KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA MIKOA YA MRADI BOMBA LA MAFUTA ZASHAURIWA KUUWEKA MRADI KWENYE MPANGO WA KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MAAFA. - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 29 January 2020

KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA MIKOA YA MRADI BOMBA LA MAFUTA ZASHAURIWA KUUWEKA MRADI KWENYE MPANGO WA KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MAAFA.



Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akisisitiza umuhimu wa Mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa ya Mikoa linakopita Bomba la Mafuta, kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri Mradi huo, wakati alipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa .

Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto, akimueleza Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe umuhimu wa Mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa wa Mkoa huo linakopita kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri Bomba la Mafuta ,  wakati walipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa.

Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe na  Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto, wakisoma Jiwe la uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la mafuta, wakati walipotembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa na kushauri mipango ya menejimenti ya maafa ya mikoa linakopita bomba hilo  izingatia athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri mradi huo.


OFISI ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa Maafa katika  mikoa 8 na vijiji 184  vinavyopatikana   katika wilaya 24 zilizopo katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, ambapo Mradi wa Bomba la Mafuta utatekelezwa kuuweka Mradi huo katika Mipango yao ya kujiandaa na kukabiliana na Maafa ili kuhakikisha mradi huo hauthiriwi na majanga yanayoweza kutokea.

Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha majukumu ya  kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika, Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji  wilaya au mkoa, pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika.

Akiongea mara baada ya kutembelea eneo la kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga ambapo utekelezaji wa Mradi huo utatekelezwa, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amefafanua kuwa Kamati za maafa zinalo jukumu la kuchukua tahadhari ya namna ya kuhakikisha majanga yanayoweza kuuathiri mradi huo yanakuwa katika mipango yao ya menejimenti ya maafa ili faida zitakazotokana na utelelezaji wa mradi huo zinakuwa endelevu.

Kwa upande wake,  Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Noel Kazimoto ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa watanzania hivyo ni dhahiri kuwa eneo la Chongoleani litakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zitakuwa zikiendeshwa, kwa kuwa wananchi ni wadau wa menejimeti ya maafa kupitia kamati za menejimenti  za maafa kuanzia ngazi ya vijiji, wataendelea kuelimishwa juu ya majanga  yanayoweza kuuathiri mradi huo ili waweze kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Tovuti rasmi ya Kampuni inayojenga mradi huo, East African Crude Oil Pipeline www.eacop.com. Kampuni hiyo inabainisha kuwa wanao mpango unaohakikisha utelezaji wa mradi huo unazingatia majanga na maafa wakati wa kupanga, kujenga na kuendesha Bomba, ambapo Mpango huo unahakikisha kwamba, katika tukio la dharura linaloweza kutokea, hatua za haraka, zinachukuliwa.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi unatekelezwa kwa ubia wa ujenzi na uendeshaji kwa kushirikisha kampuni za Total ya Ufaransa, CNOOC ya China, Tullow ya Uingereza na Serikali za Tanzania na Uganda. Mafuta ghafi yatasafirshwa kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania. Mradi wa Bomba hilo una umbali wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 298 zitakuwa nchini Uganda, na kilometa 1,147 zitakuwa nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment