kuwa mbali na taasisi hizo kuongozwa  na sheria yake kila moja, kuna umuhimu wa viongozi kukaa pamoja ili kuwa na mfumo maalum wa utoaji wa tozo moja.

Alisema Serikali haiwezi kupuuza malalamiko ya wafanyabiashara hao na kubainisha kuwa itafanya juhudi za kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuondokana na  malalamiko.

Aidha,   aliitaka Wizara hiyo kujikita katika suala la kusomesha na kuwaendeleza  wafanyakazi wake katika nyanja tofauti, ikiwemo za Injinia na nyengine zenye upungufu ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na program maalum ya mafunzo , itakayotoa fursa kwa wafanyakazi kusoma ndani na nje ya nchi, hatua aliyobainisha itaiwezesha Wizara kuwa na wataalamu wa kutosha katika kipindi kifupi.

Sambamba na hilo Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanya tafiti mbali mbali , ikiwa ni hatua muafaka katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazojitokeza.

Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha huduma zote za Maabara zinafanyika ndani ya Hospitali za Serikali badala ya kufanyika taasisi zanje, kwa kigezo kuwa Serikali imekuwa ikitenga kiwango kikubwa cha fedha na kubainisha kuwa huduma za maabara ndio msingi wa matibabu.

Aliushauri uongozi wa Wizara hiyo kuendleea kuviimarisha vituo vya Afya , hususan vile vilioko vijijini kisiwani Pemba kwa kuvipatia nyenzo, vifaa tiba na dawa, ili wagonjwa wasikimbilie hospitali ya Abdalla Mzee.

Aidha, aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubwa inazoendelea kuchukuwa katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria, sambamba na kupunguza kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka asilimia 0.6 hadi kufikia asilimia 0.4.

Vile vile aliipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa mpango mzuri wa taarifa yake, pamoja na hatua mbali mbali ilizozichukuwa kuimarisha huduma za Afya hapa nchini.

No comments:

Post a Comment