UJENZI OFISI NA STUDIO ZA ZBC PEMBA UKAMILIKE KWA WAKATI-MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 20 January 2020

UJENZI OFISI NA STUDIO ZA ZBC PEMBA UKAMILIKE KWA WAKATI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na watumishi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Studio za Shirika hilo, wilayani Chakechake Kusini Pemba. Januari 17, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa ofisi na studio za Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na kuwaagiza wahusika wahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati.

Ametoa maagizo hayo Januari 19, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa ZBC na wananchi baada ya kukagua mradi huo uliopo katika wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 1.4.

Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa ofisi na studio za ZBC kisiwani Pemba kutaboresha sekta ya TEHAMA, hivyo kuwawezesha wananchi kupata taarifa za ndani na nje kwa wakati. “Tunaimarisha ZBC ili kila mtu aweze kupata habari kwa wakati.”

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza watumishi wa ZBC waongeze ubunifu katika utayarishaji wa vipindi vyao pamoja na kutenga muda kwa ajili ya kutembelea mashirika mengine ya utangazaji kwa lengo la kujifunza.

Kabla ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuifanyia maboresho studio yake ya kurushia matangazo ya Pemba wananchi wa kisiwa hicho walikuwa wanakaa hadi wiki moja bila ya kusikia habari zinazohusu kisiwa hicho. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali kwa sababu imejipanga katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya, elimu kwa Watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee kudumisha amani na utulivu na wasikubali kushiriki katika matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kuwa hayana tija.

“Amani, utulivu na mshikamo tulionao nchini haujaja kwa bahati mbaya bali umeasisiwa na viongozi wa kwanza wa Taifa letu hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Sheikh Abeid Aman Karume hivyo ni muhimu tukawaenzi waasisi wetu kwa kuimarisha amani.”

Awali,Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba sita za Askari Polisi zinazojengwa katika eneo la Mfikiwa wilayani Chakechake. Kati ya nyumba hizo sita, tano tayari zimekamilika na zinatumika. Nyumba moja ipo kwenye hatua za kukamilika. 

Kadhalika, Waziri Mkuu alishuhudia matofali 52,000 yaliyopo eneo hilo na kuiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani itenge fedha za kugharamia ujenzi wa nyumba sita nyingine zinazokadiriwa kugharimu kiasi cha sh. 35,000,000 kwa nyumba moja iwapo zitajengwa kwa mfumo wa force account.

No comments:

Post a Comment