WANACHUO KIKUU HURIA MKOANI SINGIDA WAJIPANGA KWA UFUGAJI NYUKI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 29 January 2020

WANACHUO KIKUU HURIA MKOANI SINGIDA WAJIPANGA KWA UFUGAJI NYUKI

 Rais wa Umoja wa Wafugaji Nyuki Nchini, Philemon Kiemi, akizungumza na viongozi wa serikali ya wanafunzi na Jumuiya ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania  tawi la Singida jana.
 Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria, tawi la Singida, Nassoro Matulanga, akizungumza muda mfupi kabla ya hafla ya kupokea msaada wa mizinga 10 ya kisasa ya kufugia nyuki kwa niaba ya serikali ya wanafunzi wa chuo hicho.
 Waziri wa Mipango na Fedha, Frederick  Ndahani akizungumza kwenye tukio hilo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Kituo, Chuo Kikuu Huria, Tawi la Singida, Bernard Komba, akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Mwonekano wa mizinga ya kisasa iliyotolewa na Syeccos kama msaada kwa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria, tawi la Singida.
 Washiriki wakifuatilia tukio hilo.
 Hafla ikiendelea.
Baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi wakifuatilia hotuba mbalimbali. 

Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI ya Wanafunzi Chuo Kikuu Huria Tawi la Singida, imepokea msaada wa mizinga kumi ya kisasa ya kufugia nyuki, yenye thamani ya shilingi milioni mbili, ikiwa ni mwendelezo wa mkakati uliopo wa wanachuo hao nchini kote kuhakikisha wanaanza kubuni na kuibua miradi yenye tija, itakayosaidia kuinua kipato cha mtu mmoja-mmoja na taifa kuelekea uchumi wa kati.


Akizungumza kabla ya kupokea mizinga hiyo, kutoka Taasisi ya ‘Youth Enterpreneurs and Consultants Cooperative Society (Syeccos), kupitia kijiji cha Nyuki Kisaki, Waziri wa Mipango na Fedha wa Tawi la chuo hicho mkoani hapa, Frederick  Ndahani, alisema mradi huo unakwenda kuinua kipato cha wanachuo katika kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo upatikanaji wa ada.
Ndahani ambaye pia ni Kaimu Afisa Vijana wa Mkoa, alisema kwa sasa serikali tayari imewakabidhi eneo la Mwankonko lenye ekari zipatazo 1663, ambalo anaamini kila mwanachuo atatumia fursa hiyo kuwekeza kwenye mradi wowote wa kiuchumi atakaoubuni, lakini pia hata mizinga hiyo waliyopokea kama msaada wanatarajia kuipeleka kwenye eneo hilo.
“Niwasihi wanachuo wenzangu na serikali za wanafunzi kwenye vyuo vingine nchini badala ya kukaa na kufikiria kuanzisha migomo sasa tuanze kubuni namna ya kuanzisha miradi yenye tija kwa manufaa yetu na taifa kwa ujumla, ni fursa kwa mwanachuo yeyote mwenye mzinga wake alete kwenye eneo letu,” alisema Ndahani.
Alisema mbali ya mkakati huo wa kufuga nyuki, pia serikali ya wanafunzi hao kwa kushirikiana na Kampasi ya Makao Makuu ya chuo hicho wanakusudia kuwa na kiwanda cha kuchakata asali ndani ya mda mfupi ujao, azma hasa ni kuwafanya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa asali nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Tawi hilo, Nassoro Matulanga, alisema kwa sasa kama sehemu ya jumuiya ya chuo hicho wapo katika kipindi cha kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Chuo Kikuu Huria, ikiwemo kutekeleza miradi mbalimbali kama sehemu ya mageuzi ya kiuchumi.
“ Tukio la leo ni tukio kubwa linaloingia kwenye historia ya chuo, msaada huu tutautumia kikamililifu kwa tija na manufaa ya wanachuo… kwa kuzingatia kwa sasa tumekusudia kuwa na miradi mingi itakayoinua uchumi kama sehemu ya kuchangia juhudi ya nchi katika kuelekea uchumi wa kati,” alisema Matulanga.
Naye, Rais wa Umoja wa Wafugaji Nyuki nchini, Philemon Kiemi, aliwataka wanachuo hao kuwa chachu ya mabadiliko ya kifikra katika muktadha chanya wa maendeleo endelevu ya kiuchumi kupitia elimu na maarifa wanayoyapata.
“Andikeni papers (maandiko ya miradi) mbalimbali za namna ya kutafuta changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta ya nyuki nchini, sisi wasomi tunafahamu eneo hili kuna resources za aina nyingi, una ardhi unataka hela njoo tukuonyeshe, una mizinga unataka hela njoo tukuonyeshe…usikae bure  fanya kitu,” alisema Kiemi, na kuongeza:
“Tunaamini elimu hii ya ufugaji itasaidia watanzania wengi kupitia chuo hiki, mizinga hii tunayowakabidhi ni ishara ya mwanzo wa ushirikiano, msisite kutuita au kutushirikisha kwa lolote, mkituhitaji wakati mnataka kutoa elimu tutakuja kushirikiana, na wakati mnataka kuipeleka shamba tutakuwepo kushauriana,” alisema.

No comments:

Post a Comment